STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
19.03.2019
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mratibu Mkuu wa Program ya Kujitolea ya "United Nations Volunteers " (UNV) Bw,Oliver Adam kushoto,alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na Rais leo 19-3-2019.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza azma ya Umoja wa Mataifa (UN) kupitia programu yake ya kujitolea ya Umoja huo (UNV) kwa kuendea kuiunga mkono Zanzibar katika shughuli za maendeleo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati
alipofanya mazungumzo na Mratibu Mkuu wa Programu ya Kujitolea ya Umoja wa
Mataifa (UNV) Oliver Adam, aliyefika Zanzibar kwa lengo la kuimarisha
mashirikiano baina ya pande mbili hizo.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alimueleza Mratibu huyo kuwa (UNV) ni programu muhimu iliyo
chini ya Umoja wa Mataifa ambayo ina umuhimu mkubwa katika kuendeleza shughuli
mbali mbali za maendeleo hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa progmu
hiyo ya Umoja wa Mataifa imeanza miaka mingi na kuwez kusaidia kwa kiasi kikubwa katika
kuendeleza na kuunga mkono juhudi za serikali katika shughuli za maendeleo
ikiwemo sekta ya afya, kilimo na sekta nyenginezo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alimueleza Mkuu huyo kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Kituo
cha Ujasiriamali ambacho kinatoa mafunzo kwa vijana ya kazi za aina mbali mbali
za ujasiriamali ambapo kuna haja ya kukiongezea uwezo pamoja na kuwapatia mtaji
vijana hao ili wanaufaike na elimu wanayoipata.
Pia, alisisitiza kuwa
kuna haja ya kuweka mikakati maalum ya kuwajengea uwezo vijana wote wa Unguja
na Pemba ili waweze kujiajiri wenyewe kwa kuwapa mikopo midogo midogo
itakayowasaidia kujiendeleza na hatimae kujiajiri.
Pia, Rais Dk. Shein
alisisitiza haja ya Programu hiyo ya (UNV) kuunga mkono katika kuongeza nguvu
kwa kupata walimu wa masomo ya Sayansi kwa skuli za Sekondari za Zanzibar ambao
bado wanahitajika kwa kiasi kikubwa.
Alieleza kuwa licha ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka mikakati maalum na kuyapa kipaumbele
masomo ya Sayansi kwa kuwashajiisha wanafunzi kuyasoma kwa bidii na hatimae kujiendeleza
katika vyuo vyake vitatu vikuu vilivyopo hapa nchini.
Aliongeza kuwa lengo
la kufanya hivyo ni kuwapata walimu na wataalamu wa masomo ya Sayansi ili
kuondokana na upungufu uliopo ambapo tayari hata hivyo zipo nchi zinazosaidia
kwa kuleta walimu wa masomo ya Sayansi ikiwemo Nigeria.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza uhaba wa madaktari wa upasuaji ambao bado wanahitajika
katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini licha ya juhudi zinazochukuliwa na
Serikali za kuwasomesha wataalamu wa kada hiyo.
Rais Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa Umoja wa Mataifa (UN) kwa kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na
kuitumia programu ya kujitolea ya UN kwa kuiunga mkono Zanzibar .
Nae Mratibu Mkuu wa
Programu ya Kujitolea ya Umoja wa Mataifa (UNV) Oliver Adam alimueleza Rais Dk.
Shein azma ya Progmau hiyo katika kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza
shughuli mbali mbali za maendeleo.
Mratibu Mkuu huyo alimuhakikishia
Dk. Shein pamoja na kuihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa (UNV) iko
tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha shughuli zote za kujitolea zinazosimamiwa
na Umoja wa Mataifa (UN) na Zanzibar nayo itafaidika.
Aidha, Mratibu Mkuu huyo
alieleza azma ya (UNV) ya kusaidia kuendeleza miradi kadhaa hapa Zanzibar
sambamba na kuzifanyia kazi hoja za Rais Dk. Shein za kuwawezesha vijana,
kuimarisha sekta ya afya kwa kuongeza uwezo kwa madaktari wapasuaji pamoja na
walimu wa masomo ya sayansi na nyenginezo.
Mratibu Mkuu huyo, alimueleza
Dk. Shein kuwa (UNV) ina uzoefu na umahiri mkubwa katika suala zima la shughuli
za kujitolea zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa kupitia programu hiyo, hivyo
itautumia kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar.
Programu ya kujitolea
ya Umoja wa Mataifa (UNV) imekusudia
kusadia kufanikisha mikakati mbali mbali inayoendeshwa na Serikali ili
kuimarisha hali ya kujitolea nchini kwa manufaa ya taifa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment