RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye
pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mpango wa kujenga uwanja wa ndege wa
kisasa kisiwani Pemba ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake Chake Pemba
wakati alipofanya mazungumzo na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Chake Chake pamoja
na kufanya majumuisho ya ziara ya Wilaya hiyo ambapo viongozi mbali mbali wa
Chama na Serikali walihudhuria akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema
Shein.
Katika maelezo yake
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Rais Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na CCM ni kujenga uwanja mpya na wa kisasa
wa ndege kisiwani Pemba utakaoruhusu kutua ndege kubwa za aina zote.
Alieleza kuwa uwanja
huo utakuwa wa kisasa na mkubwa utakaoruhusu ndege za aina zote kubwa kutua
katika kiwanja hicho hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa usafiri wa anga
katika kisiwa hicho na Zanzibar kwa jumla.
Alieleza kuwa tayari
mchakato wake wa mwanzo umeanza na ameshatuma Mawaziri kumi kwenda kwa wananchi
wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa uwanja wa ndege kisiwani Pemba wakiwemo
wananchi wa Mfikiwa, Furaha na Mvumoni ili wakae tayari mara tu ujenzi
utakapoanza waweze kuondoka katika eneo hilo na kupewa fedha kwaajili ya mali
zao.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa tayari upembuzi yakinifu umeshafanywa kwa ajili ya uwanja huo mpya wa
ndege na karibu TZS milioni 500 zimetumika na hivi sasa Serikali imo katika
hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo na kuwataka wananchi
kuwa na subira hasa wale wanaoishi pembezoni mw auwanja huo na kuahidiwa kupewa
fidia mara tu ujenzi utakapoanza.
Aidha, Dk. Shein amewasisitiza
Wawakilishi wa CCM wa Majimbo yaliyomo katika Wilaya ya Chake Chake kuongeza
kasi ya kushirikiana kwa kwenda kufanya kazi nyumba ili kuwashughulikia
wananchi kwa azma ya kutatua changamoto walizonazo.
Makamu Mwenyekiti huyo
wa CCM alitoa pongezi kwa taarifa nzuri zilitolewa na Wilaya hiyo ikiwemo ile
ya Chama na Serikali pamoja na kuzipongeza taarifa zote za Mikoa yote miwili ya
Pemba na Wilaya zake nne.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa ujenzi wa barabara ya Chake Chake-Mkoani pamoja na barabara ya
Chake Chake-Wete azma ya ujenzi huo iko pale pale kwani barabara zote hizo
zimetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 na tayari mchakato
wake umeanza.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alisisitiza haja kwa viongozi kuzisoma Sheria zote zinazopitishwa
katika Baraza la Wawakilishi ili iwe rahisi katika utendaji wa kazi zao pamoja
na kuwaelekeza wananchi juu ya mamabo mabli mbali ambayo hawayajui.
Rais Dk. Shein
alisisitiza haja kwa viongozi wote wa Serikali wakiwemo Maofisa wa Vikosi
kufanya kazi zao kwa uadilifu kwa kufuata taratibu, Kanuni na Sheria zilizopo
kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa kazi zao na kuleta ufanisi zaidi.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein ameendelea kueleza kuwa ardhi yote ya Zanzibar ni mali ya Serikali
hivyo hakuna haja ya kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi.
Ameeleza kuwa ziara
hiyo imefana sana na mafanikio aliyoyaona ni mengi kuliko changamoto zilizopo
huku akisisitiza haja ya kutekelezwa kwa maagizo yote aliyoyaelekeza na kuahidi
kufanya ziara nyengine baada ya miezi minane.
Nao viongozi wa CCM wa
Wilaya ya Chake Chake pamoja na Mkoa mzima wa Kusini Pemba walitoa pongezi kwa
Rais Dk. Shein kwa ziara yake hiyo ambayo imewapa ari kubwa katika utendaji wa
kazi zao.
Viongozi hao walitumia
fursa hiyo kutoa pongezi za pekee kwa Rais Dk. Shein kwa kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya CCM kwa vitendo na kusisitiza kuwa tayari Makamu huyo Mwenyekiti wa
CCM Zanzibar ameshatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa
asilimia mia moja.
Walieleza kuwa ziara
yake hiyo ambayo aliianza katika kisiwa cha Unguja mnamo Februari 12 mwaka huu
2019 na kuanza kisiwani Pemba mnamo Februari 21 mwaka huu 2018 imeleta tija
kubwa na mafanikio sambamba na kuzidisha mashirikiano kati ya uongozi wa Chama
cha CCM na Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment