Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Uratibu) Prof. Faustine Kamuzora akizungumza wakati akifungua kikao
cha Baraza la Usimamizi wa Maafa Tanzania (TADMAC) leo Jijini Dodoma ikiwa ni kikao cha pili cha Baraza hilo.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Usimamizi wa Maafa Tanzania (TADMAC) wakifuatilia
hafla ya ufunguzi wa kikao cha Baraza hilo leo Jijini Dodoma.
Sehemu ya
watendaji na Idara ya maafa kutoka Ofisi
ya Waziri Mkuu na Wajumbe wa Baraza la Usimamizi wa Maafa Tanzania (TADMAC) wakifuatilia kikao cha Baraza hilo leo Jijini
Dodoma.
(Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Na; Mwandishi wetu;
Baraza la Usimamizi wa Maafa Tanzania
(TADMAC) limekutana leo Jijini Dodoma na kuweka mikakati ya pamoja
yakukabiliana na kuzuia majanga .
Hayo yamesemwa na Katibu Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera na Uratibu Prof. Faustine Kamuzora wakati akifungua kikao cha
Baraza hilo leo Jijini Dodoma ikiwa ni
kikao cha pili .
“ Baraza hili limepewa jukumu kubwa
na muhimu la kusimamia masuala yote yanayohusu maafa yanayotokana na majanga ya
aina zote hapa nchini”. Alisisitiza Prof. Kamuzora
Akifafanua amesema kuwa, Serikali
inaendelea kusisitiza kuimarisha hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya
majanga mbalimbali kwa kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo inazingatia
viashiria vilivyopo katika sekta mbalimbali.
Kila Taasisi katika ngazi zote
zinatakiwa kujiandaa katika maeneo yao kwa kusaidia upatikanaji wa rasilimali
za usimamizi wa maafa, Pia kutoa elimu kwa umma namna ya kuzuia majanga
yanayoweza kuathiri shughuli za uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali.
Alitaja baadhi ya matukio ya majanga
yaliyojitokeza katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2018 na kusababisha
maafa kuwa ni pamoja na mafuriko katika Wilaya 50, upepo mkali ulioambatana na
mvua kubwa katika Wilaya saba, radi
katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na ajali iliyohusisha kivuko cha Mv
Nyerere.
Kutokana na maafa hayo Serikali
ilichukua hatua mbalimbali kwa kushirikiana na wadau kuokoa maisha, kutoa
huduma kwa wananchi ikiwemo makazi ya muda, maji na chakula.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea
kuzijengea uwezo kamati za maafa katika ngazi zote kuanzia Mikoa, Wilaya na
Vijiji ili zitekeleze majukumu yao kwa weledi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Dkt Agness Kijazi amesema kuwa wamejipanga
kuhakikisha kuwa wanaendelea kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati ili
zisaidie wadau na wananchi kuchukua tahadhari.
Aliongeza kuwa wataendelea kutoa
taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa wakati na kutoa elimu kwa umma juu ya
matumizi ya taarifa hizo.
Naye Msimamizi wa Mfumo wa Kitaifa wa
Huduma za Hali ya Hewa Bi Mecklina Merchades amesema kuwa mfumo huo unasaidia
kuwawezesha wananchi kutumia taarifa hizo kufanya maamuzi sahihi na wakati.
Kikao cha pili cha Baraza la Usimamizi
wa Maafa Tanzania kimefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 7
ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine inaunda Baraza hilo.
No comments:
Post a Comment