Habari za Punde

YANGA YAVUNJA MWIKO WA KUFUNGWA CCM KIRUMBA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara ( TPL) Yanga wameendelea kukaa kileleni mwa msimamo baada ya kuibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Mbao. Mchezo huo wa TPL umechezwa leo Jijini Mwanza ukiwa ni wa ushindani kwa pande mbili Yanga wakitaka waondoe uteja wa kufungwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Mtanange huo ulianza kwa kasi kubwa sana, kila mmoja akicheza kwa umakini mkubwa na kutokutaka kuruhusu goli la mapema. Ilichukua dakik 45, kwa Mbao kuweza kuandika goli la kuongoza kupitia kwa mchezaji wake Ndaki Robert akimalizia krosi ya Amos Charles akiwaacha mabeki wakiuangalia mpira tu.

Mpaka mapumziko Mbao ilienda vyumbani wakiwa wapo mbele kwa goli 1-0, Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mashambulizi langoni mwa Mbao na katika dakika ya 50 Mshambuliaji wa Kimataifa wa Kongo Heritier Makambo anaisawazishia Yanga na ubao kusoma 1-1.

Mpira uliendelea kwa kasi na katika dakika ya 59, beki wa Yanga Kelvin Yondan akiwa nje ya 18 alipiga krosi iliyoishia mkononi mwa beki wa Mbao na mwamuzi kuweka penati.

Mshambuliaji wa Kimataifa  Burundi Amisi Tambwe anaiandikia Yanga goli la pili kwa mkwaju wa penati na kubadilisha matokeo ya ubao na kuwa 2-1.

Mpaka dakika 90 zinamalizika, Yanga wanavunja mwiko wa kutokuifunga Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba wakiwa tayari wamepoteza mechi 2 za Ligi kuu.


Baada ya ushindi huo, Yanga wanatimiza alama 61 wakiendelea kujikita kwenye kilele cha msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara. Yanga inatarajiwa kurejea Jijini Dar es Salaam na kuunganisha safari ya kuelekea Namungo kwa ajili ya mchezo wa FA  dhidi ya Namungo FC.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.