Habari za Punde

Uwekaji wa Jiwe la Msingi Kituo Cha Mbogamboga Mpendae Unguja.

Na Mwashungi Tahir.   2-1-2019.
WAZIRI asiye kuwa na Wizara maalum Juma Ali Khatib amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejikita katika kuimarisha Sekta ya kilimo kwa lengo la kutoa fursa za Ajira kwa Vijana.
Waziri Juma ameyasema hayo katika uwanja wa Mpendae wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi kituo cha mboga mboga, matunda na viungo ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema ili soko la ajira liweze kukua Vijana wawe na mashirikiano na Jumuiya ya Asasi inayoendeleza na kushughulikia mambo ya biashara (Tanzania Houriculture Association TAHA) kwa lengo la kujifunza kilimo cha kisasa na kukuza kipato chao.
Pia alisema iwapo kilimo hicho kitaimarishwa vyema kitawezesha Matunda kupatikana kwa wingi na kukidhi soko la ndani na Nje ya Nchi.
Pia aliwataka vijana wanaosoma Chuo cha Kilimo Kizimbani kuwa karibu na wataalamu ili kukuza sekta kilimo na kuongeza ajira.
“Wanafunzi mliopo Kizimbani itumieni vizuri elimu hii ili kuweza kupata wataalamu wa kuleta mabadiliko ya kilimo katika ngazi ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla ili kujiongezea kipato,” alisema Waziri Juma
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Dk Makame Ali Ussi alisema Mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1964 ndio mkombozi na Dira ya maendeleo hivyo Wananchi wanapaswa kuyaenzi kupitia kizazi kimoja na kingine.
Amesema kupitia Jumuiya ya TAHA wananchi watapata uwezo mzuri wa kusarifu Matunda na Mbogamboga ili kuweza kuyatumia vyema na kujiingizia kipato.
Alisema lengo la TAHA  ni kupunguza uingizwaji wa mazao kutoka nje na kuweza kuzalisha mazao hayo nchini ikiwemo Matikiti, Tungule na pilipli.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas aliwataka wananchi kuyaendeleza na kuyatukuza Mapinduzi yetu ambayo yameleta Maendeleo, amani na utulivu na nchi yetu.
Jumuiya ya TAHA yenye Makao makuu yake Arusha ilisajiliwa mwaka 2004 huko Tanzania Bara, na kusajiliwa rasmi Zanzibar mwaka 2002 ambapo inajishughulisha zaidi na kilimo cha kisasa cha mbogamboga, Matunda na Viungo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.