Habari za Punde

Balozi Seif: Maonyesho ya biashara yatafutiwe eneo la kudumu

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiingia katika eneo la mabanda ya Maonyesho kwenye Tamasha la Tano ya Biashara Zanzibar kusherehekea Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Maisara Suleiman Mjini Zanzibar.
 Balozi Seif akitembelea Mabanda mbali mbali ya Maonyesho ndani ya Tamasha la Tano ya Biashara Zanzibar hapo katika Viwanja Vya Michezo vya Maisara.

 Balozi Seif akiangalia mfumo wa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwenye Banda la Maonyesho la Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} 


Timu ya Watendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Limited {PBZ} wakimpatia maelezo Balozi Seif jinsi ya uboreshaji wa huduma kwa Wateja kitaifa na Kimataifa.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na eneo Maalum kwa ajili ya Maonyesho ya Tamasha la Biashara ili kukidhi mahitaji halisi ya Washiriki wa maonyesho hayo katika mazingira yote ya hali ya Hewa.
Alisema mpango wa kukodi mahema au ujenzi wa Mabanda kwa ajili ya shughuli hiyo unayofanyika kila Mwaka unachukuwa gharama kubwa zinazoweza kuepukwa kwa kuwa na eneo la kudumu.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko Zanzibar alipofanya ziara ya kutembelea Mabanda mbali mbali kwenye Tamasha la  Tano la Biashara kusherehekea Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema Serikali kuu tayari imeshaamua kuwepo kwa Mpango huo na kinachohitajika kwa wakati huu ni Wizara na Taasisi zinazohusika na masuala ya Maonyesho kulifanyia kazi suala hilo.
Balozi Seif alisema Watendaji wa Taasisi hizo wanapaswa kusoma kwa kufuatilia Taasisi za wenzao zilizo Tanzania Bara ambazo tayari zimeshapiga hatua kubwa ya Maendeleo katika Masuala ya Matamasha na Maonyesho mbali mbali.
“ Yapo Maonyesho ya Biashara Dar es salaam, Morogoro na Hata Dodoma ambayo tumekuwa tukiyashuhudia na wakati mwengine hupata nafasi ya kualikwa kama wageni Rasmi. Hivyo si vibaya kwenu kuiga mifano hiyo”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibahatika kuyatembelea mabanda mbali kwenye Maonyesho ya Tamasha hilo la Tano la Biashara hapo katika Viwanja vya Maisara Suleiman Mjini Unguja.
Katika matembezi hao Balozi Seif alivutia na Bidhaa tofauti zinazozalishwa na Wajasiri amali wa Zanzibar, Tanzania Bara pamoja na baadhi ya wale wa Nchi za Afrika ya Mashariki kama Unganda, Kenya, Rwanda na Burundi.
Mapema Mkurugenzi Biashara na Masoko Zanzibar Nd. Khamis Ahmada Shauri alisema jumla ya Taasisi 290 zimeshiriki Maonyesho hayo ikiwa ni onyezeko la Taasisi 71 ikilinganishwa na Taasisi 250 za Mwaka Jana.
Nd. Khamis Ahmada alimueleza Balozi Seif  kwamba katika mgawanyo huo Taasisi za Serikali mwaka huu zimefikia 55, zile zilizotoka Tanzania Bara zilikuwa 44 Rwanda 3, Kenya 3, Uganda 3, Burundi 1 na Misri 2.
Alisema Uongozi unaosimamia Tamasha hilo umelazimika kuwapanga washiriki wa Maonyesho hayo katika Maeneo finyu kutokana na ongezeko kubwa la Taasisi zilizothibitisha kushiriki maonyesho hayo.
Alieleza kwamba Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko inaendelea kufarajika na ushiriki wa Taasisi hizo uneokwenda sambamba na hamasa ya Wananchi wanaopendelea na kujitokeza kutembelea maonyesho hayo hasa wakati wa Jioni na Usiku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.