Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Asaini Kitabu Cha Maombolezi Kufuatia Vifo Vya Wananchi wa Msumbiji.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitia saini Kitabu cha Maombolozo kwenye Ubalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Msumbiji uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar kufuatia maafa yaliyotokea Nchini Msumbiji yaliyotokana na kimbunga kikali kilichosababisha Mafuriko.Kulia ya Balozi Seif aliyesimama ni Balozi Mdogo wa Msumbiji aliyepo Zanzibar Bwana Jorge Augusto Menezez.
Balozi Mdogo wa Msumbiji aliyepo Zanzibar Bwana Jorge Augusto Menezez Kushoto akimsindikiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif baada ya kuweka saini Kitabu cha Maombolezo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema maafa yaliyowakumba Wananchi wa Msumbiji baada ya kukumbwa na  kimbuka kikali kilichotokea Nchini humo Wiki iliyopita yamewagusa pia Watanzania walio wengi kufuatia uhusiano wa ujirani mwema uliopo kati ya Nchi hizo mbili.
Alisema ameshtushwa na tukio hilo lililoleta huzuni na simanzi kubwa kwa Familia kadhaa ya Wana Msumbiji waliopoteza roho zao kupitia vyombo vya Habari mbali mbali Duniani wakati akiwa safarini nje ya Nchi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo alipofika Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Msumbiji iliyopo Mtaa wa Kikwajuni Mjini Zanzibar kutia saini Kitabu cha Maombolezo kufuatia vifo vya Wananchi wa Msumbiji zaidi ya 500 vilivyotokana na Maafa yaliyosababishwa na Kimbunga hicho.
Alisema maafa hayo yaliyozigusa pia Nchi za Malawi na Zimbabwe yameleta hali ya kusikitisha iliyowaacha Wananchi wengi wa Msumbiji hasa wale walioko kwenye Mji wa Beira katika mazingita hatarishi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Balozi Mdogo wa Msumbiji aliyepo Zanzibar alizitaka Familia za Wananchi waliopatwa na misiba Nchini Msumbiji kuwa na moyo wa subira katika kipindi hichi kigumu cha maafa na maombolezo.
Akitoa shukrani zake Balozi Mdogo wa Msumbiji aliyepo Zanzibar Bwana Jorge Augusto Menezez ameendelea kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua yake ya mara moja iliyochukuwa katika kuipatia msaada wa dharura wa Kibinaadamu Nchi yake.
Balozi Jorge alisema Serikali ya Msumbiji kwa sasa iko katika harakati za awali za kurejesha miundombinu iliyoharibika kutokana na kimbunga hicho huku ikikaribisha kupokea misaada mbali mbali kutoka kwa washirika wao itakayotoa afueni kwa Jamii za Watu walioathirika kutokana na Maafa hayo.
Alisema katika kipindi hichi cha mpito jitihada zinaendelea kuchukuliwa katika kujiweka tayari kukabiliana na miripuko ya maradhi ya kuambukiza iwapo yatachomoza ambayo mara nyingi huibuka wakati yanapotokea maafa kama hayo.
Balozi Jorge alifahamisha kwamba idadi ya vifo vilivyoripotiwa kwa sasa inaeleza kufikia zaidi ya Watu Mia 500 ambayo Takwimu halisi kutokana na zilizaha hiyo inakisiwa kufikia zaidi ya Watu 1,000.
Alisema Mji wa Beira umeteketea kutokana na Kimbunga hicho kilichowaacha Watu zaidi ya Milioni Moja kukosa Makaazi baada ya Nyumba zao kukumbwa kabisa na Mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga hicho.
Balozi Jorge alieleza kwamba idadi ya Majengo ya Skuli yaliyoathirika kwa sasa yanakadiriwa kufikia Elfu 3,000, Wanafunzi Elfu 4,000 hivi sasa wamekosa Majengo ya kusomea, Hospitali 45 zimebomoka na Mashamba ya Kilimo yapatao Laki 450,000 yameharibika kabisa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.