Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Viwanja Vya Ndege Vya Oman.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Ujumbe wa Viongozi Sita wa Viwanja vya Ndege vya Oman ukiongozwa na Afisa Mtendaji wake Sheikh Aimen Ahmed Al – Hosni Vuga Mjini Zanzibar.
 Balozi Seif Kulia akimkabidhi Afisa Mtendaji wa Viwanja vya Ndege vya Oman Sheikh Aimen Ahmed Al – Hosni bidhaa za viungo zinazozalishwa Zanzibar.
Afisa Mtendaji wa Viwanja vya Ndege vya Oman Sheikh Aimen Ahmed Al – Hosni kati kati akimkabidhi Balozi Seif zawadi kama ishara ya kumbukumbu ya ziara yao Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif wa Pili kutoka Kushoto akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Viongozi Sita wa Viwanja vya Ndege vya Oman baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Seif akiagana na Afisa Mtendaji wa Viwanja vya Ndege vya Oman Sheikh Aimen Ahmed Al – Hosni pamoja na Ujumbe wake mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.Kati kati yao ni Makamu wa Rais wa Viwanja vya Ndege vya Oman Bwana Ali Zaid.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Viwanja vya Ndege vya Oman Sheikh Aimen Ahmed Al - Hosni alisema Serikali ya Oman imeamua kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za uimarishaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ili ufikie vigezo sahihi vinavyohitajika Kimataifa kama ulivyo ule wa Muscat Oman.
Alisema hatua hiyo ina madhumuni ya kuona harakati za Kibiashara na Mawasiliano ya Anga yaliyokuwa yakifanyika Zanzibar zinarejea kama kituo cha kiunganishi baina ya Nchi za Mwambao wa Afrika Mashariki na Mataifa mbali mbali Ulimwenguni.
Sheikh Aimen Ahmed Al –Hosni alieleza hayo akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Sita wa Taasisi hiyo ya Usafiri wa Anga ya Oman wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali ya Oman tayari imeshajitolea kuisaidia Zanzibar katika hatua za ujenzi wa Uwanja huo kwa kadri ya mahitaji halisi yaliyopo ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano na uhusiano wa Kidamu unaowaunganisha Wananchi wa Mataifa hayo Mawili.
Afisa huyo Mtendaji  Mkuu wa Viwanja vya Ndege vya Oman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Viwanja hivyo uko tayari kutoa mualiko kwa Watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Zanzibar kwenda kujifunza hatua iliyofikiwa kwenye uwanja huo wa Kimataifa.
Sheikh Aimen Ahmed alimthibitishia Balozi Seif kwamba ukweli ulio wazi ni kwa Wananchi wa Oman na Zanzibar kuona fahari wanapoendelea kushirikiana zaidi katika masuala ya Maendeleo ya Kiuchumi  badala ya yale yaliyozoelekea ya Mila na Utamaduni unaofanana.
Naye Makamu wa Rais wa Viwanja vya Ndege vya Oman Bwana Ali Zaid alisema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat Nchini Oman hivi sasa umefikia nafasi ya 20 ya ubora wa huduma za Usafiri wa Anga Duniani kasi iliyotokana na Serikali ya Nchi hiyo kufanya juhudi ya ziada ya kuimarisha Miundombinu yake.
Bwana Zaid alisema Uwanja huo ambao kwa sasa unaongoza katika Ukanda wa Mataifa ya Mashariki ya Kati kwa kutoka huduma bora za viunganishi wa usafiri wa Anga pamoja na mambo mengine kwa Abiria ambapo pia tayari umeshatoa ajira zaidi ya Wafanyakazi 1,224.
Alisema wakati huduma za usafiri katika viwanja vilivyopo imeimarika zaidi malengo yametayarishwa kwa ujenzi wa Viwanja vipya Viwili  katika Miji ya Muscat na Salala ili kuifanya Nchi hiyo ya Mashariki ya kati kuwa kiunganishi cha Usafiri kwa Bara la Asia na Bahari ya Pacific.
Makamu wa Rais huyo wa Viwanja vya Ndege vya Oman alisisitiza kwamba Oman kwa sasa imekuwa Mwanachama mzoefu katika utoaji wa huduma za usafiri wa Anga na kupata Tunzo kwenye Shirika la usafiri wa Anga la Kimataifa.
Akigusia masuala mengine ya Uchumi na Maendeleo Mmoja miongoni mwaWajumbe wa Msafara huo Bwana Mohamed Al – Mandhari alisema upo uwezekano wa Taasisi za Kiuchumi za Oman kuangalia uwezekano wa kuwekeza Miradi ya pamoja katika Sekta ya Umeme na Kilimo.
Bwana Mohamed alisema Taasisi hizo zina uwezo wa kuzalisha Umeme Megawati 30 kwa wakati mmoja zinazoweza kusaidia huduma za wazalishaji wadogo wadogo sambamba na Kilimo cha kisasa kinachoweza kutoa ajira hasa kwa Wajasiri Amali.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar bado inaendelea kutumia njia moja ya Umeme katika matumizi ya Taasisi za Umma pamoja na Wananchi jambo ambalo ni changamoto inapotokea hitilafu.
Alisema uwezo wa Mradi huo wa Umeme unaotegemea nguvu za jua unaweza kuwa mkombozi hatua itakayoweza kuongeza kasi ya ushirikiano uliopo baina ya Zanzibar na Oman zenye mafungamano kwa karne nyingi zilizopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi huo wa Viwanja vya Ndege vya Oman kwenye sekta ya Umeme una fursa ya kuandaa utaratibu wa kuandika Maombi yatakayowasilishwa Serikalini kwa hatua zinazofaa.
Alisema Zanzibar kwa muda mrefu tayari imeshajipanga katika uimarishaji wa Uchumi wake kwa kujenga miundombinu kwenye sekta tofauti ili kujiweka tayari kuingia katika mfumo wa uchumi wa Kati wa Viwanda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.