Habari za Punde

Kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Yapania Kurudisha Hadhi ya Chuo Cha Mweka

Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii wakipewa maelezo kutoka kwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Hashimu Paschal kuhusiana na matumizi ya silaha za moto aina ya AK-47 i wanapofanya doria wakiwa Hifadhini wakati wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge walipotembelea chuo hicho mjini Moshi. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Shabani Shekilindi (wa pili kulia) akiwa na Wajumbe wa Kamati  hiyo wakipewa maelezo huku wakiangalia baadhi ya taswira  za wanyamapori mbalimbali wanaotumika kwa ajili ya kuwafundishia  wananfunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro wakati kamati hiyo ilipofanya ziara Chuoni hapo.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii wakipewa maelezo kutoka kwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Judith Mwela  kuhusiana na handaki lililotengenezwa na kabila la Wachaga mnamo  karne ya 18  kwa ajili ya kujihami dhidi ya maadui kabla ya Wajumbe hao kuingia ndani ya Handaki hilo  kwa ajili ya kujionea  , Handaki hilo lipo katika Chuo hicho
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Shabani Shekilindi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na  Wajumbe wa Kamati  hiyo pamoja na watumishi wakati kamati hiyo ilipofanya ziara katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Shabani Shekilindi akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu  akiwasalimia  na baadhi ya Watumishi  wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara Chuoni hapo.
Baadhi ya magari maalum yAnayotumiwa na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakati wanapofanya  mafunzo kwa vitendo katika Hifadhi nchini.
 (Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)

Wizara ya Maliasili na Utalii imesema imeanza  kuzifanyia kazi baadhi ya  changamoto zinazokikabili  Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka ili kiendeleze hadhi yake ya  kuwa Chuo cha Kimataifa.

Hatua hiyo  inakuja kufuatia kupungua kwa idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaojiunga na Chuo hicho  kila mwaka.

Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyotembelea Chuo hicho mkoani  Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amesema shabaha ya Wizara  ni kukiona  chuo  hicho  kikiendelea kuwa na hadhi ya Kimataifa.

Amewaeleza Wajumbe hao kuwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Wizara kuendelea kufanya  mazungumzo na vyombo vya udhibiti na Usimamizi wa Elimu hapa nchini ( TCU na NACTE) ili viangalie namna ya kuondoa masharti magumu yanayosababisha baadhi ya masomo yanayotolewa na nchi nyingine yasitambuliwe chuoni hapo.

Mhe.Kanyasu ameiambia kamati hiyo kuwa sababu nyingine  ya idadi ya Wanafunzi  wa kigeni kupungua ni  baadhi  nchi kama  Malawi  na Kenya kuanzisha vyuo vyao tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

 Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Shabani Shekilindi  amesema Chuo hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za uhaba wa wahadhiri pamoja na uchakavu wa miundombinu.

Amesema kupitia Kamati anayoiongoza atahakikisha kuwa changamoto zote zinapatiwa majibu ili chuo hicho kiendelee kutoa huduma bora.

 Amekishauri chuo hicho kiendelee kuzitangaza kozi zake ndani na nje ya nchi.

Naye Mjumbe wa Kamati  hiyo Mhe. Boniphace Getere amekishauri chuo hicho kiingie mkataba na watu binafsi kwa ajili kujenga mabweni yatayokayosaidia kutatua changamoto ya wanafunzi 228 kati ya 600 wanaolazimika kupanga nyumba nje ya Chuo hicho.

Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori , Mweka kilianzishwa mwaka 1963 kikiwa na wanafunzi 25 kutoka Kenya, Uganda Malawi , Cameroun na Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.