Habari za Punde

Urasimishaji Ardhi ni Kichocheo cha Maendeleo Endelevu-MKURABITA

Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania ( MKURABITA)  Bi Seraphia Mgembe akionesha hati milki ya kimila ya kumiliki ardhi na kusisitiza umuhimu wa wananchi Wilayani Chamwino mkoani Dodoma kuchukua hati milki hizo  baada ya kurasimisha mashamba yao ili waweze kujiletea maendeleo.
Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini kutoka Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bw. Antony Temu akisisitiza umuhimu wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wananchi waliorasimisha mashamba yao katika kijiji cha Membe Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Afisa Maendeleo ya Jamii  wa Wilaya ya Chamwino Bi Juliana Mtolera akisisitiza jambo wakati wa mafunzo kwa wakulima zaidi ya 100 katika kijiji cha Membe Wilayani humo wakati wa mafunzo yakuwajengea uwezo ili waweze kuzalisha kwa tija, mafunzo hayo yameandaliwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania ( MKURABITA) kwa kushirikiana na Halmshauri ya Wilaya hiyo.
Sehemu ya wakulima zaidi ya 100 wa kijiji cha Membe Wilayani Chamwino wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze kuzalisha kwa tija baada ya kurasimisha mashamba yao.

                                    (Picha  na Frank  Mvungi- MAELEZO)                                                  


Na; Frank Mvungi, Dodoma
Serikali  ya Awamu ya Tano imejikita katika kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA ) kwa kuwawezesha wananchi kurasimisha ardhi wanazomiliki yakiwemo  mashamba na kupatiwa hati za kimila za kumiliki ardhi.

Ni vyema wananchi Wilayanis Chamwino na maeneo mengine ambayo ymeshanufaika na urasimishaji wakatambua kuwa jukumu lao sasa ni kutumia fursa zitokanazo  na urasimishaji kujiletea maendeleo.

Sasa wananchi  wote mlionufaika na urasimishaji tambueni kuwa Serikali imewekeza kwenu kwa kuwajengea uwezo hali inayowawezesha kujikwamua na kujiletea maendeleo ikiwemo kupata mikopo katika Taasisi za fedha kama mabenki kupitia hati za kimila za kumiliki ardhi.

Dhamira hii safi ya Serikali inapaswa kuungwa mkono na wananchi wote ambao wameshanufaika na urasimishaji uwe wa ardhi au biashara, nalisema hili kwa kuwa nimeshudia hivi karibuni Mratibu wa MKURABITA  Bi Seraphia Mgembe akihamasisha wananchi wa Wilaya ya Chamwino na maeneo mengine hapa nchini  kujitokeza kuchukua hati zao ambazo ni ukombozi wa kiuchumi na mwarobaini wa umasikini kwa wananchi wanyonge.

Uhamasishaji huu nimeushuhudia  ukifanyika mara kwa mara na  hata wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wakulima zaidi ya 100 na viongozi 10 wa Kijiji cha Membe, Wilayani Chamwino Bi Mgembe alionekana kuguswa na suala la wananchi kuchelewa kuchukua hati zao za kimila baada kurasimishiwa mashamba yao, akionesha shauku yake ya kutaka kuona wananchi wanajikwamua kiuchumi kupitia hati hizo.

Kutokana na urasimishaji huo ambao umefanyika katika Wilaya ya  Chamwino mkoani Dodoma  jumla ya mashamba 1145 yalipimwa katika Kijiji cha Membe   ambapo hatimiliki 1000 zimeweza kuandaliwa na sehemu kubwa ya hati hizo hazijachukuliwa na wananchi  na kuzitumia katika suala zima la kujenga  uchumi na kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo alizeti.

Dhamira hii njema ya  Serikali inatekelezwa na Ofisi ya Rais-  MKURABITA ambayo imejipambanua kwa vitendo kutokana na kutekeleza  dhana yakujenga uchumi shirikishi au jumuishi unalenga kuwawezesha wananchi kupitia rasilimali zilizopo katika maeneo yao ikiwemo ardhi.

Hati hizo ziwe chachu kwa wananchi kujikwamua kiuchumi na  kuunga mkono nia hii njema ya Serikali  ya kuwaletea  maendeleo; katika hili ni wazi kuwa  wananchi wa Wilaya ya Chamwino wamepata ukombozi wa kiuchumi ambapo sasa wanapaswa kuunga mkono juhudi hizi kwa  kuchukua hati hizi.

Aidha, jambo jingine muhimu ni wananchi wote ambao tayari maeneo yao yamepimwa na kupatiwa hati ni kuongeza bidii katika uzalishaji ili kuendana na dhana ya ujenzi wa viwanda ambavyo vinategemea malighafi kutoka katika sekta ya kilimo.

Aidha,  faida za urasimishaji ni kama ; kuhakikisha usalama wa milki  kwa kuiongezea thamani ardhi husika, Kuweza kujipatia mikopo na kuwawezesha wamiliki kuingia ubia katika uwekezaji kwenye ardhi na kilimo kupitia wadau mbalimbali.

MKURABITA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa dhamira ya Serikali kuwezesha wananchi kiuchumi inatimia kwa wakati kutokana na mkazo inaouweka katika kuwezesha wananchi kurasimisha mashamba yao, viwanja na biashara zao katika maeneo mbalimbali yaliyofikiwa na mpango huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.