Habari za Punde

Kiongozi Chama Cha Tadea Akabidhi Msaada wa Kifusi Kwa Ajili ya Ujenzi wa Barabara ya Shehia ya Shakani.

Na Takdir Ali,  Maelezo -Zanzibar.
Waziri asiekuwa na Wizara Maalum (MBM)Mh.Juma Ali Khatibu amesema atahakikisha anaendeleza kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo kwa kuwaletea Maendeleo Wananchi katika maeneo yao.
Ameyasema hayo huko Shakani alipokuwa akikabidhi kifusi cha ujenzi wa njia  yenye urefu wa mita 300,chenye thamani ya zaidi ya milioni 6 na kusema ameamua kukabidhi kifusi hicho ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Amesema Wananchi wanahitaji huduma mbali mbali kama vile ya maji,umeme na barabara hivyo ni vyema kwa viongozi hao kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuwatatulia matatizo wananchi.
Hata hivyo amewataka wengine kuunga Mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein za kuwatumikia Wananchi na kuomba kupewa mashirikiano ya hali na mali ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri.
Mh,Khatib ambae pia ni Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Ada Tadea amewataka Viongozi waliochaguliwa kutatua matatizo yanayowakabili Wananchi ikiwa ni pamoja na Maji,Umeme na Barabara bila kujadili Itikadi za vyama vyao.
Nao baadhi ya Wakaazi wa Shehia ya Shakani Wilaya ya Magharibi “B” wamempongeza Waziri huyo kwa msaada huo ambao utawasaidia kuondosha usumbufu wanaoupata hasa wakati wa mvua na kuwaomba Viongozi wengine kuiga mfano kama huo.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.