Habari za Punde

Balozi Seif atembelea Shamba la Kimataifa la Ufugaji Kuku wa Nyama na Mayai la Al Rawdah , Dubai

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyeji wake  kati kati Mwenyekiti wa Shamba la Kimataifa la Ufugaji Kuku wa  Nyama na Mayai la Al Rawda Sheikh Abdullah Sultani nje ya Jengo la Ofisi ya Shamba hilo nje ya vitongoji vya Mji wa Dubai.
Wa kwanza kutoka Kulia ni Afisa wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  Muungano wa Falme za Kiarabu Bwana Mwadini.
 Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Uongozi wa Shamba la Kimataifa la Ufugaji Kuku wa  Nyama na Mayai la Al Rawda kwenye  Jengo la Ofisi ya Shamba hilo nje ya vitongoji vya Mji wa Dubai.
Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Shamba la Kimataifa la Ufugaji Kuku wa  Nyama na Mayai la Al Rawda Sheikh Abdullah Sultani.
 Meneja uzalishaji wa Miradi ya Shamba la Kuku la Al Rawdha Mhandisi Ali Idris Osman akimpatia maelezo balozi Seif ndani ya Kiwanda cha kusindika bidhaa za Nyama ya Kuku.
 Mhandisi Ali Idris Osman akimuonyesha Balozi Seif baadhi ya Nyama za Kuku zilivyohifadhiwa katika mfumo wa pipi maarufu {Sousarge} kwenye Kiwanda cha kuzindika nyama za Kuku.
Balozi Seif akiangalia baadhi ya bidhaa zinazotokana na mali ghali ya nyama ya Kuku zilizokwishawekwa kwenye vifurushi Maalum tayari kwa kuingia sokoni.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis , OMPR Dubai
Uongozi wa Shamba la Kimataifa la Ufugaji Kuku wa  Nyama na Mayai la Al Rawda liliopo pembezoni kidogo mwa Mji wa Dubai katika Muungano wa Falme za Kiarabu limeonyesho nia ya kutaka kuwekeza miradi yao Zanzibar katika azma ya kudumisha uhusiano kati ya Zanzibar na Muungano huo.
Mwenyekiti Mtendaji wa Shamba hilo Sheikh Abdullah Sultani alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika na Ujumbe wake kulizuru shamba hilo ili kuangalia hali ya uzalishaji pamoja na kujifunza mambo mbali mbali katika Mradi huo mkubwa.
Sheikh Abdulla Sultani alisema Uongozi wa Shamba hilo umeridhika na hali halisi ya mazingira ya Visiwa vya Zanzibar wakati wa ziara yake mwaka uliopita iliyomshawishi na kumvutia kutaka kufunguwa tawi la Shamba la Mradi huo ili liweze kutoa huduma zinazozalishwa kutokana na kuku katika Kanda ya Afrika Mashariki.
Alisema Shamba hilo hivi sasa lina uwezo wa kutosha wa kuzalisha Kuku wa Mayari na Nyama na kusambaza ndani ya Mataifa yaliyomo katika Muungano wa falme za Kiarabu na mikakati yake kwa sasa ni kuelekea katika uzalishaji unaokusudiwa kulenga Mataifa mengine Duniani.
“ Zanzibar ni mahali ambapo tumevutiwa napo katika masuala ya uwekezaji wa miradi yetu ya Kuku wa Mayai na Nyama ambao kwa sasa unafikia zaidi ya Kuku Milioni Moja”. Alisisitiza Sheikh Abdullah.
Sheikh Abdullah alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi huo unaweza kuanzisha Tawi lao la Ufugaji wa Kuku Visiwani Zanzibar kama wanaweza kupata eneo la ardhi linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa Kilomita Mbili kwa hatua za awali.
Mwenyekiti huyo Mtendaji wa Shamba  la Kimataifa la Ufugaji Kuku wa  Nyama na Mayai la Al Rawda alisema Mradi huo ulioasisiwa zaidi ya Miaka 27 iliyopita hivi sasa umeshaajiri Wafanyakazi wasiopungua 60,000 idadi ambayo ni kubwa katika soko la Ajira.
Alisema Mradi huo kwa sasa umekuwa ukihudumia nyama, Mayai na vifaranga vya Kuku kwa Watu wapatao Milioni 11,000,000, kutoa Mafunzo kwa Wafugaji wa Kuku sambamba na kutembelewa na Watu zaidi ya 10,000 kwa Mwaka wanaokwenda kujifunza mbinu za ufugaji Kuku wa Kiasa.
Akitoa shukrani zake kwa Uongozi wa Shamba hilo la Kuku la Al Rawdha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Tanzania bado inahitaji kuwa na Soko la uhakika linalotokana na bidhaa zinazozalishwa na Kuku kufuatia muingiliano mkubwa wa Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Balozi Seif alisema zipo Taasisi, Jumuiya na hata Wananchi wanaojishughulisha na Miradi inayotokana na Ufugaji wa Kuku Nchini Tanzania lakini bado hazijaweza kukidhi mahitaji halisi ya walaji akitolea mfano Zanzibar wakati mwengine huagiza Nyama na Vifaranga vya Kuku kutoka Nchini Brazili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Uongozi wa Shamba hilo la Kuku la Al Rawdha kwamba Serikali zote mbili Nchini Tanzania zimekuwa zikitoa msukumo katika uimarishaji wa Mifugo ya kuku kupitia Sekta ya Kilimo na Ufugaji kwa vile hutoa ajira nyingi kwa Wananchi walio wengi.
Alisema bidhaa zinazozalishwa kutokana na Kuku kama mayai na nyama mbali ya kupendwa na Watu wengi kutokana na gharama zake lakini pia zina ladha tamu inayovutia kuliwa kwa wakati wote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ujumbe wake alipata fursa ya kutembelea shamba hilo na kujionea hali halisi ya ufugaji wa Kuku unaotumia mfumo wa Teknolojia ya kisasa.
Meneja uzalishaji wa Miradi ya Shamba hilo Mhandisi Ali Idris Osman alimueleza Balozi Seif na Ujumbe wake kwamba ufugaji huo unazingatia zaidi hali ya usafi ili kujiepusha na maradhi yanayoweza kuathiri mifugo hiyo kwa haraka.
Mhandisi Ali Idris alisema mradi huo umelazimika kutengwa mbali na makaazi ya Watu ili uwe salama, sambamba na kuepuka uchafuzi wa mazingira unaoweza kusababisha magonjwa.
Alisema shamba hilo lenye mabanda saba marefu kwa ajili ya Kuku wa Nyama na mengine saba marefu kwa kuku wa Mayai lina ukubwa wa Hekta Mia Tano za mraba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kurejea Zanzibar Jumatatu ya kesho Mchana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.