Habari za Punde

Balozi Seif mgeni rasmi katika Kongamano la Mwaka la Tatu la Taasisi za Kiraia Zanzibar

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Mwaka la Tatu la Taasisi za Kiraia Zanzibar lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.+
 Mwakilishi wa Mradi wa Kusaidia Taasisi za Kiraia  Zanzibar {ZANSASP} kutoka Umoja wa Ulaya {EU} Bwana Fager Rayern akiwasilisha Salamu za Umoja wake kwenye Kongamano hilo la Asasi za Kiraia.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Mwaka la Asasi za Kiraia Zanzibar Bwana Bakari Omar Hamad akitoa Taarifa ya Kongamano hilo kwa Washiriki katika hafla ya Ufunguzi.
 Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed akiushukuru Umoja wa Ulaya {EU} kwa mchango wake mkubwa wa kusaidia Mradi wa kuzijengea uwezo Taasisi za Kiraia Zanzibar alipokuwa akijiandaa kumkaribisha Mgeni Rasmi.
 Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Mwaka la Tatu la Asasi za Kiraia wakifuatilia hatua za ufunguzi wa Kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Asasi za Kiraia pamoja na washiriki wengine wa Kongamo la Taasisi za Kiraia lililofunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema imani sahihi itakayoendelea kuwekwa na Taasisi mbali mbali za Kiraia kwa Serikali ndio nia ya dhati katika kuweka mazingira mazuri yatakayoziwezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Alisema Asasi za Kiraia ni miongoni mwa washirika Wakuu wenye dhamana na kuwaunganisha Wananchi na Serikali yao katika kusimamia utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akilifungua Kongamano la Mwaka la Tatu la Asasi za Kiraia lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini na kushirikisha zaidi ya Wawakilishi wa Taasisi za Kiraia zipatazo 150 kutoka Unguja na Pemba.
Alisema Serikali iko katika utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini { MKUZA 111} ambapo katika Mkakati huo Taasisi za Kiraia zimepewa majukumu endapo  zitafanya kazi vyema zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha Mkakati huo.
Balozi Seif alizishauri Taasisi zote za Kiraia pamoja na Sekta Binafsi hapa Nchini kuusoma Mkakati huo na baadae kuufanyia kazi ipasavyo kwa maslahi yao, Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Alieleza kwamba Kundi hilo linapaswa kuzingatia kwamba shughuli wanazozifanya au wanazokusudia kuzitekeleza ziwe za kudumu ili kuzipa uwezo wa kupambana na changamoto mbali mbali zinazowakabili.
“ Ni muhimu sana kuilenga Jamii ya Wazanzibari katika kupambana na kero mbali mbali ikiwemo tatizo la Umaskini”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na Taasisi za Kiraia hivi sasa  kuwa na ukaribu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  uliopelekea ushiriki wa Taasisi hizo katika utengenezaji wa Sera mbali mbali za Kitaifa .
Alisema ipo Sera ya Serikali za Mitaa ambayo hivi sasa utekelezaji wake unakwenda kwa kasi kupitia mfumo wa Ugatuzi wa Madaraka kutoka katika Serikali Kuu na kwenda kwa Wananchi.
“ Ni vyema Taasisi za Kiraia zikajipanga na kushiriki kikamilifu katika kufanikisha suala la Ugatuzi wa Madaraka Mikoani”. Alisema Balozi Seif.
Alionyesha matumaini yake kutokana na baadhi ya Taasisi hizo kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Wadi na Kamati za Mashauriano za Shehia. Hivyo kuwemo kwa vyombo hivyo kutasaidia kuwasilisha mawazo ya Wananchi katika maamuzi yenye manufaa kwa Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Jumuiya ya Nchi za Ulaya {EU} kwa kukubali kugharamia kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Programu hiyo muhimu ya ZANSASP iliyosaidia kuzijengea uwezo Taasisi za Kiraia hapa Zanzibar.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Mwaka la Asasi za Kiraia Zanzibar Bwana Bakari Omar Hamad alisema Taasisi nyingi za Kiraia Nchini hivi sasa zimepata maendeleo makubwa kiutendaji yanayowawezesha kutekeleza malengo waliyojipangia.
Bwana Bakari alisema yapo matumaini makubwa ya mueleko wa Taasisi hizo kutokana na ongezeko kubwa lililopelekea Taasisi kadhaa kuanzishwa hali iliyofikia kuwa na zaidi ya Taasisi 150 Unguja na Pemba.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Mwaka la Asasi za Kiraia aliihakikishia na kuithibitishia Serikali Kuu kuendelea kushirikiana nayo kutokana na kuziunga mkono katika mazingira ya kujiendesha kimafanikio.
Akitoa salamu Mwakilishi wa Mradi wa Kusaidia Taasisi za Kiraia  Zanzibar {ZANSASP} kutoka Umoja wa Ulaya {EU} Bwana Fager Rayern alisema Umoja wa Ulaya utaendelea kuiunga Mkono Zanzibar kwa kuzisaidia Taasisi za Kiraia zifikie malengo ya kujitegemea zaidi.
Bwana Fager alisema masuala ya Taaluma yanazingatiwa zaidi katika kuzijengea Uwezo wa Kiutendaji Taasisi hizo ambapo kwa sasa inatia moyo kuona zaidi ya Asilimia 49% ya Taasisi zilizopo Nchini zinasimamiwa na Akina Mama.
Aliwapongeza Akina Mama waliojitolea kuanzisha Taasisi zao zitazokuwa mkombozi wa harakati zao za kujikwamua kiuchumi pamoja na kuondokana na ukali wa Maisha.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kulifungua Kongamano hilo Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed ameushukuru Mradi wa kusaidia Asasi za Kiraia Zanzibar {ZANSASP} unaosimamiwa na Umoja wa Ulaya { EU} kwa kusaidia maendeleo ya Taasisi za Kiraia Zanzibar.
Dr. Khalid alisema Mradi huo uliotiwa saini Mwaka 2013 na kuanza kazi Mwaka 2015 umezisaidia Taasisi za Kiraia Zanzibar kwa Jumla ya Euro Milioni Tatu ambapo hadi sasa asilimia 90% ya Fedha hizo zimeshatumika ikibakia Asilimia 10%.
Alisema Mradi huo umesaidia kujenga mazingira bora  ya kiutendaji kwa Taasisi hizo licha ya uwepo wa awali wa kutoaminiana kati ya Taasisi hizo na zile Taasisi za Serikali.
Waziri wa Fedha alifahamisha kwamba bado zipo Taasisi nyingi hazijafikiwa na Mradi huo na kumuomba Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya {EU} kuzishawishi Taasisi za Umoja huo ziendelee kuangalia uwezekano wa kuunga mkono mpango huo ili kuzifikia na zile Taasisi zilizobakia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.