Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Afungua Ukumbi wa Kisasa wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni leo Kisiwani Pemba.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kuashiria kuufungua Ukumbi wa Mikutano wa Kisasa wac Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Kisiwani Pembe wakati wa ziara yake Kisiwani Pemba leo.kulia Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.Bi,Radhia Rashid Haroub. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,amesema Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, utasaidia sana kufanikisha maandalizi ya mikutano ya Chama na Serikali na kuondokana na utaratibu uliopo wa shughuli hizo kufanyika katika kumbi za Skuli. 

Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipofungua ukumbi mpya wa kisasa wa mikutano unaomilikiwa na Halmshauri ya Wilaya Micheweni, hafla iliyokwenda sambamba na kuzungumza na viongozi na wanachama wa CCM, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake kisiwani Pemba.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa ukumbi huo ni fursa adhimu kwa wananchi wa Wilaya hiyo pamoja na taasisi za chama na Serikali kupata fursa ya kufanya mikutano yao, na kuondokana na utaratibu uliozoeleka wa mikutano ya aina hiyo kufanyika katika kumbi za skuli wakati wanafunzi wanaendelea na masomo.

Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Halmshauri hiyo kwa kujenga ukumbi mzuri na wa kisasa na kuwataka watendaji wake kuutunza ili uwe endelevu pamoja na kuutumika kwa njia zilizo bora na zitakazoweza kuwanufaisha.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alisema Zanzibar itaendelea kutumia Katiba na Sheria katika matumizi ya ardhi na kubainisha kuwa ardhi itaendelea kuwa mali ya serikali na hakutakuwa na mtu mwenye mamlaka ya kuhodhi rasilimali hiyo.

Dk. Shein alisisitiza haja ya viongozi na wanachama wa CCM kuendelea kuwa na umoja na kubainisha kuwa hatua hiyo ndio chachu ya ushindi wa chama hicho sambamba na kuwataka kuepuka kutengeneza migogoro.

Mapema Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi (OR), Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ, Bi.Radhia Rashid alisema ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Halamshauri ya Wilaya Micheweni, uliopo kwa Shaame Mata Micheweni umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 441.9 hadi kukamilika kwake.

Alisema fedha za ujenzi huo zimetokana na makusanyo ya Halmshauri (shilingi Milioni 113), Mfuko wa Maendeleo wa Mbunge wa Jimbo la Micheweni (shilingi Milioni 11) pamoja na Serikali kuu kupitia bajeti ya 2018/19 iliyochangia zaidi ya shilingi Milioni 297.8.

Alisema ukumbi huo unauwezo wa kuchukuwa wastani wa watu 350, ambapo pia unahusisha ukumbi mdogo wa mikutano unaochukuwa watu 30, chumba cha kupumzikia wageni mashuhuri, jukwaa, vyumba vya kubadilishia mavazi, ukumbi wa chakula pamoja na vyoo.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa ukumbi huo kutasaidia sana shughuli za kibiashara na kiuchumi ambazo zitachangia kuongeza mapato ya Halmshauri hiyo pamoja na wajasiriamali wa maeneo ya Micheweni.

Aidha,alisema kuwepo kwa ukumbi huo ni ukombozi kwa taasisi za umma na binafsi ambapo utaweza kutumika katika shughuli za makongamano, mikutano na shughuli mbalimbali za kijamii. 

 Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822

 E-mail: abdya062@gmail.com 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.