Habari za Punde

Rais Dk Shein aifariji Familia ya Bi. Johari Yussuf Akida, muasisi wa CCM

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akimsalimia na kumpa mkono wa pole Ndugu wa Marehemu Bi. Johari Yussuf Akida,alipofika nyumbani kwao Mwanakwerekwe  na Mkewe Mama Mwanamwema Shein,kutowa mkono wa pole leo.13/1/2019.(Picha na Ikulu)  
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, atowa mkono wa pole kwa Wanafamilia ya Marehemu Bi. Johari Yussuf Akida, aliyefariki wiki iliopita, katikati Mtoto wa Marehemu Bi. Shawana Buheti,anayefuata Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, walipofika katika makaazi yao Mwanakwerekwe kutowa mkono wa pole leo 13/1/2019.(Picha na Ikulu) 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akimfariji Mtoto wa Marehemu Bi. Johari Yussuf Akida, muasisi wa CCM.katikati Bi.Shawana Buheti na kushoto Mke wa Rais wa Zanzibar. Mama Mwanamwema Shein, walipofika nyumbani kwake Mwanakwerekwe Unguja kutowa mkono wa pole leo.13/1/2019.(Picha na Ikulu) 

Zanzibar                                                                13.01.2019
---
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Mama Mwanamwema Shein wametoa mkono wa pole kwa familia ya Marehemu Bi Johari Yussuf Akida kufuatia kifo cha kiongozi huyo  kilichotokea hivi karibuni.

Alhaj Dk. Shein akiwa amefuatana na Mama Mwanamwema Shen walifika nyumbani kwa mwanawe Bi Shawana Buheti huko Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi na kutoa pole kwa familia ya Marehemu Bi Johari Yussuf Akida.

Katika maelezo yake ya pole kwa familia ya Bi Johari, Alhaj Dk. Shein ameiomba familia hiyo kuendelea kuwa na subira hasa katika kipindi hichi kigumu cha msiba na kusisitiza haja ya kuendelea kuombewa dua Marehemu.

Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa Marehemu Bi Johari atakubukwa kwa mazuri yake makubwa aliyoyafanya kwa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na jamii kwa ujumla.

Nao wanafamilia kwa upande wao walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein na Mama Shein kwa kwenda kuwapa mkono wa pole na kueleza kuwa wamefarajika kwa hatua yao hiyo kwani wameonesha kuijali familia hiyo hasa ikizingatiwa Rais Dk. Shein wakati wa maziko alikuwa Kisiwani Pemba.

Waliongeza kuwa wamefarajika kuona mara tu kurudi kisiwani humo yeye na mama Shein wamefanya safari ya kwenda kuwapa mkono wa pole.

Hata hivyo familia hiyo ilipongeza juhudi zilizochukuliwa na Rais Dk. Shein katika kumjuulia hali Bi Johari na kumsaidia katika maradhi yake kwa muda mrefu tokea hajawa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha, familia hiyo ya Bi Johari ilitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ushirikiano na msaada mkubwa uliotoa wakati akiugua hadi anafariki.

Familia hiyo pia, imetoa shukurani za pekee kwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kwa kutoa ushirikiano wake katika kipindi chote cha mazishi ya kiongozi huyo kwa kuhakikisha anazikwa kwa kufuata taratibu zote za Kichama.

Marehemu Bi Johari Yussuf Akida ambaye pia ni muasisi wa ASP, pamoja na Chama Cha Mapnduzi (CCM) alifariki dunia Januari 10 huko Kinondoni mjini Dar-es-Salaam na kuzikwa Januari 11 mwaka huu huko kijijini kwao Mwakaje

Marehemu Bi Johari alizaliwa mwaka 1938 kwenye kijiji cha Mwakaje Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi wakati huo ambapo kielimu amesoma kwenye Skuli ya Msingi ya Mfenesini nakupata elimu ya Msingi.

Bi Johari alipata elimu ya Uongozi nchini Ujerumani mwaka 1966-1967 katika Kosi ya Uongozi wa Chama kwa mwaka, Kosi ya Uongozi kwa mara nyengine huko Ujerumani mnamo mwaka 1969 pamoja na Semina mbali mbali mbali za Uongozi na mambo ya siasa.

Aidha, alikuwa mwanachama wa CCM mwenye kadi yenye namba A.681788 iliotolewa tarehe 11.4.1977 katika tawi la CCM Mwakaje Wilaya ya Magharibi Unguja.

Marehemu wakati wa uhai wake aliwahi kushika nafasi za uongozi kwenye chama ambapo aliwahi kwua Katibu wa ASP katika Tawi la Mwakaje, Katibu wa UWT ASP katika Tawi hilo, Mwenyekiti wa UWT ASP katika Wilaya ya Magharibi pamoja na Katibu Msaidizi Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa ASP Ungua.

Marehemu pia,ni Muanzilishi wa mwanzo wa UWT walioungana kutoka TANU na ASP kuwa Mjumbe wa mwanzo wa Baraza Kuu na Mjumbe wa Kamati Tekelezaji UWT Taifa mwaka 19787.

Pia,a aliwahi kuwa Balozi wa Shina ASP, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Tawi, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Jimbo la Mfenesini, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya na Mkoa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya, Mkoa na Taifa, Mwenyekiti wa CCM wa kwanza Mkoa Mjini Magharibi kuanzia 1977 hadi 1992, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mzee wa Chama na Mshauri wa CCM.

Kwa upande wa Serikali Marehemu alishika nafasi mbali mbali ikiwemo Meya wa Mjini wa Zanzibar, Mjumbe wa Mahakama Maalum ya kuhujumu Uchumi, Katibu wa Ulinzi na Usalama, Mjumbe wa W.H.O Kilimo na Mifugo, Biashara, Derava, Kiongozi wa Ulinzi na Usalama na Waziri Mgodo wa Biashara.

Marehemu amewacha watoto watatu na wajukuu tisa, Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu Bi Johari Yussuf Akida Mahali Pema Peponi, Amin.
  
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.