Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Afungua Barabara na Kituo cha Afya Kiyuni na Ngomeni Pemba.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema uamuzi wa Serikali kujenga Barabara ya Kuyuni hadi Ngomeni pamoja na Ujenzi wa Kituo cha Afya Ngomeni,  umekuja kufuatia eneo hilo kuzalisha kiwango kikubwa cha zao la karafuu.

Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipofungua barabara ya Kuyuni hadi Ngomeni yenye urefu wa kilomoita 3.2, iliojengwa kwa kiwango cha Lami pamoja na kituo cha Afya , ujenzi uliofanikishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema ili zao hilo liweze kuimarika ipasavyo, Serikali ililazimika kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo barabara, maji safi na salama, ujenzi wa kituo cha Afya pamoja na elimu.

Alisema ili Taifa liweze kupata maendeleo kuna umuhimu wa wananchi kuishi kwaa amani, umoja, ushirikiano na mapenzi makubwa.

Aidha alisema juhudi za ujenzi wa barabara na kituo hicho cha Afya, utaenda na na ujenzi wa barabara ya Mgelema hadi Wambaa, kazi itakayotekelezwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Alisema maendeleo makubwa yaliopatikana katika eneo hilo yanatokana na uzalishaji mkubwa wa karafuu, hivyo akawapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa kuuza karafuu zao ZSTC na kuondokana na utaratibu wa kusafirisha kwa njia za magendo.

Alisema uwepo wa barabara safi kuwa nimiongoni mwa faida kubwa ambapo itaweza kuwarahisishia wananchi kupeleka wagonjwa, ikiwemo wajawazito

Aidha, alisema kabla ya mapinduzi, huduma zote muhimu zilikosekana katika maeneohayo kwa vile wakoloni hawakujali maisha ya wananchi hao.
                                                                                               
Dk. Shein aliwataka wananchi kukaa pamoja na Wawakilishi wao ili waweze kusaidia upatikanaji wa gari la wagonjwa (ambulance) ili kusaidia usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma za ziada katika Hospitali kuu.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alimtaka Katibu Mkuu Wizara Afya kujipanga na watendaji wake na kuainisha gharama za ujenzi wa kituo cha Afya Ngomeni, baada ya kushindwa kubainisha katika taarifa yake.

Vilevile, aliitaka Wizara hiyo kuanza matayarisho ili kuhakikisha kituo hicho kinakuwa na watendaji wa kutosha katika nyanja zote, ili kiweze kutoa huduma bora kwa jamii.

Mapema, Waziri wa Nchi, (OR), Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ, Haji Omar Kheir alisema kulikuwa na sababu za kutosheleza hadi Serikali kuamua kujenga Kituo cha Afya Ngomeni, kwa msingi kuwa eneo hilo ni kianzio kikuu cha mapato ya Serikali, kutokana na uzalishaji mkubwa wa karafuu.

Alisema katika msimu wa mwisho wa Karafuu, eneo hilo lilizalisha wastani tani 246.7 pekee na kuongoza kisiwani humo.

Nae, Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji, Sira Ubwa Mamboya, alisema ujenzi wa Barabara ya Kuyuni hadi Ngomeni ni uthibitisha wa juhudi za Serikali za kuwafikishia huduma muhimu na miundombinu wananchi wake.

Alisema Wizara yake itaendelea kuzifanyia matengenezo barabara mbalimbali Unguja na Pemba ili kuhakikisha zinapitika muda wote.

Aliwataka wananchi kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu kwa kuzingatia kuwa ujenzi wa barabara huhitaji fedhan yingi..

Aidha, Katibu Mkuu wa Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe alisema Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 3.2 imegharimu zaidi ya shilingi Milioni 436 hadi kukamilika katika kiwango cha lami, wakati ambapo katika kiwango cha kifusi iligharimu zaidi ya Shilingi Milioni 225.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo utawasidia wananchi wa maeneo hayo kuondokana na kadhia ya usafiri pamoja na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kuelekea maeneo mengine.

Katibu MkuuWizara ya Afya Asha Abdalla, alisema ujenzi wa kituo cha Afya Ngomeni, unafanikisha sera ya Afya nchini inayolenga kuwafikishia huduma za afya wnanachi karibu na maeneo yao.

Wakati huohuo, Rais wa Zanzibar alipokea taarifa za Utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na Utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/18 na kusema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wake.

Taarifa ya hali ya kisiasa katika Wilaya hiyo imebainisha kushamiri, hivyo kutoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila kikwazo.

Katika nasaha zake, Dk. Shein aliwasitiza viongozi wa Chama na Serikali Wilayani humo, kuendeleza umoja na mashirikiano ili kujijengea mazingira bora ya ushindi chama hicho.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.