Habari za Punde

WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA KONDOA WAPATA NEEMA

Na Peter Haule, WFM, Kondoa
WANAFUNZI wote 3,287 waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma, wanatarajia kuanza masomo baada ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dkt. Ashatu Kijaji, kutoa msaada wa mabati 1080 ya kuezekea vyumba 20 vya madarasa.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Bw. Mustapha Semwaiko, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa kipaumbele chake kikubwa ni elimu na anataka kila mwanafunzi aliyefaulu na kuchaguliwa kuendelea na masomo anapata fursa hiyo ya kusoma.
"Tumeamua kutumia mfuko wa Jimbo, zaidi ya sh. 20m zimetumika kununulia mabati haya na niombe Mkurugenzi wewe ndiye mwenye watendaji mpaka ngazi ya vijiji na vitongoji ambako shule zetu zipo, mabati haya yafikishwe kwenye kila shule ili inapofika mwisho wa mwezi Februari, 2019, watoto wote waanze kusoma" alisema Dkt. Kijaji
Aidha, Dkt. Kijaji amewapongeza viongozi na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kwa jitihada zao za kukuza elimu na kufanikisha Wilaya hiyo kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2018 ambapo shule nane kati ya kumi zilizofanya vizuri katika Mkoa wa Dodoma, zinatoka Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
"Tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, hatuwezi kuwapeleka wanaKondoa wasio na elimu ndio maana tumefanya mapinduzi makubwa katika wilaya yetu kutoka kuwa ya mwisho kielimu katika Mkoa wa Dodoma miaka mitatu iliyopita hadi kuwa na shule 8 zilizofanya vizuri kati ya 10, kimkoa" aliongeza Dkt. Kijaji
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Bw. Mustapha Semwaiko na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya wilaya hiyo Bi. Hildegard Saganda, wamesema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka baada ya kuwa na wasiwasi wa namna ya kuwawezesha zaidi ya wanafunzi elfu 3 kupata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa uliokuwa ukiikabili Halmashauri ya Wilaya hiyo.
"Mbati haya yatapelekwa kwenye shule ambazo wananchi wamejenga maboma na zimefikia hatua ya lenta ambazo ni Busi, Kikore, Changaa, Kalamba, Itaswi, Kwadelo, Hondomairo na Loo" alifafanua Bi. Hildegard Saganda
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kondoa, ameelezea kuridhishwa kwake na namna Ilani ya CCM inavyotekelezwa katika wilaya yake katika nyanja mbalimbali na kumpongeza Dkt. Ashatu Kijaji kwa jitihada zake za kuiletea Maendeleo wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.