Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Mfuko wa Umoja wa Mataifa Unaoshughulikia Maendeleo ya Watoto (UNICEF) Nchini Tanzania Bi.Maniza Zaman, alipofika Ikulu Zanzibar,kumtambulisha Mkuu wa UNICEF Ofisi ya Zanzibar Bi. Maha Damaj, na kufanya mazungumzo leo.4/12/2018.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza mikakati inayochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na maradhi mbali mbali yakiwemo ya miripuko ambapo yanapozuka huathiri watu wa rika zote wakiwemo watoto.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Maendeleo ya Watoto (UNICEF) nchini Tanzania Maniza Zaman
aliyefuatana na Mkuu mpya wa Shirika hilo hapa Zanzibar Maha Damaj ambaye
alifika kujitambulisha kwa Rais.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa miongoni mwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa ni pamoja na kujenga mitaro mikubwa katika eneo
la mji wa Zanzibar ambayo matokeo yake itaisadia kuondosha matuamo ya maji
ambayo hatimae huleta maradhi ya miripuko na kulata athari kubwa kwa jamii.
Aliongeza kuwa katika
kipindi kifupi ambacho bado mradi huo ujenzi wake unaendelea tayari mradi
umeanza kuleta matumaini makubwa ambapo athari mbali mbali ambazo hapo siku za
nyuma zilikuwa zikitokea zimepungua ikiwemo kutuama kwa maji pamoja na kuleta
mafuriko.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa mbali ya jitihada hizo suala zima la elimu pamoja na kuendeleza
Sera na mikakati ya Serikali katika kupambana na maradhi mbali mbali pamoja na
kuimarisha ustawi wa akina mama na watoto zimekua zikichukuliwa.
Hata hivyo, Rais Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la UNICEF kwa jitihada zake za kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha watoto wa Zanzibar wanapata haki zao
za msingi ikiwa ni pamoja na elimu, afya pamoja na huduma nyengine za kijamii.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa Programu ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP),
inayohusisha Mashirika tisa ya UN iliyozinduliwa hivi karibuni kutasaida katika
kuleta mafanikio yaliokusudiwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Nae Mwakilishi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto Duniani (UNICEF) nchini
Tanzania Bi Maniza Zamani alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika suala zima la kuwahudumia watoto pamoja na akina
mama.
Bi Zamani alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika
kuwahudumia watoto sambamba na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo
kupata elimu na afya bora huku akizipongeza juhudi za Serikali.
Alieleza kuwa Shirika
hilo linathamini juhudi hizo na limeweza kushuhudia mafanikio na mabadiliko
makubwa katika sekta za maendeleo hatua ambazo zimewawezesha watoto wa Zanzibar
kuweza kupata haki zao za msingi pamoja
na mahitaji yao muhimu ya kimaisha.
Mwakilishi huyo alieleza azma
ya programu ya pamoja ya UN hapa Zanzibar kuwa mbali na mambo mengine pia,
itasaidia kupunguza vifo vya uzazi, ukatili dhidi ya wanawake
na watoto.
Aliongeza kuwa Shirika
la (UNICEF) limekwua likichukua juhudi zake katika kuhakikisha wananchi wa
ngazi ya chini katika jamii wanashirikishwa kwa kuweka Kamati ndogondogo katika
jamii katika kuhakikisha inakwenda sambamba na mikakati iliyowekwa na Shirika
hilo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment