Habari za Punde

Kampeni ya Jiongeze Tabora Yazinduliwa na Mhe. Aggrey Mwanri..

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe, Aggrey Mwanri, pamoja na viongozi wengine wakizindua rasmi kampeni ya jiongeze Tabora tarehe 25.01.2019
  Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe, Aggrey Mwanri, akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe, Aggrey Mwanri, viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa maendeleo kwa pamoja wakikata utepe kuashiria kukabidhiana magari ya wagonjwa pamoja na vifaa tiba kwa halmashauri za Wilaya 3 katika mkoa huo.
 Magari ya wagonjwa yaliyokabidhiwa na wadau wa maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe, Aggrey Mwanri, akijaribu moja ya magari ya wagonjwa yaliyotolewa na wadau wa maendeleo.


Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe, Aggrey Mwanri amezindua kampeni ya Jiongeze, Tuwavushe Salama! Uzinduzi huo wa Kampeni hiyo ya kitaifa mkoani humo unalenga kuwahamasiha mashirika yasiyo ya kiserikali, washirika wa maendeleo, watoa huduma za afya, familia, jamii pamoja na viongozi wa serikali na dini kwa kuchangia juhudi za taifa za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mh. Aggrey Mwanri ameshuhudia wakuu wa Wilaya 7 za Mkoa huo wakitia saini makubaliano yanayozitaka halmashauri zote katika mkoa huo kutoa kipaumbele kwa maswala ya uzazi na watoto.

Akizindua kampeni hiyo mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe, Aggrey Mwanri amesema kuwa maisha ya kila mwananchi yana thamani na hivyo “hata kifo cha mama mmoja au mtoto hakikubaliki.”

Amesema kuwa vifo vingi vya akina mama na watoto mkoani Tabora vinatokana na uzembe na kuwataka viongozi mkoani humo kujielekeza zaidi kwenye kinga kuliko tiba.  “Swala la afya ya mama na mtoto ni ya kupewa kipaumbele namba moja.” alisema

Baadhi ya maeneo yenye kupewa kipaumbele katika kampeni hiyo yanajumuisha kuboresha miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma bora zaidi za uzazi na watoto pamoja na kuhakikisha uwepo wa wahudumu wenye utaalam ili kuwezesha asilimia 50 ya vituo vya afya kuweza kufanya operesheni kwa ajili ya akina mama wajawazito na kutoa huduma ya damu salama.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya wengine Mkuu wa Wilaya ya Tabora mjini Mh. Eric Komanya Kitwala amehimiza ujenzi wa vyumba viwili katika hospitali ya Mkoa (Kitete) ili kuwasaidia akina mama wajawazito kama sehemu ya utekelezaji wa malengo  ya kampeni.

Katika uzinduzi huo pia Mkuu wa Mkoa wa Tabora amekabidhi magari 4 ya wagonjwa pamoja na vifaa tiba kwa halmashauri za Wilaya 3 katika mkoa huo. Mkuu wa mkoa wa Tabora  ameshukuru wadau hao kwa kuunga mkono juhudi za mkoa huo katika kuzuia vifo vya akina mama na watoto na kuwataka kutochoka kuchangia juhudi  hizo.

Akitoa salamu za shukrani Mkuu wa Wilaya ya Uyui Gift Msuya ameipongeza Wizara ya Afya kwa kutoa suluhisho la matatizo yaliyokuwa yakiikabili sekta ya afya kupitia kampeni hii na kutoa rai kwa watu wote kuongeza juhudi za kuhakikisha kuwa mama na mtoto wanavuka salama.  

Uzinduzi huu mkoani Tabora ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo ya kitaifa iliyozinduliwa kitaifa Tarehe 6 Novemba 2018, Mkoani Dodoma na Mhe. Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan. Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi.

Katika kampeni hii serikali ya Tanzania imeshirikiana na wadau wa maendeleo kama vile UNICEF, UNFPA, USAID, World Bank, Tanzania Communication and Development Center, FHI 360 pamoja na Ubalozi wa Canada.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.