Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Ahusa Ufisadi Ukarabati wa Jengo la Songea. *Ni la wajawazito wanaosubiri kujifungua, limegharimu sh. milioni 129

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amenusa harufu ya ufisadi katika mradi wa ukarabati wa jengo la mama na mtoto  katika Hospitali ya Rufaa  ya Mkoa wa Ruvuma (HOMSO) na amesema kwamba hajaridhishwa na kiasi ya sh. milioni 129 zilizotumika.

Hivyo, amemuagiza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile afuatilie suala hilo ili kumbaini mtu ambaye amehusika katika kupitisha zabuni ya ukarabati wa jengo hilo na kisha kumpelekea taarifa.

Waziri Mkuu amenusa harufu ya ufisadi katika mradi huo leo (Jumamosi, Januari 5, 2019) wakati alipotembelea hospitali hiyo na kukagua ukarabati wa jengo la akinamama wajawazito wanaosubiri kujifungua (mama ngojea) ambalo umegharimu sh. milioni 129.

“Sijaridhishwa na gharama za ukarabati wa jengo hilo kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika kwani Serikali inajenga vituo vya afya vyenye jengo la maabara, jengo la kujifungulia, wodi ya mama na mtoto, chumba cha upasuaji, nyumba ya watumishi kwa gharama za sh. milioni 400 hadi 500 sasa inawezekajane jengo moja linalokarabatiwa ligharimu kiasi hicho.”

Waziri Mkuu amesema kila mtumishi wa umma lazima azingatie maadili ya kiutumishi na kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na Serikali. Amesema Serikali imeagiza miradi ijengwe kwa kutumia force accountna kuhakikisha miradi inalingana na thamani ya fedha.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia kikamilifu utoaji wa huduma ya watoto waliochini ya miaka mitano zinazotolewa katika hospitali kwani baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa wakiwatoza gharama za dawa wakati wanatakiwa watibiwe bure.

Waziri Mkuu amesema hayo baada ya Kanisia Fusi ambaye amelazwa na mtoto wake katika hospitali hiyo kumueleza kwamba ameandikiwa dawa na kuambia akanunue wakati mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu anatakiwa atibiwe bure.

Pia baada ya Dkt. Ndungulile kuangalia cheti cha mtoto huyo alisema dawa aliyoandikiwa ipo hospitalini hapo jambo ambalo lilithibitishwa na Mganga Mfawidhi wa hopitali hiyo Dkt. Majura Magafu, hivyo Waziri Mkuu amemuagiza mganga huyo amtafute mtendaji aliyemuambia mama huyo akanunue.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezindua mpango wa usambazaji wa x-ray za kidigitali ambazo zitazambazwa kwenye hospitali mbalimbali za rufaa za mikoa ili kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa kwa njia ya mionzi.

Waziri Mkuu amesema kwa kuanzia x-ray hizo zitasambazwa kwenye hospitali za rufani katika mikoa 11 na kisha baadae zitasambazwa kwenye hospitali zingine 20, lengo ni kuhakikisha hospitali zote za rufaa za mikoa zinakuwa na x-ray hizo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Ndungulile amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha huduma za nchini.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania wote karibu na maeneo yao ya makazi tena kwa gharama nafuu. ”Katika kufikia azma hii moja wapo ya kipaumbele ni kununua vifaa vya kisasa vinavyoendana na teknolojia iliyopo.”

Amesema kwa sasa wizara hiyo imenunua mashine 11 za x-ray za kidigitali zenye thamani ya zaidi ya shilingi 2,027,029,794.60 ambazo zimekusudiwa kupelekwa kwenye hospitali 11 zenye x-ray za zamani. Hospitali hizo ni Amana, Bukoba, Katavi, Morogoro, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Singida na zingine tatu zitafungwa katika hospitali za wilaya za Chato, Magu na Nzega.  

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 5, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.