Habari za Punde

Balozi Seif afanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Kilimo ya Cuba mjini Havana

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia na kupata maelezo ya utengenezaji wa sigara zinazopendwa zaidi na Watalii na matajiri maarufu {Siga} kwenye maonyesho ya Kilimo Mjini Havana Nchini Cuba.
 Mtaalamu wa Kilimo cha Migomba na vyakula vya Mizizi akimpatia maelezo balozi Seif  taalum inayotumika katika kulima maazo hayo Kisasa zaidi.
Balozi Seif akifurahia na kuridhika na ubora wa bidhaa za Mapapai na Mananasi zilizopo kwenye Maonyesho ya Kilimo Mjini Havana Nchini Cuba.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Tanzania ina kila sababu ya kuimarisha Sekta ya Kilimo kutokana na kubarikiwa kuwa na Rasilmali za kutosha zinazoiwezesha kujikita zaidi katika eneo hilo muhimu kwa Uchumi wa Taifa na Ustawi wa Wananchi wake.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo ya Cuba Mjini Havana mwanzoni mwa Maonyesho ya Siku Nne ya Kimataifa ya Kilimo {FIAGRO - 2019} yanayofanyika kila Mwaka Nchini humo na kuhudhuriwa na wadau wa Sekta hiyo kutoka Mataifa mbali mbali Duniani.
Alisema Sekta ya kilimo inayochukuwa asilimia kubwa ya Watu wake hasa katika Maeneo ya Vijijini inaweza kuwa mkombozi mkubwa wa Ajira hasa kwa kundi kubwa la Vijana wanaomaliza masomo yao.
Balozi Seif  alisema yapo mazao ya asili hasa Muhogo Majimbi, Viazi na mboga mboga yanayoendelea kuzalishwa na Wakulima mbali mbali Nchini Tanzania, lakini kinachokosekana kwa kiasi kikubwa ni ile Taaluma ya kutosha ya kuendeleza uzalishaji wa mazao hayo Kitaalamu zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi huo wa Wizara ya Kilimo wa Cuba kuendelea kuiunga mkono Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwa vile Taifa hilo limeshapiga hatua kubwa Kitaalamu kwa miaka mingi sasa katika kuendeleza Sekta hiyo.
Alisema hatua hiyo muhimu itaweza kusaidia zaidi kuongeza chachu ya uhusiano wa muda mrefu uliyopo baina ya Mataifa hayo mawili yanayoendelea kushirikiana Kidiplomasia tokea yapate  Uhuru na ukombozi wao kutoka katika makucha ya kikoloni.
Akizungumza katika ufunguzi wa Maonyesho hayo Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Bwana Jose Migeil Rodriguez De Armas alisema Cuba imekuwa na Utamaduni wa kuwalika Wadau wa Sekta ya Kilimo kutoka Nchi Rafiki kushiriki Maonyesho hayo.
Alisema Maonyesho hayo huambatana na utolewaji wa Taaluma inayolengwa kupewa wakulima hatua iliyowezesha kuzalishwa Matunda na Mpunga Kitaalamu na kusafirisha nje ya Nchi tokea Mwaka 1933.
Bwana Jose aliwaeleza washiriki wa Maonyeshao hayo wakiwemo Mabalozi wa Nchi rafiki pamoja na wale 26 wa Mataifa ya Bara la Afrika kwamba Cuba imeanza kufungua milango ya uimarishaji wa Seka za Maendeleo ikilenga kujetegemea yenyewe kwa kila nyanja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea mabanda mbali mbali ya maonyesho na kuridhika na hatua kubwa iliyofikiwa na wazalishaji wa mazao tofauti yenye ubora wa kiwango kinachokubalika Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.