Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ashiriki Katika Tamasha la Mazoezi Kisiwani Pemba Leo.



Kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa maendeleo ya Zanzibar Awamu zote Saba za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanya jitihada mbali mbali za kuimarisha sekta ya michezo ikiwemo miundombinu ya michezo hasa ujenzi wa viwanja.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo leo huko katika uwanja wa Gombani Pemba mara baada ya kushiriki kikamilifu katika Bonanza maalum la Mazoezi ya Viungo ambalo lilianzia Wawi Matrekta hadi uwanja wa Gombani Chake Chake Pemba.

Mazoezi hayo ya viungo yalivishirikisha vikundi mbali mbali vya mazoezi kutoka Unguja, Tanzania Bara pamoja na wenyewe kutoka Pemba ambapo pia, yaliwashirikisha viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais  wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na wananchi.

Katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya mazoezi hayo ambayo hufanyika Kitaifa kila mwaka mnamo tarehe mosi ya mwezi wa Januari, Dk. Shein alisema kuwa katika Awamu ya mwanzo ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ulijengwa uwanja wa Amaan ambao ni wa kisasa wenye viwango vya Kimataifa uliofunguliwa rasmi mwaka 1970.

Aidha, katika Awamu ya Nne Marehemu Sheikh Idriss Abdulwakil alianzisha ujenzi wa uwanja wa Gombani Pemba.

Katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imefanya jitihada kubwa za kuimarisha miundombinu ya michezo ikiwa ni pamoja na kukifanyia matengenezo na kukiwekea majani ya bandia na mpira wa kukimbilia kiwanja cha Amaan na Gombani.

Vile Vile, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kimejengwa upya kiwanja cha michezo cha Mao Tse Tung ambacho kinaweza kutumika kwa michezo mbali mbali .

Kwa maelezo ya Rais Dk. Shein kiwanja hicho kinaweza kutumika kwa michezo ya mpira wa mikono, mpira wa wavu, mpira wa vikapu, mpira wa pete na mpira wa miguu hatua ambayo itaondokana na tatizo la uhaba wa viwanja vya michezo na kusaidia kuimarisha sekta ya michezo.

Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali imeanza hatua ya ujenzi wa kiwanja kimoja cha michezo kwa kila Wilaya ya Zanzibar kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020.

Aliongeza kuwa Serikali imekamilisha ujenzi wa uwanja wa  Kitogani katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja na hatua za ujenzi wa kiwanja cha michezo cha Kishindeni katika Wilaya ya Micheweni na kiwanja cha Kangani katika Wilaya ya Mkoani zinaendelea.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa maandalizi ya ujenzi wa uwanja wa Wilaya ya Kaskazini A huko Mkokotoni nayo yataanza hivi karibuni.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa bado ana imani kuwa iwapo utawekwa mbele uzalendo, ubunifu na kurudisha ari na hamasa ya kupenda timu za nyumbani kuliko za nje timu za nyumbani zitaweza kufanya vizuri katika mashindano.

Aliwahimiza wananchi kuzionea ufahari na kuzipenda timu za za nyumbani kwani mtu kukipenda chake si ila isipokuwa ni wajibu jambo ambalo ni ishara ya uzalendo na litasaidia kuwapa moyo wachezaji ili michezo iimarike zaidi nchini.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara na sekta binafsi kuziunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya michezo kwani michezo ina nafasi nzuri katika kuzitangaza biashara na inasaidia katika matamasha na kampeni za shughuli zinazofanywa na asasi za kiraia.

Alieleza jinsi anavyothamini jitihada za wawekezaji wote walioahamasika kuweka huduma za michezo katika hoteli za kitalii akiwemo Said Salim Bakhressa aliyeanzisha kichezo ya maji katika hteli ya Verde pamoja na mwekezaji Subash Patel aliyejenga kiwanja cha gofu katika hoteli ya Sea Cliff, Magapwani.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein  alitoa wito kwa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kuendelea kushirikiana ili walitumie Tamasha la Utalii la Zanzibar la kila mwaka katika kukuza michezo na kuimarisha sekta ya utalii ambayo inachangia pato la Zanzibar.

Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Taifa la Michezo pamoja na Chama cha Mazoezi ya Viungo (ZABESA) kwa maandalizi mazuri ya bonaza la mwaka huu ambalo kwa mara ya kwanza limefanyika kisiwani Pemba.

Nae Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Micezho Balozi Ali Abeid Karume  alieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya michezo.

Mapema Kamishna wa Michezo Sharifa Khamis alieleza kuwa Wanamichezo wamefarajika na juhudi za Rais Dk. Shein anazozichukua katika kuhakikisha michezo inakua na kuendelea na ndio maana akaamua kufanya matengenezo ya viwanja vya Amaan, Gombani, Mao Tse Tung.

Nao Uongozi wa ZABESA katika risala yao walieleza umuhimu wa mazoezi kwa mwanaadamu huku wakitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwakubalia maombi yao likiwemo kufanyika kwa Bonanza hilo kisiwani Pemba mwaka huu.

Pia, ujenzi wa viwanja vya kila Wilaya, kuwapatia eneo kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Taifa pamoja na kuziwezesha timu za Taifa kushiriki mashindano ya Kitaifa.

Pia, Kamishna huyo alimuarifu Rais Dk. Shein kuwa eneo la ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa michezo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 huko Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja limeshapatikana na limeshaanza kupimwa.

Katika hafla hiyo Rais Dk. Shein alitoa vyeti maalum kwa Vikundi Shiriki pamoja na waazilishi na viongozi wa ZABESA ambapo pia, Balozi Seif Ali Idd nae alitoa vyeti maalum kwa wadhamini wa Bonanza hilo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.