Habari za Punde

Balozi Seif mgeni rasmi ufungaji wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili la Bakiza.

  Baadhi ya Wajumbe wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili na Bakiza wakifuatilia matukio ya ufungaji wa Kongamano hilo ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
 Wahadhiri wa Vyuo Vikuu mbali mbali Duniani wanaofundisha Lugha ya Kiswahili wakiwa sehemu ya Wana Kongamano hilo la Pili la Kiswahiuli lililofanyika Visiwani Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziubar akimkabidhi zawadi Profesa Baby Masamba baada ya kulifunga Kongamano la Kimataifa la Kiswahili la Bakiza
 Dr. Shani Omar hakua m,bali kupokea zwadi yake kutoka kwa Balozi kutokana na mchango wake wa kukisomesha Kiswahili lugha fasaha na inayopenda na Walimwengu wengi.
 Dr. Shahal Ahmed akikabidhiwa zawadi kama walivyopewa wenzake kutokana na michango yao ya kukieneza Kiswahili ndani ya Mgongo wa Dunia.

 Mhadhiri Legere kutoka Nchini Austria akikabidhiwa zawadi kutokana na mchango wake mkubwa wa kukisomesha sambamba na kukisambaza Kiswahili Nchini mwake
 Mhadhiri Makoto Promoto kutoka Nchini Japan akifurahia zawadi yake aliyokabidhiwa na Balozi Seif baada ya kushiriki Kongamano la Kiswahili la Bakiza.
  Balozi Seif kati kati awaliokaa akiwa katika picha ya pamoja na Wahadhiri pamoja na washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili la Bakiza lililofanyika Zanzibar kwa mara ya Pili.

