Habari za Punde

Majumuisho ya Ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Ali Mohamed Shein.Wilaya ya Magharibi A,Unguja
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa migogoro ya ardhi iliyopo katika Wilaya ya Magharibi A, inachingiwa na baadhi ya viongozi wa Wilaya hiyo ambao wanajihushisha na migogoro hiyo.  

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika Majumuisho ya ziara yake ya Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi katika ukumbi wa Kituo cha Utengamano Welezo mjini Zanzibar ambapo Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa chama na Serikali walihudhuria.

Katika hotuba yake ya Majumusho, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wilaya hiyo kutojihusisha na migogoro hiyo na badala yake wawasaidie wananchi kuondokana na migogoro hiyo ya ardhi.

Aliongeza kuwa tayari Zanzbar kuna Sheria sita za Ardhi hivyo hakuna sababu za kuwepo migogoro hiyo ambayo haileti tija wala manufaa.

Dk. Shein alieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia migogoro na kusema kuwa yeye anapochagua viongozi hachagui kwa lengo la kusemwa vibaya Serikali na badala yake huchagua kwa lengo la kuwasaidia wananchi ambapo wapo baadhi viongozi wanafanya kinyume na lengo hilo.

Aidha, alieleza kuwa katika ziara yake hiyo ya Wilaya ya Magharibi A, kuna mambo amaeyaona ambayo yapo kinyume na utaratibu  hivyo, aliitaka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ pamoja na uongozi wa Mkoa na Wilaya hiyo kuyatafutia ufumbuzi.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika ziara yake hiyo akiwa eneo la Chuini alikuta gari za mawe, wauza miti pamoja na soko ambavyo vyote hivyo vipo kinyume na utaratibu huku viongozi wa Wilaya wakiiona hali hiyo na kuifumbia macho hivyo, aliwataka kuifuatilia hali na kuitafuta ufumbuzi wa haraka.

Dk. Shen alisikitishwa kuona agizo alilolitoa siku za nyuma la kuondoshwa kwa gari za mawe katika eneo la Mwanakwerekwe likiwa bado halijafanyiwa kazi na bado gari hizo zimeendelea kuwekwa katika eneo hilo na kuleta usumbufu kwa wapita njia.
Alieleza kuwepo kwa gari za Mawe katika eneo la Welezo pamoja na kujaa kwa wauza miti katika eneo hilo pamoja na lile la Mwera kwenye kituo cha mafuta kuwa kituo cha gari za mawe si jambo la busara na viongozi wanatakiwa kuchukua hatua stahiki.

Dk. Shein alishangazwa kuwa hivi sasa katika eneo hilo gari za mchanga zinaengeshwa barabarani kinyume na utaratibu pamoja na kueleza hatua za uchimbaji wa rasilimali hiyo zilivyofanywa hali ambayo imechangia mchanga Zanzibar kuadimika.

Alieleza kuwa wapo baadhi ya watu wameuficha mchanga likiwemo eneo la Chechele hali ambayo imezidisha kuwepo uhaba wa mchanga hali inayopelekea hadi baadhi ya ujenzi wa miradi ya Serikali kusuasua ukiwemo ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) kutokana na uhaba wa rasilimali hiyo hapa nchini hivi sasa.

Alisema kuwa mchanga na mawe ni mali ya serikali akiwa na maana kwamba ni mali ya watu wote hivyo, alishangazwa na wale waliozihodhi mali hizo katika maeneo yao huku wakiwaacha wananchi wakipata tabu kusaka rasilimali hiyo.

Hivyo, aliutaka uongozi huo wa Wilaya kuwasimamia wenye gari za mawe na mchanga kwa lengo la kuyaondosha katika maeneo ambayo hayajaruhusiwi  na kuutaka uongozi  wa Wilaya hiyo kuongeza mapato kutokana na kuwepo kwa vianzio vingi vya mapato.

Rais Dk. Shein alieleza haja kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Makaazi pamoja na uongozi wa Mkoa na Wilaya hiyo kushirikiana katika kuangalia miundombinu ya maji ili maji machache yaliopo wananchi waweze kuyapata na kuyatumia ipasavyo.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa uongozi wa Wilaya hiyo  kuongeza kasi katika kusimamia masuala mazima ya udhalilishaji huku akipongeza hatua zilizochukuliwa na Wilaya hiyo katika kupambana na janga hilo hatari.

