Habari za Punde

Kutoka Baraza la Wawakilishi leo Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Baraza la 9 la Wawakilishi uliokuwa ukifanyika  huko katika Majengo ya Baraza hilo Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Mh. Simai Mohamed Said, Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake Pemba Mh. Suleiman Sarahan Said na Mwakilishi wa Kuteuliwa Mh. Ahmada Abdul wakil wakiwa makini kusikiliza Hotuba ya Balozi Seif.
Mwakilishi wa Jimbo la Mtoni Mh. Hussein Ibrahim Kulia na Mwakilishi wa Jimbo la Malindi Mh. Mohamed Ahmada Salum Kushoto wakimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Kati kati nje ya Ukumbi baada ya kumaliza Hotuba yake.
Picha na – OMPR – ZNZ.  
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba udanganyifu wa Mitihani ya Taifa ya Darasa la 10 { Form 11} uliotokea na kulazimisha Serikali kufuta Mitihani yote haukubaliki hata kidogo kwa vile una nia ya kutaka kuliangamiza Taifa Kimaendeleo.
Alisema hakuna Serikali hata moja Duniani inayokubali kuchezewa Elimu yake na uamuzi aliochukuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wa kufuta mara moja Mtihani wote wa Darasa la 10 baada ya kugundua kuvuja kwa Mitihani ni uthibitisho  kwamba Serikali kamwe haitokubali kutokea upuuzi huo
Akitoa Hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Baraza la 9 la Wawakilishi  huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukuwa hatua kali na za Kisheria dhidi ya wale wote waliohusika na uhalifu huo wa kuvuja kwa Mitihani.
Balozi Seif aliviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wahusika wote walioshiriki  kwenye  uhalifu huo na wanatakaobainika  na hujuma hizowapelekwe Mahakamani mara moja kujibu dhambi zinazowakabili.
“ Tutang’oa Miti hata kama ni mikubwa kama Mbuyu, Miche, Mizizi na mbegu zinazosubiri kuchipua ili tukio hili lililoitia  aibu Serikali yetu lisitokezee tena”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi wote  wa Zanzibar washirikiane na Serikali katika kupiga vita uhalifu kama huo ambao ukiachiliwa utaliangamiza Taifa huku akiiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuchukuwa tahadhari zote ili udanganyifu wa Mitihani Nchini usitokee tena.
Akizungumzia masuala yanayowasumbua Wananchi wenye Ulemavu Nchini ambayo huwapa usumbufu mkubwa katika harakati zao za Kimaisha za  kila siku na hatimae kuwadhalilisha  ni miundombinu isiyo rafiki kwao hasa Majengo ya Taasisi za Umma wakati wanapofuatilia kutaka kupatiwa huduma za Msingi.
Balozi Seif alisema Majengo mengi ya Taasisi za Umma yamejengwa bila ya kuzingatia mahitaji halisi ya Watu wenye Ulemavu  ambayo yanawapa matatizo makubwa kutokana na Miundombinu iliyopo.
Aliendelea kutoa wito kwa vyombo vyote Nchini vinavyosimamia ujenzi wa Miundombinu yote pamoja na Majengo kuzingatia Muongozo wa Serikali wa Miundombinu rafiki ambao unaeleleza upatikanaji wa Haki na Fursa kwa Watu Wenye Ulemavu kuweza kufikia huduma zitolewazo bila ya vikwazo vyovyote.
Balozi  Seif alitanabahisha Wananchi kuelewa kwamba  wote ni Walemavu watarajiwa. Hivyo wanahitaji kujitengenezea  mazingira ya Miundombinu isiyokwaza wala kumpa tabu Mtu ye yote katika Maisha yake ya kawaida.
Kuhusu mapambano dhidi ya maradhi thakili ya Ukimwi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar kama zilivyo Nchi nyengine Duniani imejiwekea malengo ya kuzifikia shabaha za Tisini Tatu {90-90-90} ifikapo Mwaka 2020 ili kumaliza janga hilo ifikapo Mwaka 2030.
Alisema katika kuzifikia shabaha hizo Zanzibar  tayari imeshazifikia Tisini Mbili za mwanzo ambazo ni asilimia 90% ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wanakuwa wanajitambua.
Balozi Seif alifafanua kwamba inapendeza kuona kwamba hadi kufikia Septemba Mwaka huu wa 2018 asilimia 92%  ya Watu wanaokisiwa kuishi na Virusi vya ukimwi wanajitambua ikiwa ni sawa na Watu 5,861 kati ya Watu  6,393.
Alieleza kwamba Tisini ya Pili ni ya wale waliojielewa kwamba wameathirika na Virusi vya Ukimwi na kuanza kutumia Dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi ambapo imeshafikia asilimia 98%  sawa na Watu 5,725 kati ya Watu 5,861.
Alifahamisha kwamba bado haijafikia shabaha ya asilimia 90% ya Tatu inayotaka asilimia 90% ya wale wanaotumia dawa za kupunguza makali ya Virusi kwa kiwango cha chini cha virusi mwilini ambapo hadi Mwezi Septemba Mwaka  huu tayari imefikiwa asilimia 76%.
Balozi Seif alitanabahisha wazi kwamba kwa vile ukimwi bado upo na unaathiri nguvu kazi ya Taifa kwa vile hauna dawa aliendelea kutoa wito kwa Wananchi wote kuchukuwa juhudi za makusudi kutumia ipasavyo huduma za upimaji Afya ili kuutendea haki ujumbe wa Mwaka huu wa 2018 unaoelezea ” Pima Virusi vya Ukimwi ujuwe Afya yako”
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dr. Ali Mohamed Shein kwa kutekeleza matakwa ya Wazanzibari ya kutia saini Mkataba wa Mgawanyo wa uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
 Balozi Seif alisema Mkataba huo uliotiwa saini  baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Rakgas ya Nchini Ras Al – Khaimah mnamo Tarehe 23 Mwezi Oktoba Mwaka huu wa 2018 ni halali kama ilivyokuwa halali boribo siagi kuliwa.
Alieleza kwamba wale wanaodhani kwamba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein amevunja Katiba au Sheria ya Nchi anahaki ya kwenda Mahakamani kwa vile Zanzibar  inafuata misingi ya Utawala Bora katika uendeshaji wake.
Mkutano wa 12 wa Baraza la 9 la Wawakilishi umejadili kwa kina Miswada Mitatu ambayo ni ule wa Sheria ya kuweka Masharti yanaosimamia utoaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Kurahisisha upatikanaji wa Haki na Kuweka Masharti mengine hanayohusiana na hayo.
Wa Pili ni Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Ukuzaji na Kulinda Uchumi Zanzibar Nambari 11 ya Mwaka 2004 na kutunga Sheria ya Mamlaka ya Ukuzaji na Kulinda Vitega Uchumi Zanzibar na Kuweka Masharti mengine yanayohusiana na hayo.
Mswada wa Tatu ni ule wa Sheria ya kufuta Sheria ya Vyama vya Ushirika Nambari 4 ya Mwaka 1986 na Kutunga Sheria ya Vyama vya Ushirikia Zanzibar ya Mwaka 2018 ambayo inaweka utaratibu wa Uundaji  na Uendeshaji wa Vyama vya Ushirika na Mambo Mengine yanayohusiana na hayo.
Baraza hilo ambalo ni Taasisi iliyopewa Mamlaka ya Kutunga Sheria Zanzibar Wajumbe wake walipata fursa ya kuuliza Maswali ya Msingi 123 na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara tofauti limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 06 Febuari Mwaka 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.