Habari za Punde

Askari usalama wa barabarani washughulikie usalama wa wananchi - Wito

Na Mwashungi Tahir   Maelezo Zanzibar  .
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo Mkoa wa Mjini  ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa  wa Mjini Maghribi Ayoub Mohamed Mahmoud  amewata askari usalama wa barabarani kushughulikia usalama wa wananchi katika matumizi ya bara bara .
Hayo ameyasema leo huko Rahaleo kwenye ukumbi wa Studio wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa wilaya zote  , wawakilishi na wabunge  kuhusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha Julai 2018-Februari 2019 kikao cha Kamati ya Maendeleo.
Amesema suala la matumizi ya barabara haiko salama miundo mbinu yake hairidhishi hata kidogo na inahatarisha usalama wa raia wakiwemo watu wazima ,walemavu, wagonjwa  na hata watoto wadogo.
Pia amesema hali  hatarishi zaidi iko kwa wanaoendesha daladala  kwani wao hawatendei haki abiria kwa kuwa wengi hawawafikishi vituoni mwao, pia wanafunzi wa skuli wanawanyanyasa  kwa kutowachukua  na wakiwachukua maneno ya bughudha hadi wanapofika vituoni mwao.
“Wanaoendesha dala dala ndio chanzo kikubwa cha kuhatarisha usalama wa raia kwa kufanya wanavyotaka ikiwemo kutokuwafanyia haki abiria kwa kuwapeleka wanapotaka kushuka , kuwanyanyasa wanafunzi  na pia boda boda hawafati sheria “, alisema Mwenyekiti huyo.
Hivyo amewaomba askari trafik kuweza kushughulikia masuala haya ili wananchi waepukane na usumbufu wanaoupata  na kuhakikisha usalama wao wa safari unakuwa mzuri kwani Serikali inawajali wananchi wake na ndio  utekelezaji wa ilani wa Chama Cha Mapinduzi kutaka raia wawe salama .
Nae Naibu Waziri wa  Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Mohamed Ahmada Salum amekiri suala hilo lipo na ameahidi kulisimamia na   kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na usalama katika matumizi ya barabara.
Wakitoa michangio Mwakilishi wa Jimbo la Jaango’mbe Ramadhan Abdullah Chande ameiomba Baraza la Manispaa mjini kujenga vyoo katika vituo vya daladala ikiwemo Michenzani ambapo kutaweza kuondosha  uharibifu wa mazingira unaofanywa na wananchi kwa ukosefu wa vyoo kituoni hapo
Pia amesema skuli za maandalizi katika jimbo lake la Jaango’mbe ziko kidogo na kuomba kuzidishwa skuli hizo ili kwa lengo la watoto wote wanaofikia umri wa kusoma wapate fursa hizo.
Akimjibu Mwakilishi huyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Mjini Saidi Juma Ahmada alisema jumla y ash Millioni sabiini na nne laki tano na ishirini  zimetengwa kwa ajili ya kujenga vyoo katika manispaa ya mjini ili kwa lengo la kuweka mji kuwa safi na kupuka uchafuzi wa mazingira.
Sambamba na hayo Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Maendeleo Mkoa wa Mjini Mh Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa maazimio  kuhusu vyoo ameahidi vitashughulikiwa na pia amewaomba baraza la Manispa kuviimarisha na vile vya zamani ili kufanya  mji upendeze na kuwa  kuwa safi na salama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.