Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Kamati ya Mashindano ya Mapinduzi Cup ya ZBC

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Kamati ya Mashindano ya Mapinduzi Cup ya ZBC iliyofika Ofisini kwake kupokea zwadi ya Vifaa na vikombe kwa washindani wa mashindano hayo zilizotolewa na Kampuni ya ZAT.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Kamati ya Mashindano ya Mapinduzi Cup ya ZBC iliyofika Ofisini kwake kupokea zwadi ya Vifaa na vikombe kwa washindani wa mashindano hayo zilizotolewa na Kampuni ya ZAT.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ubebaji Mizigo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Mohamedraza Hassanaali akisisitiza azma ya kampuni yake kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha Sekta ya Michezo.
  Balozi Seif kati kati akimkabidhi zawadi na baadhi ya vifaa vya Michezo Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} Bibi Nasra Mohamed kwa washindani wa mashindano ya Mapinduzi Cup ya Watoto.
Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} Bibi Nasra Mohamed akitoa shukrani kw wadau wa michezo waliojitolea kusaidia nguvu katika uimarishaji wa mashindano ya Mapinduzi Cup.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali iko tayari kuunga mkono wazo la kutaka kuanzishwa kwa Mashindano ya Mapinduzi Cup  kwa kuzishirikisha Timu za Kombaini za Soka za Vijana wa Nchi Tano za Afrika ya Mashariki wenye Umri usiozidi Miaka 17.
Alisema wazo hilo mbali ya kuongeza hamasa ya sherehe za Maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwakja 1964 bali pia yataamsha ari na kuibua vipaji vya Vijana wanaoweza kuiletea sifa Afrika ya Mashariki katika ulimwengu wa Soka.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi zawadi na Vifaa vya Michezo pamoja na Vikombe vilivyotolewa na Uongozi wa Kampuni ya ubebaji Mizigo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar {ZAT} kwa ajili ya washindi wa Mashindano ya Mapinduzi Cup kwa Watoto yanayosimamiwa na Shirika la Utangazi Zanzibar {ZBC}.
Alisema endapo wazo hilo litafikia maamuzi sahihi, alishauri wasimamizi wake kuzingatia taratibu zitakazowekwa hasa suala la Umri wa Wachezaji ambalo Zanzibar imewahi kupata aibu baada ya wachezaji wake kupindukia Umri katika mashindano ya Afrika Mashariki kwa Umri usiopindukia Miaka 17.
Balozi Seif  aliueleza Uongozi wa Kampuni ya ZAT na Kamati ya Mashindano ya Mapinduzi Cup ya Watoto ya ZBC kwamba kuanzishwa kwa Mashindano ya soka ya umri usiopindukia Miaka 17 ni jambo zuri na linalopaswa kuungwa mkono wa wadau wote wa Soka Nchini.
Alisema Zanzibar ina historia ndefu katika Medani ya Michezo. Hivyo kuibuka kwa Taasisi au Wadau wanaojitolea kutaka kuunga Mkono Sekta hiyo muhimu ni faraja kwa Serikali Kuu iliyokwishaamua kuimarisha Sekta ya Michezo kwa maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Kampuni ya ubebaji Mizigo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar {ZAT} chini ya Mkurugenzi wake Mtendaji Mohamedraza Hassanaali kwa jitihada zake za kuunga mkono Sekta ya Michezo Nchini.
Alisema Jamii Nchini imekuwa ikishuhudia jitihada zinazofanywa na mdau huyo wa Michezo ndani ya kipindi cha takribani Miaka 30 sasa anayepaswa kuheshimiwa na kila Mwanamichezo Nchini.
Akitoa Shukrani kwa Niaba ya Uongozi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} na Kamati yake ya Mashindano Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo Nasra Mohamed alisema mashindano ya Mapinduzi Cup kwa Watoto yamepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwake Miaka Mitatu iliyopita.
Nasra alisema licha ya changamoto zilizojitokeza katika kusimamia Mashindano hayo lakini ipo faraja kubwa kwa wasimamizi wake kutokana na kasi kubwa ya kuungwa mkono na Wadau wa Soka wakiwemo pia wananchi wa kawaida Mitaani.
Naibu Mkurugenzi huyo wa ZBC aliushukuru Uongozi wa Kampuni ya ZAT pamoja na taasisi nyengine zinazojitolea kila wakati kuunga mkono undelezaji wa mashindano hayo ambayo kwa upande mwengine yamekuwa yakiibua Vipaji wa Vijana.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ubebaji Mizigo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar {ZAT}ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini  Mohamedraza Hassanaali alisema wakati umefika kwa Zanzibar kuandaa Mashindano ya kombe la Mapinduzi kwa Timu za Soka za Kombaini za Vijana wasiozidi Umri wa Miaka 17 wa Nchi za Afrika Mashariki.
Raza alisema Uongozi wa Kampuni yake kwa vile unaumwa na Suala la Michezo uko tayari kugharamia usafiri na malazi kwa Vijana wa Timu hizo shiriki katika azma ya kuzishajiisha zaidi Sherehe za Mapinduzi, mashindano yatakazokuwa chini ya Uratibu wa ZBC.
Alisema Timu hizo Kombaini za Soka la Vijana ingependeza zikaalikwa kutoka Uganda, Rwanda, Kenya, Tanzania Bara, na wenyeji Zanzibar wakatoa timu mbili kutoka Unguja na Pemba.
Zawadi zilizotolewa kwenye hafla hiyo na Kukabidhiwa Kamati ya Mashindano ya ZCB ni pamoja na Kikombe kwa mshindi wa kwanza na wa Pili wa Kombe la Mapinduzi Cup, muamuzi bora, Mlinda Mlango bora pamoja na Viatu kwa Mchezaji bora.
Nyengine ni medali za kila mchezaji wa Timu iliyoshika Mshindi wa kwanza na wa pili wa Mashindano pamoja na seti ya jezi kwa mshindi wa kwanza na wa pili wa mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.