Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Amaliza Ziara Yake Wilaya ya Kusini Unguja leo Kwa Kuzungumza na Viongozi wa Wilaya hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,akizungumza na Viongozi wa Chama na Serikali katika Mkutano wa Majumuisho ya ziara yake Wilaya ya Kusini Unguja leo, kukamilisha ziara yake katika Mikoa ya Mjini Magharibi, Kaskazini na kumalizia leo Kusinu Unguja.
Na. Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar 20/02/2019
Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameweka msimamo wa Chama hicho kwamba kitawapitisha kugombea katika nafasi za uongozi wale tu wenye mapenzi ya dhati na moyo wa kukitumikia Chama hicho.
Dk Shein ametoa msimamo huo wakati akihutubia Wanachama na Wanachi katika Ukumbi wa Hoteli ya Residence Kizimkazi ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua shughuli za Chama na Serikali katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesisitiza kwamba Chama kitawapitisha wale wote wataaobainika kufuata vyema taratibu na miongozo mbali mbali ya Chama na wale wasiokuwa na sifa wasipoteze muda kugombea.
“Nasema wazi asiyekitumikia Chama Fomu za kugombea hapewi, asigombee bure” alitahadharisha Dk Shein.
Amewasisitiza Viongozi wa Chama na Serikali kufuata vyema maadili ya kazi zao ili kuwaletea wananchi maendeleo kama walivyoahidi.
“Chama kina maadili yake na Serikali ina maadili yake asiyeweza kufuata maadili aache” alisisitiza Dk. Shein.
Ameendelea kutoa indhari kwa Viongozi mbali mbali hasa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa na lugha nzuri wakati wa kuchangia hoja mbali mbali ili kuepuka kuichafua Serikali na Chama kwa ujumla.
Hata hivyo amesisitiza kuwa Wajumbe hao hawakatazwi kuihoji Serikali kwa vile ndio wajibu wao wa msingi lakini wanapaswa kuzingatia lugha nzuri wakati wa mijadala.
“Serikali zote Duniani zinahojiwa Wajumbe wanapaswa pia kuhoji lakini kwa kuzingatia kauli nzuri” alibainisha Dk. Shein
 Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi Dk. Shein amesema Serikali yake imeendelea kutekeleza vyema ahadi zake alizoahidi kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Aidha ameongeza kuwa zipo shughuli mbali mbali za kimaendeleo zinazoendea kutekelezwa na Serikali yake ambazo hazipo katika Ilani ya CCM.
Miongoni mwa hizo ni ujenzi wa Daraja la Kibonde mzungu na Barabara ya Mwanakwerekwe ambazo zinajengwa kwa gharama kubwa lakini hazipo katika Ilani ya CCM
Dk. Sheini aliwahimiza viongozi kwenda katika Majimbo yao ya uchaguzi kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.
“Wakati ni sasa, sisi tunapita kusikiliza changamoto na kuzipatia ufumbuzi Viongozi nanyi mwende Majimboni kwenu kutekeleza kile mlichoakiahidi” aliwanasihi Viongozi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrisa Kitwana Mustafa wakati akisoma Taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbali mbali za kimaendeleo katika Wilaya yake amesema Wilaya hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na kuiwezesha Wilaya kukusanya shilingi Milioni 488 mwaka jana.
Pesa hizo ni ongezeko la asilimia 38% ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo Wilaya ilikusanya Shilingi Milioni 366.2
Aidha amefahamisha kuwa Wilaya inaendea na miradi mbali mbali ya kuongeza fursa za kujiajiri Vijana ambapo wanatarajia kuazisha Kilimo cha Midimu kukabiliana na tatizo la ajira kwa Vijana.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri amesisitiza Wananchi wa Mkoa wa Kusini kujiepusha na Vitendo vya magendo ambavyo vinalikosesha taifa mapato.
Aidha amebainisha kwamba Kikosi cha Kupambana na Magendo KMKM kiko imara na kitaendelea kumkamata kila atakayejaribu kufanya biashara hiyo haramu.
Rais wa Zanzibar kesho anatarajiwa kuanza ziara yake kisiwani Pemba baada ya kuhitimisha ziara yake katika Wilaya saba za Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.