Ameeleza furaha yake kutokana na makusanyo ya fedha na kuwapongeza kwa kukusanya mapato ya wastani Bilioni 1.5 ambalo ni ongezeko la asilimia 14 ya makadiria yao nan kuvuka lengo walilojiwekea pamoja na kufanya vizuri katika masuala ya kesi za udhalilishaji, ajira kwa vijana kwa kukusanya nguvu ili waweze kujiajiri.

Aliwapongeza kwa kufanya vizuri katika masuala ya ulinzi na usalama kwa kupambana na wezi, vitendo vya wizi wa kutumia nguvu ambapo wengine hutumia silaha katika kutekeleza hujuma hizo.

Pia, alitoa pongezi zake kwa kukusanya nguvu kwa vikundi vya vijana katika Wilaya hiyo kwa azma ya kutaka kujiajiri wenyewe pamoja na mafanikio mengine.

Kwa upande wa changamoto ya uhaba wa maji, Rais Dk. Shein alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupunguza changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kuutumia mkopo wa Dola za Marekani 92 kutoka Exim Benki ya India ambapo tayari maandalizi ya kukusanya tenda yameshaanza.

Aidha, katika kutatua changamoto ya maji, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Shehia 26 zikiwemo za Mji Mkongwe na maeneo mengine ya Mji wa Zanzbar zitafaidika na Mradi wa maji wa ujenzi wa matangi ya maji ya Saateni na Mnara wa Mbao mradi utakaogharimu TZS Bilioni 37.1 ambao unatarajiwa kumalizika mwezi Disemba mwaka huu 2019 ambao tayari umeshafikia asilimia 55 ya utekelezaji.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alieleza hatua zinazochukuliwa na  Ofisi hiyo katika kutatua changamoto kadhaa zilipo ambazo zilikuwa ni vikwazo kwa wananchi.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Wilaya ya Magharibi  A, Mkuu wa Wilaya hiyo Kepteni  Khatib Khamis Mwadini alisema kuwa Wilaya hiyo inatekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA III), Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) na Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020.

Akieleza miongoni wa changamoto alisema ni pamoja na uhaba ajira ambapo alieleza hatua walizozichukua katika kuhakikisha ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi ambavyo vimepewa taaluma.

Alisema kuwa Wilaya hiyo inakabiliwaa na wimbi 114 ziliripotiwa zikiwemo kesi za wazazi kutowahudumia watoto wao, ubakaji na nyenginezo ambapo imejipangia mkakati wa kutoa mafunzo ya kujilinda na udhalilishaji zikiwemo kuunda Kamati pamoja na kuitumia sanaa na mikutano kadhaa kati yao na wananchi.

Mkuu wa Wilaya hiyo alieleza kuwa huduma ya maji safi na salama bado haiko vyema na inapelekea wananchi wa maeneo hayo kuhangaika katikam kutafuta huduma hiyo ya maji hali ambayo inapelekea kudhorotesha utendaji wao wa kazi.

Alieleza kuwa migogoro ya ardhi imekuwa ikijitokeza katika Wilaya hiyo na kueleza mikakati iliyowekwa ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia watu wanaojenga bila ya kuwa na Vibali vya ujenzi.

Nae Mwenyekiti wa Wilaya ya Mfenesini akisoma ripoti ya Wilaya hyo kwa ufupi alitoa pongezi kwa niaba ya viongozi na wanaCCM wa Wilaya hiyo huku akiahidi kuwa ushindi katika Majimbo yote sita ya Wilaya hiyo ni lazima kwa CCM.

Akitoa neno la shukurani, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud alisifu hekima na busara za Dk. Shein katika uongozi wake hatua ambayo inasaidia katika kuleta maendeleo endelevu.

Alimuahidi Rais kuwa yale yote aliyowaelekeza watayafanyia kazi hasa migogoro ya ardhi, maegesho ya gari za mawe na mchanga katika maeneo yasiyoruhusika pamoja na kuongeza bidii na mkazo katika suala la udhalilishaji na ukusanyaji wa mapato pamoja na mengineyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.