Habari za Punde

Mahakama watakiwa kutoa ushirikiano kwa taasisi muhimu ili kesi zikamilike kwa wakati



RAYA HAMAD –WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Watendaji wa Mahakama wametakiwa kutoa mashirikiano na taasisi ambazo zipo nje ya Mahakama ikiwemo  Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka , Jeshi la Polisi ili ufatiliaji na muendelezo wa kesi ziweze kukamilika kwa wakati

Iwapo hakutakuwa na mashirikiano ni wazi kuwa mianya ya Rushwa na ukiukwaji wa maadili hautakuwepo jambo ambalo haliwezi kuleta ufanisi na hivyo kupelekea malalamiko ya wananchi ambao wanahitaji huduma za mahakama hasa katika kupata ufumbuzi wa kesi zao

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Khamis Juma Mwalim ameyasema hayo alipokutana na watendaji wakuu Mahakama wakiwemo Majaji na  Mahakimu pamoja na Makadhi wa Mikoa miwili ya Pemba ambapo amewataka watendaji hao kutambua na kuelewa kuwa rushwa ni adui anaeuwa na kuhujumu uchumi wanchi hivyo hawapaswi kuikaribia   iwe kutoa ama kupokea

Amewataka Majaji kuongeza kasi  na uwezo wa kusikiliza kesi na kutoa maamuzi sahihi kwa haraka na wakati  pasina kuingizwa sitofahamu ama kuingiza masuala yasiyoendana na  maadili ya kazi na kutolea mfano wa kesi za Ubakaji na udhalilishaji kuhakikisha wanatoa adhabu kwa mujibu wa taratibu za sheria zilizopo ili yeyote mwenye tabia hii chafu aogope na asitamani kufanya kosa la udhalilishaji na kusisitiza kuwa wadhalilishaji  ni watu makatili wasio na huruma hivyo hawastahilki kuonewa huruma

Waziri Khamis  pia amewakumbusha Watendaji hao kuwa uwepo wa Taasisi ya Mahakama ni utekelezeji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi hivyo ni vyema kuitumikia wananchi kuitekeleza kwa vitendo kwa maslahi na maendeleo ya nchi
Ameahidi kuendelea kushughulikia suala la uhaba wa nafasi pamoja stahiki zao  ambapo taayari  Serikali kuu inatambua tatizo hilo pamoja na kuwataka Watendaji kutoridhika na kiwango cha elimu walichonacho pamoja na kutoa elimu kwa jamii kutokwepa  kutoa ushahidi ili Kesi ili waweze kuisaidia mahakama 

Katibu Mkuu wa Wizara hio ndugu George Kazi amesema jukumu la usimamizi wa Katiba na Sheria ndilo walilokabidhiwa ambapo ndani yake zinapatikana taasisi za Mwanasheria Mkuu,  Mahakama, Ofisi ya  Mkurugenzi wa Mashtaka, Ofisi ya Mufti na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana  hivyo itakuwa si sahihi kuona taasisi hizi zinakiuka maadili

Sheria ya usimamizi wa Mahakama inatakiwa ifuatwe sheria ambayo imegawanya majukumu ya kiutendaji na kiutawala ili masuala ya Mahakama yasiingiliane yatekelezwe  na mujibu wa taratibu   hivyo sheria inapofuatwa hakutakuwa na mrundikano wa kesi na ndio maana Wizara baada kuona umuhimu ilitoa vitabu vingi kwa kila hakimu ili vifanyiwe kazi na kuelewa wajibu wao

