Habari za Punde

SERIKALI YAZUIA SH. BILIONI 5.5 ZA UJENZI WA MRADI WA SOKO LA KISASA LA MAGOMENI DAR ES SALAAM

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati) akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya Kimkakati ikiwa ni pamoja na Soko la Magomeni Jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Daniel Chongolo na Kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Aron Mjuli.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati) akisikiliza maelezo ya Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Justin Lukaza, kuhusu ramani ya Mradi wa Kimkakati wa Soko la Magomeni Jijini Dar es Salaam lenye ghorofa tatu ambalo limepewa kiasi cha Sh. bilioni 3.5, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa unasuasua.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akitoa maelekezo ya Serikali ya kuzuia Sh. bilioni 5.5 zilizosalia kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Kimkakati wa Soko la Magomeni Jijini Dar es Salaam kwa kuwa tangu fedha hizo zilipotolewa Mei, 2018 utekelezaji wake hauridhishi. Kulia ni Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Jastin Lukaza.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa pili kushoto), akionesha kushangazwa na kitendo cha Mkandarasi wa Mradi wa Kimkakati wa Soko la Magomeni Jijini Dar es Salaam kutokuwepo eneo la mradi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Daniel Chongolo, wa pili kulia ni Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Jastin Lukaza na watatu kulia ni Mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi Bw. Sospeter Leonidas kutoka Kampuni ya GSI.
Muonekano wa eneo la Mradi wa Kimkakati wa Soko la Magomeni Jijini Dar es Salaam, ukiwa katika hatua za awali za maandalizi, wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipotembelea mradi huo ambao hadi kukamilika kwake utagharimu Sh. bilioni 9.
Mwenyekiti wa Soko la Magomeni Yusuph Waziri, akifafanua jambo mbele ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi  wa Soko la Kisasa la Magomeni, Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
                               (Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imezuia Sh. bilioni 5.5 ambazo zilipaswa kutumika kutekeleza mradi wa Kimkakati wa Soko la Magomeni, liliko wilaya ya Kinondoni,  Jijini Dar es Salaam kutokana na kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mradi huo licha ya kupewa fedha za kutosha kwa awamu ya kwanza.
Hatua hiyo imechukuliwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mradi huo unaotarajia kugharimu shilingi bilioni 9 na kukuta ujenzi wake unasuasua.
Dkt Kijaji alisema kuwa  Serikali, imeipatia Manispaa ya Kinondoni shilingi bilioni 3.5 tangu mwezi Mei, 2018 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao ungepaswa ukamilike ndani ya miezi tisa tangu kusainiwa kwa mkataba wa ruzuku hiyo lakini ameshangaa kutomkuta mkandarasi kwenye eneo la ujenzi.
“Serikali inasitisha kutoa kiasi cha Sh. bilioni 5.5 mpaka watakapo dhihirisha wako tayari kuwahudumia wananchi na kutekeleza dhamira njema ya Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya kuwahudumia wananchi wake”, alieleza Dkt. Kijaji.
"Jana Manispaa ya Ilala wametuangusha kwenye usimamizi wa mradi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti tumerejesha shilingi bilioni 3 Hazina na leo Manispaa ya Kinondoni nao wametuangusha na tunalazimika kuzizuia fedha hizo sh. bilioni 5.5 mpaka tujiridhishe na maendeleo ya ujenzi" alisisitiza Dkt. Kijaji
Awali, akitoa maelezo ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi wa Manispaa hiyo Justin Lukaza, ameeleza kuwa Manispaa hiyo imeingia mkataba wa kujenga soko hilo litakalo kuwa na ghorofa tatu na Kampuni ya Group Six International na kwamba ujenzi ungekamilika katika kipindi cha miezi sita ijayo na kutofautiana maelezo na mwakilishi wa Mkandarasi ambaye alimweleza Dkt. Kijaji kuwa ujenzi huo ungechukua muda wa  miezi 12.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Daniel Chongolo, amekiri kuwa kuna uzembe umefanywa na watendaji wa Manispaa ya Kinondoni uliosababisha mradi huo kuchelewa kuanza na kumwomba Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji ampe muda mfupi wa kurekebisha kasoro hizo.
Alisema kuwa tayari kuna hatua mbalimbali zilichukuliwa kwa maafisa waliofanya uzembe katika utekelezaji wa mradi hapo awali na hakujua kama bado kulikuwa na uzembe uliokuwa unaendelea baada ya kuchukua hatua hizo kwa sababu aliamini watendaji waliokabidhiwa kusimamia ujenzi wa mradi huo walijifunza kutokana na makosa ya wenzao walioondolewa kusimamia mradi huo
"Mimi nakubaliana na wewe (Naibu Waziri wa Fedha) kwamba kuna uzembe na kazi yetu sisi ni kuhakikisha tunarekebisha haya makosa na nichukue dhamana na tutawajika na watu hawa na nitalazimika kutumia dhana ya punda mwenye mzigo na mwenye punda anaye mchapa bakora ili punda aende" alisisitiza Bw. Chongolo
Baadhi ya wakazi wa Kinondoni, wameipongeza Serikali kwa ufuatiliaji wa miradi ya wananchi na kusikiliza kero zao wakitolea mfano wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, na kwamba hatua hiyo inaleta uwajibikaji wa watendaji ambao walijenga mazoea ya kuzembea kwa makusudi kusimamia miradi ya wananchi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuliletea Taifa maendeleo
Mradi wa Soko la Kisasa la Magomeni ni miongoni mwa miradi 22 iliyopewa ruzuku na Serikali katika Mpango wa Awamu ya Kwanza wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kujitegemea kimapato ambapo zaidi ya shilingi bilioni 147 zilitolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.