Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akikata Utepe kuashiria Uzinduzi wa Skuli ya Msingi Chimba Wilaya ya Micheweni Shehia ya Chimba, ikiwa ni shamra shamra za Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizoaza leo Kisiwani Pemba.kushoto Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Pembe.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kuiunga mkono Serikali yao
ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imeamua kwa makusudi kutoa elimu bure kuanzia
Chekechea, Msingi hadi Sekondari.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko Chimba, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba katika
uzinduzi wa Skuli ya Msingi ya Chimba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za
maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Alisema kuwa Serikali
ya Mapianduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa elimu bure na kuwataka wazazi
wasitoe fedha kwa ajili ya matumizi ya ufagio na wala kununua chaki na badala
yake kazi hiyo ni ya Wizara na Serikali itatoa gharamia gharama zote.
Alisema kuwa jambo
hilo ni kubwa na Serikali itaendelea kugharamika kwa wananchi wake kwa kila
hali na lisilobudi litafanywa na kusisitiza kuwa elimu haina mbadala.
Rais Dk. Shein
aliwakata wazee kutochangia chochote na kama kuna mapungufu basi Serikali
itafanya kazi wenyewe la wala sio wao.
Alisema kuwa elimu
inatolewa bure kuanzia Chekechea, Msingi hadi Serkondari na kuwataka wananchi
kuwaepuka wale wanaosema uongo kuhusu Serikali yao ambayo imekuwa ikiendelea
kuimarisha sekta za maendeleo kila pembe ya Zanzibar.
Alieleza kuwa hadi
mwisho wa mwaka jana uchumi wa Zanzibar umekuwa kwa asilimia 7.7 na sio kweli
wale wanaosema kuwa uchumi wa Zanzibar umeanguka na kueleza kuwa kama ni hivyo
Serikali isingeweza kutoa elimu zote bure.
“Msiwasikilize waongo
wengine ni waongo na watu wazima hawaambiwi waongo....vile vile nataka
kukwambieni kuwa afya pia bure...kwani Serikali imeamua afya nayo kuwa bure
”alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alishangazwa
na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutoa takwimu za uongo na kuwataka
wananchi kuwasikiliza viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuachana
na wale wanaosema uongo kwa kuwadanganya wananchi.
Rais Dk. Shein
aliwasisitiza wananchi kuwaendeleza watoto wao kusoma ili waweze kujipatia
manufaa wao na nchi yao.
Aidha, alisema kuwa
wananchi wanaposhikana maendeleo makubwa yanapatikana na iwapo neema watazibeza
Mwenyezi Mungu huleta mtihani na kusisitiza kuwa hapana haja ya kuleta utani
katika elimu kwani imetukuka.
Alisema kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar haina mbadala na elimu
na itasimama kidete katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika huku
akitumia fursa hiyo kuwaahidi wananchi wa Chimba kuwa skuli yao itajengwa hadi
elimu ya Sekondari katika kijiji chao.
Rais Dk. Shein alisema kuwa kazi kubwa ya kuwapelekea
maendeleo wananchi wa Zanzibar inafanywa na CCM, hivyo aliwataka wananchi wa
Chimba wasidanganyike kwani hakuna mbadala wa elimu.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alisema kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni
kuwasomesha watoto wote ili waje kuwa wataalamu na kuwataka wazee kukaza kamba
na walimu nao kwa upande wao wawasaidia watoto.
Pia, aliwataka walimu
kuwasomesha na kuwasaidia vyema watoto pamoja na jamii nzima kwani zamani
watoto wakilelewa na Kiambo jambo ambalo hivi sasa halipo na kuitaka jamii
kuishi kwa mapenzi na kulea kwa pamoja watoto wao.
Rais Dk. Shein
aliiagiza Wizara ya Elimu kutafuta walimu haraka na kuwapeleka katika skuli ya
Chimba kutokana na upungufu wa walimu uliopo kwani Serikali inataka kwenda na
kasi ya CCM katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ikiwa
ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein alieleza kuwa umuhimu wa
elimu Zanzibar umeelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na chama cha ASP.
Alieleza kuwa wakati
kunaanzimishwa miaka 55 ni lazima kukubukwe mambo makubwa mazito yaliyofanywa
katika kupata ukombozi na uhuru wa Zanzibar.
Alisema kuwa ASP
ilipigania uhuru ili wananchi wa Zanzibar waishi bila ya kutawaliwa na
kuondosha madhila kwani wakoloni walikuwa wakipokezana katika kuitawala
Zanzibar.
Alisema kuwa zaidi ya
karne nne Zanzibar ilitawaliwa na kabla ya hapo Zanzibar haikutawaliwa na ilikuwa
huru na licha ya kutafuta uhuru kwa demokrasi haukupatikana na ndipo
yakafanyika Mapinduzi ya Januari 12, 1964 chini ya ASP na uongozi wa Mzee Karume.
Alisema kuwa mambo
makubwa aliyoyaahidiwa Rais Abeid Karume yalitekelezwa ikiwa ni pamoja na elimu
ambayo itakuwa yenye manufaa kwa watu wote tena bila ya ubaguzi, ardhi yote
itakuwa mali ya serikali na leo ndivyo ilivyo pamoja na wananchi kupata heka
tatu tatu, afya kuwa bure pamoja na elimu bure.
Alieleza kuwa mnamo
mwezi Machi mwaka 1965 Rais Abeid Karume alitangaza afya bure na hadi hivi leo
miaka 54 afya hailipiwi isipokuwa wananchi wanachangia tu jambo ambalo hakuna
hata nchi moja duniani inayofanya hivyo kama ilivyo kwa Zanzibar.
Alisema kuwa maendeleo
yote yanaletwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo sekta ya elimu.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alieleza kuwa wananchi wote wa Chimba wamefarajika kwa
kuona kwamba jengo hilo aliloliweka jiwe la msingi Rais Dk. Shein amelifungua
mwenyewe.
Alisema kuwa tayari
Wizara yake imeshajenga madarasa mengi sana na kutoapongezi kwa Dk. Shein kwa
uongozi wake kwa kuwapelekea maendeleo wananchi wote bila ya kujali vyama vyao
vya siasa, dini, rangi wala kabila.
Alisema kuwa tayari
madarasa mengi yameshajengwa yakiwemo madarasa ya kwenye skuli mpya za ghorofa ambapo
hadi sasa kuna skuli zisizopungua 600, na kutoa shukurani huku akiahidi Wizara
yake itaendelea kumuunga mkono Rais Dk. Shein
katika kuhakikisha malengo ya Mapinduzi yanaendelea kusimamiwa.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dk.
Idrisa Muslih Hija alieleza kuwa skuli hiyo ni miongoni mwa skuli zilizopo katika
Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo wazo la kuanzisha skuli hiyo
lilitokana na wananchi wenyewe ikiwa ni hatua ya kukabialiana na tatizo la
wanafunzi wanaoishi vitongoziji vya Bule, Jichwa, Maziwa njia na Pombwe kwa
kwenda masafa marefu.
Alieleza kuwa katika
ziara yake Rais Dk. Shein kijijini hapo mnamo Julai 22 mwaka 2017 wakati wa ziara yake alipokwenda kuweka jiwe
la msingi kituo cha afya Chimba ambapo
wananchi walipata fursa ya kueleza changamoto yao ya skuli na Rais aliahidi
kuwa Serikali itaunga mkono na Wizara pamoja na Halmashauri, wananchi , Mbunge
na Mwakilishi pamoja na wananchi wapenda maendeleo walitoa michango yao.
Alisema kuwa wanafunzi
wanaotarajiwa kuandikishwa darasa la kwanza katika maeneo ya Chimba ni 185
ambapo hadi hivi sasa wanafunzi
walioahikishwa ni 145 wakiwemo
wanafunzi 76 wanaotoka katika vituo vya TUTU na wanafunzi 69 wanaotoka mitaani.
Alieleza kuwa upande
wa wanafunzi wa maandalizi bado wanaendelea kuandikishwa katika vituo vya TUTU
ambavyo viko vitatu vilivypo katika Shehia ya Chimba na hadi sasa
vimeshaandikisha jumla ya wanafunzi 86.
Alisema kuwa Ujenzi wa
Skuli ya Chimba ulianza rasmi mnamo Juni 23 mwaka 2012, ambapo skuli hiyo ina
madarasa 4, vyoo,ofisi za walimu na hadi kukamilika kwa ujenzi huo umegharimu
Shilingi za Tanzania milion 92.5.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment