Habari za Punde

Balozi Seif afungua skuli ya Sekondari ya JKU ikiwa ni katika shamrashamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Rasmi Jengo la Ghorofa Tatu la Skuli ya Sekondari ya JKU Mtoni ikwa ni shamra shamra za kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
 Balozi Seif akiangalia Meza za moja ya Darasa la Kompyuta la Skuli ya Sekondari ya JKU alipolizindua Rasmi katika shamra shamra za kusherehekea Maadhimisho ya Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
  Balozi Seif akikagua baadhi ya madarasa ya Jengo la Skuli ya Sekondari ya Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} Mtoni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Balozi Seif akiangalia baadhi ya Vifaa vya Maabara vilivyomo ndani ya moja ya Darasa la Maabara ya masomo ya Sayansi ndani ya Jengo la Ghorofa Tatu  la Skuli ya Sekondari ya JKU
  Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya JKU wa Masomo ya Sayansi pamoja na Ufundi wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye uzinduzi wa Jengo lao la Ghorofa Tatu.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akicheza ngoma ya Kikundi cha Utamaduni cha JKU kilichokuwa kikitoa burudani ya ngoma Maarufu ya Kibati kwenye hafla ya Uzinduzi wa Jengo la Skuli ya Sekondari ya JKU.

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar hainabudi kudumisha makubaliano na kuendelea kuitambua Skului ya Sekondari ya Jeshi la Kujenga Taifa {JKU} kama sehemu ya kuwafundisha Vijana wa Michepuo ya masomo ya Sayansi.
Alisema jambo la muhimu katika kulizingatia ni kuukumbusha Uongozi huo kutosahau kuwapatia huduma zote Wanafunzi hao kama wanavyopatiwa Wanafunzi wa skuli nyengine  zilizo chini ya Wizara hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akilizindua Jengo la Ghorofa la Skuli ya Sekondari ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar {JKU} hapo Mtoni ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kutimia Miaka 55.
Alisema amefarajika kufahamu kwamba Skuli ya Sekondari ya JKU imekubaliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Aamali Zanzibar kuendelea kuwasomesha Wanafunzi wa Michepuo ya Sayansi kila Mwaka bila ya malipo yoyote kama ilivyo katika Skuli nyengine za Serikali.
Balozi Seif alisema jambo hilo linatoa fursa kwa Watoto wa Kimaskini kunufaika na uwekezaji huo wa Serikali katika Jeshi la Kujenga Uchumi pamoja na kuipa fursa JKU kulea Watoto wa Zanzibar kama ilivyo dhamira ya kuwepo kwa kwa Jeshi hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi Mzima wa Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} kwa kuona umuhimu wa Jeshi hilo kushiriki kikamilifu katika utoaji wa Taaluma kwa Vijana wa Taifa hili.
Alisema ujenzi wa Jengo hilo la Ghorofa Tatu uliosimamiwa na Wahandisi wa Jeshi lenyewe kuanzia hatua ya Msingi mnamo Mwaka 2013 hadi hatua za mwisho ni kielelezo cha Uwezo na dhamira ya dhati ya Wana JKU  katika kuenzi mawazo, fikra na busara za Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume za kuwapatia Elimu Bure Wananchi wote na kuchangia maendeleo ya Zanzibar.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Jeshi la Kujenga Uchumi lililoundwa Mwaka 1977 ni zao la Kambi za Umoja wa Vijana zilizoanzishwa mara tuu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964  ambayo kwa wanyonge ndio chimbuko la Maendeleo yaliyopop Nchini.
“ Ukiona vyaelea vimeundwa”. Tukiona Skuli ya Sekondari ya JKU imepata maendeleo makubwa kwa kipindi kifupi ni kutokana na Uongozi bora na imara wa Mwalimu Mkuu na Wasaidizi wake”. Alisisitiza Balozi Seif.
“ Nikiwa pia Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nikipewa usimamizi wa masuala ya Watu wenye mahitaji Maalum {Walemavu} nimefarajika kuona Skuli hii imezingatia maeneo maalum yatakayotumiwa na Wanafunzi wenye mahitaji Maalum”. Hongereni sana kwa kazi hiyo nzuri.
 Aliushauri Uongozi wa JKU kufikiria kujenga Dakhalia ili kutoa nafasi kwa Wanafunzi wanaotoka sehemu za mbali hasa Vijijini kuondoashaka ya Makaazi katika Skuli hiyo inayofanya vyema katika Mitihani yake ya Kitaifa na Kikanda.
