Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Azungumza na Uongozi wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Ikulu leo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wake na Uongozi wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar uliuofanyika leo Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza haja ya Kamisheni ya Utalii kutoa elimu ya historia ya Utalii hapa Zanzibar ili kuujua unakotoka na unakokwenda na hatua zilizofikiwa hivi sasa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar. 

Dk. Shein aliyasema hayo leo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, na Mambo ya Kale uliofuatana pamoja na uongozi wa Kamisheni ya Utalii na Makamishna wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, katika kikao kilichofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali walihudhuria.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuijua historia ya utalii hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kujua na kufahamu lengo lililokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuelewa jinsi utalii ulivyokuwa hapo siku za nyuma na jinsi uliyo hivi sasa sambamba na hatua na mafanikio yaliofikiwa kutokana na sekta hiyo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa sekta ya utalii imekuja baada ya zao la karafuu kushuka thamani yake na ndipo marehemu mzee Aboud Jumbe Mwinyi akaona haja ya kuiimarisha sekta hiyo pamoja na baadhi ya mazao mengine ya viungo.

Alieleza kuwa tokea kipindi hicho sekta ya utalii imeweza kuimarika kwa kiasi kikubwa kwa kuwepo vivutio kadhaa hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar inajitangaza wenyewe kutokana na vivutio vilivyopo hapa nchini.

Aliongeza kuwa hivi sasa Zanzibar iko vizuri kiutalii ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo siku za nyuma kwani utalii wa Zanzibar unasifika zaidi duniani kote na kuwapelekea watalii wengi kuja kuitembelea Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa hivi sasa utalii wa Zanzibar unaongozwa na Sheria ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2012 kwa lengo la kuufanya utalii uwe kwa wote kwani ndio uchumi wa Zanzibar.

Alieleza kuwa Sheria ndio ngao kubwa ya kuendesha Kamisheni ya Utalii hivyo alisisitiza haja kwa Kamisheni pamoja na Makamishna wote kuizingatia na kuifanyia kazi Sheria hiyo pamoja na kanuni zake ili iweze kuwasaidia kuendeleza sekta hiyo.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza maamuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa sekta zote zinabebwa na sekta ya utalii pamoja na kuonesha umakini wake katika sekta hiyo na kuipa dhamana Kamisheni hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Waziri, Wizara, Bodi, Kamisheni na Makamishna wake kwa lengo la kuiimarisha sekta ya utalii ambayo ndio ukombozi wa uchumi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza matumaini yake kuwa mazungumzo ya kikao hicho yataongeza kasi mpya na ari mpya katika kuiimarisha sekta ya utalii.

Nae Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alisema kuwa sekta ya Utalii ni sekta muhimu katika kuimatisha uchumi wa Zanzibar na kukuza pato la Taifa, hivyo kuna haja ya sekta hiyo kuengwaengwa.

Aidha, Balozi Seif alieleza haja ya kujifunza katika kuiendeleza sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ina vivutio vingi pamoja na historia katika mambo ya utalii ikilinganishwa na visiwa vyengine vikiwemo vile vilivyopo katika Bahari ya Hindi  ambavyo vimejitangaza vyema na kuweza kupokea wageni wengi.

Nae Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo pamoja na uongozi wa Wizara hiyo ulieleza jinsi Zanzibar ilivyopata mafanikio katika sekta ya utalii na jinsi wawekezaji na wageni wanaokuja kuekeza na kuitembelea Zanzibar.

Nao Makamishna wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar walitoa pongezi kwa Rais Dk Shein kwa jinsi alivyodhamiria kuiimarisha na kuiendeleza sekta ya utalii ambayo imepiga hatua kubwa iliyopelekea kuongezeka kwa watalii na kuvuka lengo lililowekwa.

Sambamba na hayo, Makamishna hao walieleza kuwa hatua hizo za Dk. Shein ni miongoni mwa juhudi zake alizozichukua na mafanikio aliyoyapata katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Pia, walieleza mikakati waliyoiweka katika kuhakikisha idadi ya watalii inakwenda sambamba na mapato yanayopatikana kutoka katika sekta hiyo ya utalii.
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822  
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.