 Balozi Seif akifurahia machapisho mbali mbali ya Vitabu yaliyochapishwa na Wahadhiri pamoja na watunzi wa Vitabu vya Kiswahili kutoka pembe zote za Dunia.
Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahilio Zanzibar Dr. Mohamed Seif  Khatib, Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nd. Omar Hassan Omar, na kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Mjini Bibi Marina Thomas.
Balozi Seif  Kushoto akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahilio Zanzibar {BAKIZA} Dr. Mohamed Seif  Khatib baada ya kulifunga Kongamano la Kimataifa la Kiswahili la Bakiza.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ni ukweli usiopingika kuwa Waswahili wasipokuwa na jitihada za kuipa uhai Fasihi kwa kuiepusha kuwa chapwa ipo hatari  kwa hazina hiyo ya miaka mingi kupotea kama moshi.
Alisema Kiswahili ni Lugha nzuri sana na yenye ladha tamu inayopaswa kuendelezwa kwa vile ni nyenzo ya kuchangia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanayokwenda kwa kasi kubwa.
Akilifunga Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili la Bakiza lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idissa Abdulwakil Mnazi Mmoja Balozi Seif alisema Wataalamu wa Lugha ya Kiswahili wana kazi ya kupunguza changamoto zinazojitokeza katika Lugha hiyo katika muktaza wa matumizi yote.
Balozi Seif alisema hiyo si kazi rahisi ikizingatiwa kusambaa kwa mifumo mingi ya mawasiliani ikiwemo Mitandao ya Kijamii kama vile Vaiba, Twita, Wasap, Imo na mifumo mengine ambayo inakuwa vigumu kuipitia na kuihakiki kwa kuwa kazi yenyewe inahitaji muda mwingi na utulivu.
Alilitaka Baraza la Kiswahili {BAKIZA} kuchukuwa jitihada za makusudi kipindi kijacho kwa kuandaa Maonyesho ya Vitabu vya Kiswahili vyenye hadhi ya Kimataifa ili wapenzi wa Lugha hiyo kutoka kila pembe ya Dunia  wafike Zanzibar kujionea wenyewe na kufaidika na Lugha hiyo adhim.
Balozi Seif alieleza kwamba Maonyesho ya Vitabu yatasaidia kujenga Utamaduni wa kupenda kusoma Vitabu kama ilivyoainishwa na wasomi mbali mbali Duniani wakitolea mfano nyumba isiyo na Vitabu ni sawa na chumba kisicho na dirisha.
Alitahadharisha kwamba Utamaduni huo usipoendelezwa kwa usimamizi wa Wataalamu na wasahili wenyewe  upo uwezaekano wa kuwa na Taifa la Vijana wanaotegemea kupata Elimu yao kupitia mitandao ya Kijamii ambayo kwa bahati mbaya imetawaliwa zaidi na mambo ya starehe pamoja na uzushi mwingi.
Alisema Kitabu kinaweza kuwa ni mshauri na nguzo ya kujitegemea katika kupata maarifa mapya yatakayoongeza umahiri wa Mtu ambae akili yake inahitaji matunzo, sawa na bustani inayohitaji kurutubishwa na kupaliliwa ili inawiri vyema.
“ Kusoma Vitabu ni kuirutubisha akili na kuiongezea maarifa yanayofaa. Hivyo ni muhimu kuvisoma vitabu vya aina mbali mbali kama vile Vitabu vya Saikolojia, Sarufi, Fasihi, Sayansi, Falsafa, Historia, Uchumi pamoja na Siasa”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba ni makosa kudhani kuwa kusoma Vitabu inawahusu Wanafunzi na Walimu pekee ambapo baadhi ya wakati wakifikiria ni kopoteza muda.
Balozi Seif alieleza kwamba  kila Mtu anapaswa kusoma Vitabu ili apate faida ya kuongeza ujuzi wa ziada katika maisha, kukuza mawasiliano ndani ya Jamii, kuhamasika katika kufanya mambo mazuri, kuongeza uwezo na umahiri wa kuandika hasa kwa wanaopenda kutunga na kuandika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliitaka Jamii ya Kiswahili kuelewa kwamba mahitaji ya kujifunza Kiswahili Duniani hivi yameonyezeka kutokana na Lugha  hiyo kuzungumzwa katika Mataifa mbali mbali Duniani.
Alisema Lugha ya Kiswahili kwa sasa tayari inafundishwa ndani ya Vyuo Vikuu Tofauti Ulimwenguni ikiwa ni miongoni mwa Biashara kubwa ya Kimataifa. Hivyo Waswahuli wasipokuwa na jitihada ya kuzitafuta fursa zinazozalishwa na Kiswahili wanaweza baadae kubakia Nyuma.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Mataifa mengi Ulimwenguni yanahitaji Wataalamu wa Kiswahili ambao kwa kweli Wataalamu hao ni Waswahili wenyewe wanaopaswa kuamka hasa Vijana kuichangamkia fursa hiyo muhimu na adhimu iliyopo.
Alisisitiza dhima ya Waswahili kukiendeleza, kukienzi na kukitunza Kiswahili ili Zanzibar ionekane kweli ndio chimbuko la Lugha ya Kiswahili na tayari hivi sasa kishakuwa tayari kutumika katika Mikutano ya Kimataifa kama vile Sadc, AU na hata Umoja wa Mataifa.
“ Kiswahili kina ladha ya pekee ndiyo maana hata Mabalozi wa Nchi za Nje waliopo Tanzania wanajifunza Kiswahili kwa kasi kubwa”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Ameipongeza Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Baraza la Kiswahili, Watendaji, Waandaaji wa Kongamano pamoja na Wahadhiri kutoka ndani na Nje ya Nchi kwa kushiriki Mijadala na Maonyesho ya Vitabu yaliyosaidia kuimarisha uhimili wa Lugha ya Kiswahili inayozidi kutanuka Ulimwenguni kote.
Mapema Katibub Mkuu Wizara  ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar Nd. Omar Hassan Omar aliiomba Jamii ya Waswahili kuwa na Utamaduni wa Kusoma, Kuandika na Kuchapisha Vitabu ili kuwapa ufahamu wa Lugha Waswahili.
Nd. Omar alisema katika kulifanikisha hilo aliwataka Wataalamu wa Lugha ya Kiswahili Kuutumia Ujumbe wa Mwaka huu unaosema Kiswahili Fahari yetu kwa Maendeleo ili kwenda sambamba na azma hiyo muhimu.
Katibu  Mkuu huyo wa Wizara  ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar alieleza kwamba Wazanzibari walio wengi wanaendelea kufarajika na mfumo wa uendelezaji wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili Visiwani Zanzibar penye chimbuko halisi la Lugha hiyo.
Wanakongamano hao wametoa Mapendekezo 25 yaliyoainishwa kufuatia Majadiliano ya kina yaliyoshirikisha Magwiji wa Lugha hiyo muhimu inayosimamia na kulinda Utamaduniwa Mswahili.
Miongoni mwa Maazimio hayo ni pamoja na wazo la kuanzishwa kwa mfuko wa Uchapishaji utakaotoa fursa ya kusaidia Waandishi wachanga wa Vitabu, Baraza la Kiswahili kutangaza kazi zake ndani na Nje ya Nchi pamoja na uwepo wa siku Maalum ya kukumbukwa Waandishi wa Kiswahili Zanzibar ili Jamii ielewe Mchanga wa Waasisi hao wa Lugha.
Azimio jengine muhimu ni lile la Kuitaka Serikali kuchukuwa hatua kali dhidi ya Watu wanaoiba kazi za Waandishi wa Vitabu ili kulinusuru soko lao linaloweza kuwapatia tija kutokana na Uandishi huo.
Kongamano hilo la Kimataifa la Siku mbili la Kiswahili la Bakiza liloshirikisha Waswahili zaidi ya 200 kutoka pembe zote za Dunia pamoja na mambo mengine lilijadili masuala mbali mbali ikiwemo Fasih.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Kongamano hilo pia alikabidhi zawadi kwa Waandishi mbali  mbali  pamoja na Wahadhiri waliochangia kukikuza Kiswahili.
Waliopata zawadi kwa niaba ya wenzao ni Profesa Baby Masamba, Dr. Shani Omar, Profesa Shahal Ahmed, Pacific Malonga, Ala Sala Abdulwakil, Walad Bin Walad, Makoto Promoto, Maseleka, Legele pamoja na Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili Zanzibar BAKIZA Bibi Mwanahija Ali Juma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.