Balozi Seif ameridhika na malengo ya Jeshi hilo la kuanzisha Skuli yake ambayo kwa sasa imekuwa miongoni mwa Skuli zinazogombaniwa na Wananchi katika kuwapeleka Watoto wao kwa kupata malezi bora
Alisema inatia moyo kuona Skuli ya Sekondari ya JKU katika Mitihani ya Darasa la 12 { Form 1V} imefanikiwa kuondosha Daraja la 0 kwa takriban Miaka Mitatu sasa wakati Mitihani ya Darasa la Kumi imeingia katika Skuli Kumi Bora kwa Zanzibar na Skuli Kwanza kwa Wilaya ya Magharibi “A”.
Balozi Seif alifahamisha kwamba katika Mitihani ya Kanda ya Magharibi “A” Mwezi wa Agosti 2018 ambayo inajumuisha Skuli 11 za Sekondari kwa Mwaka wa Pili mfululizo imekuwa ikichukuwa nafasi ya Kwanza  kwa masomo yote na kwa ujumla.
Alisema kwa upande wa Skuli za Majeshi Tanzania katika Mitihani yao ya pamoja  ya mwisho wa Mwezi wa Oktoba mwaka 2018 Wanafunzi wa Skuli ya JKU wameingia katika nafasi Tatu bora  kwa masomo Manane ya Kidato cha Nne.
“ Bila shaka Skuli yenu ya Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} inasaidia kujenga taswira nzuri ya Jeshi letu la JKU Machoni mwa Wananchi wetu”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wahandisi wa Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} kutobweteka na hatua waliyofikia na badala yake waongeze jitihada kulingana na mabadiliko ya mfumo wa Dunia katika masuala ya Ujenzi yanayokwenda kwa kasi ya Teknolojia ya Kisasa.
Alisema wahandisi hao wanapaswa kuzingatia mabadiliko ya ujenzi yaliyokumbwa na changamoto ya upungufu  wa rasilmali ya mchanga inayovikabili Visiwa vya Zanzibar ambapo kwa sasa wanalazimika kubadilisha njia za ujenzi ili ziende sambamba na rasilmali zinazopatikana hivi sasa nchini.
Akitoa Taarifa za Kiufundi za Ujenzi wa Jengo hilo la Skuli ya Sekondari ya JKU Mtoni Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum wa SMZ Bibi Radhia Haroub Rashid  alisema Jengo hilo limeanza ujenzi wake mnamo Mwaka 2013 kwa michango ya ada za Wanafunzi wenyewe.
Bibi Radhia alisema Awamu ya Pili ya Ujenzi huo imefanywa baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuidhinisha Shilingi Bilioni 1.2 kwa gorofa ya Pili naa baadae kuidhinisha Shilingi Bilioni 1.12 kukamilisha Awamu ya Tatu iliyoambatana na Vifaa vya ndani.
Alisema kukamilika kwa Ujenzi huo kulikoungwa Mkono na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na jitihada za wapiganaji na Makamanda wake kutakamilisha Malengo ya Jeshi hilo ya kuwapatia Taaluma Askari wake pamoja na Watoto wa Taifa hili.
Aliahidi kwamba Uongozi wa Wizara utaendelea kuratibu katika kuona jengo hilo linatumiwa  vyema katika malengo yaliyokusudiwa ili liendelee kutoa huduma za Kitaaluma kwa miaka mingi ijayo.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir alisema Wizara hiyo itaendelea kuimarisha Miradi iliyoanzishwa na Wapiganaji na Makamanda wa Kikosi hicho.
Waziri Kheir alisema Serikali kupitia Wizara anayoisimamia ina kila sababu ya kuunga mkono jitihada hizo ambazo zimewezesha kuifanya skuli hiyo ni ya mwanzo kuwa na Lifti Zanzibar sambamba na uwekwaji wa miundombinu kwa Wanafunzi wenye mahitaji Maalum.
Jengo la Skuli ya Sekondari ya Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} hadi kukamilika kwake ina uwezo wa kuchukuwa Wanafunzi 1,640 ikiwa na Madarasa 31, Vyumba Vitatu vya Maabara ya Sayansi, Maktaba, Vyumba viwili wa Kompyuta, Ofisi ya Walimu pamoja na huduma nyengine zinazohitajika katika Majengo ya Skuli.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.