Habari za Punde

PBZ yakanusha taarifa zilizosambazwa mitandao ya kijamii kuhusiana na kutolewa namba mpya


MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Juma Ameir Hafidh akikanusha taarifa zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kutolewa kwa namba mpya za wateja wa benki hiyo. taarifa hiyo aliitoa katika Ofisi za PBZ ziliopo Mpirani Mjini Unguja.

Kulikuwa na Taarifa zilizokuwa zikienea kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuanzia jana Jumatatui 03/12/18 PBZ iliingia katika mfumo mpya wa kisasa  wa kutunza taarifa za kibenki na hivyo namba za zamani za akaunti hazitumiki tena.

Hata hivyo taarifa hizo si za kweli kama ilivyothibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji PBZ.


NA MWASHAMBA JUMA

BENKI ya Watu wa Zanzibar PBZ imekanusha taarifa zilizoenea kwenye mitandao jamii kuhusiana na marekebisho yaliyofanywa hivi karibu na benki hiyo.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari hapo ofisini kwao Mpirani, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Juma Ameir Hafidh aliwataka wananchi na wateja wa benki hiyo kuupuuza uvumi huo na kusema kuwa hauna ukweli wowote.

Alisema PBZ ni benki ya Serikali hivyo taarifa zake haziwezi kutolewa mitaani bila kufuata utaratibu rasmi wa utoaji taarifa sahihi.

“Hii ni benki ya serikali taarifa zetu haziwezi kuwa za mitaani, hivyo tunawaomba wananchi wazipuuzie taarifa zisizo rasmi ambazo zimezagaa kwenye mitandao” alitahazarisha Mkurugenzi huyo.

Aidha, alieleza hivi karibuni Benki hiyo ilifanya mabadiliko ya mtandao mpya wa kutolea huduma za kibenki kwa lengo la kuboresha huduma bora kwa wateja wake.

Alisema mabadiliko yaliyofanywa na benki hiyo hayatoathiri miamala yoyote ile ikiwemo kutoa na kuweka fedha kwa kutumia akauti za zamani za wateja wake.

 “Wateja wote wa benki yetu wataendelea kupata huduma kama kawaida kwa kutumia akauti zao za zamani, aidha, huduma za hundi na kadi za ATM zitaendelea kutumika zile zile” alifahamisha Mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo, aliwatoa wasiwasi wateja wa benki hiyo na kueleza kuwa PBZ itaendelea kuwa benki ya watu wa Zanzibar kwa kutoa huduma bora kwa wateja na wasiokuwa wateja wake.

Kufuatia PBZ kuingia katika mfumo mpya wa kisasa, tokea ulipoanza rasmi Disemba tatu mwaka huu, alisema sasa benki hiyo inatoa huduma ya ‘PBZ Instant Pay’ ambayo inamuwezesha mteja wa benki hiyo kutumia fedha ndani ya Tanzania ya malipo ya papo kwa papo.

Aliongeza kuwa huduma hiyo pia itamuwezesha mtumiaji wa PBZ kutuma pesa hata kwa mtu asiekua mtejawa PBZ sambamba na kuchukua fedha katika tawi lolote la benki hiyo.

Akizungumzia mfumo wa ATM alisema wateja sasa wanaweza kutoa fedha kwa masaa 24 bila ya kuwepo kwa usumbufu wowote pamoja na kutuma, kuhaulisha pesa kutoka akaunti zao na kwenda katika akaunti ya mteja mwengine wa PBZ.

Huku mtumiaji wa simu za mkononi mwenye tigopesa, M pesa ama Aitel Money pia atakuwa na uwezo wa kutoka fedha katika ATM za PBZ.

Akizungumzia huduma za “Internet Banking” pia alieleza kuwa ni moja ya maboresho mapya yaliyofanywa na benki hiyo, ambapo alieleza kuwa wateja wao watakuwa na uwezo wa kutuma fedha katika akaunti za ndani za PBZ na benki nyengine zilizopo Tanzania, pamoja na kumuwezesha mteja wa benki hiyo kufanya malipo kwa wazabuni wenye akaunti katika benki hiyo na benki nyengine za ndani  na  nje ya nchi.
Aidha, huduma nyengine ni kumuwezesha mwajiri kulipia mishahara ya wafanyakazi wake ambao wana akaunti katika benki yoyote iliyopo Tanzania pamoja na wateja kupata huduba za PBZ pasipo kufika matawini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.