Aidha aliwasisitiza viongozi wa Mahakama kushirikiana na Wizara  ili Waziri aweze kusimamia vyema na kufahamu masuala yote ya muhimu kwa maslahi na maendeleo ya wizara  hasa suala la uwekaji wa takwimu sahihi ambazo zitasaidia kuwepo kwa uhalisia sio wa kupikwa na utaratibu mzuri ili kuwa na kumbukumbu nzuri za kiutendaji “ Waziri ndie anaekwenda kujibu masuala katika chombo cha kutunga sheria tuwe karibu nae na kufikisha taarifa kwa wakati tusisubiri mpaka tuhimizwe bali tufahamu wajibu wetu ”
Nae Mtendaji Mkuu wa Mahakama ndugu Kai Bashiru amesema Wizara inafahamu kuwa Mahakama inakabiliwa na baadhi ya changamoto lakini  mashirikiano ya Wizara na watendaji  yataweza kutatua changamoto hizo kiufanisi
 Katika utekelezaji wa sheria ya Utawala  wa Mahakama Idara imejipanga kutekeleza na kusimamia muundo wa watendaji , majukumu ya wafanyakazi, kufanya tathmini kwa watendaji ili kuleta ufanisi  hatua ambayo itawezesha pia kuwapima watendaji utendaji wao wa kazi kuanzia Majaji na Mahakimu ili kufahamu wapi kesi zimekwama na kwanini ikiwemo kupata takwimu sahihi ya kesi zinazohukumiwa  pamoja na kusisitiza ufinyu wa  bajeti inakuwa ni kikwazo lakini watahakikisha wanayapa kipaumbele kwa kuyasimamia vyema maslahi ya wafanyakazi wote ili kujenga ari ya kutendaji

Akitoa taarifa fupi Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu na Mrajis wa Jimbo Mahakama Kuu Pemba  Mhe Abdulkadir Ali amesema Pemba ina jumla ya wafanyakazi 120 wanawake 41 na wanaume 79 idadi ambayo inajumuisha kada ya Mahakimu na Makadhi

Katika kila kituo cha  kuna Mahakama ya Kadhi zinazoshughulikia masuali ya Kiislam kama ilivyoongoza sheria ya Mahakama ya Kadhi sheria No. 9 ya mwaka 2017
Malengo makuu ya Mahakama ni kusikiliza  mashauri na kuyatolea maamuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na sheria ambapo Mahakama ya Pemba inajumuisha vituo vikuu vitano ikiwemo Mahakama kuu Chake chake , Mahakama ya Wilaya Mkoani, Mahakama ya Mwanzo Kengeja,  Mahakama ya Mkoa Wete na Mahakama ya Wilaya Konde

Mkurugenzi wa Wizara hio ndugu Juma Ali Simai amesisitiza suala la nidhamu heshima na uwajibikaji na kusema kuwa linamhusu kila mfanyakazi kufanya hivyo kutasaidia kuondosha mapungufu nakasoro ziliopo katika ngazi zote na hivyo kutoa huduma bila ya upendeleo .

Akitoa shukurani kwa niaba Taasi ya Mahakama Pemba Hakimu wa Mkoa Kusini Pemba Mhe Luciano Makoye Nyengo kuhusu mrundikano wa baadhi ya kesi amesema  sheria ipo wazi na kutolea mfano iwapo kesi miezi mine haijasikilizwa kisheria ifutwe ingawa jamii hawezi kuelewa na hapo ndipo panapotokea sitafahamu kwa jamii

Pia ameziomba taasisi ambazo wanafanya nao kazi kwa karibu kujitahidi kusimamia na kufatilia kutatua baadhi ya mkigogoro ya kesi kabla kufikisha  mahakamani kwani sio lazima kila kesi hufikishwa mahakamani zipo kesi ambazo kuna taratibu zikifutwa zinawezwa kumalizwa kwa ngazi ya chini badala kuzifikisha mahakani na kusababisha kuwepo kwa mlolongo wa kesi .

Luciano ameiomba Wizara kuandaa makaazi maalum ya Mahakimu na Majaji  wa Mahakama ili wawe huru na kazi zao kwa vile  kulingana na mazingira yao ya kazi si rafiki  sehemu wanazoishi za uraiani ni tatizo kesi wanaziamua ni nzito hivyo wanahitaji  kuishi maeneo salama zaidi










No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.