Habari za Punde

Madiwani wa na Masheha Wilaya ya Magharibi Wapata Elimu

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akizungumza na Madiwani na Masheha wa Wilaya ya Magharibi “B” hapo katika Ukumbi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi B  Mombasa.
Kulia ya Nd. Shaaban ni Naibu Meya wa Manispaa ya Magharibi “B” Mh. Asha Hassan Juma na Kushoto ya Nd. Shaaban ni Mratibu wa shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ishaq Kundi Vuai.
Katibu Mkuu Shaaban akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi hao wa Wadi na Shehia zilizomo Wilaya ya Magharibi “B”.
Baadhi ya Madiwani na Masheha wa Baraza la Manispaa la Wilaya ya Magharibi “B”.
Diwani wa Kuteuliwa Thuwaiba Jeny Pandu akichangia kwenye Kikao cha Madiwani na Masheha wa Wilaya ya Maghari “B”.

Viongozi wa Shehia na Madiwani kutoka Wilaya ya Magharibi “B” wametakiwa kufanya kazi kwa kujiamini sambamba na kuachana na tabia ya mughali ili kuepusha athari za maafa  zinazoweza kutokea katika jamii.
Kufanya hivyo ni hatua muhimu ya kuisaidia serikali kuu kuepusha kubeba gharama zisizo kuwa za lazima na badala yake kuweka mkazo zaidi katika miradi ya maendeleo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif Mohamed alieleza hayo wakati akizungumza na masheha pamoja na madiwani wa wilaya ya magharibi “B” katika kikao maalum kilichofanyika kwenye ukumbi wa Baraza la Manispaa Magharibi “B” uliopo Kwa Mchina.
Katibu Shaaban aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia dhamana zao kupitia maeneo yao kwa kuwatambua wageni wanaoingia na kutoka kwa lengo la kudhibiti maafa yanayoweza kuepukika.
Alisema kumekuwa na tabia isioridhisha ya baadhi ya Watu kuvamia na kujenga maeneo yasioruhusiwa hasa yale ya mabondeni jambo linalopelekea kutokea kwa maafa ya kupotea kwa mali na maisha ya watu kila inapofika kipindi cha mvua kubwa.
Akigusia suala la uchimbaji wa vyoo Katibu Mkuu alisema ni jambo la aibu katika wilaya ya magharibi “B” kuzikuta baadhi ya nyumba hazina vyoo hasa wakati huu ambao Serikali ipo katika mkakati wa kutokomeza maradhi ya mripuko yanayoweza kuathiri afya za wananchi hasa kipindi kilichopita
.”Niseme  tu Masheha bado mna jukumu la kuhakikisha mnazikagua nyumba zote na kuziorodhesha zile ambazo hazina vyoo”. Alisema Katibu Mkuu Shaaban.
Nae Naibu Meya wa Baraza la Manispaa magharibi “B” Mhe. Asha Hassan  Juma aliwaeleza viongozi hao katika kipindi hichi ambacho wananchi wamepatwa na maafa katika shehia zao wana wajibu wa kurikodi  idadi  kamili kwa kila mwananchi aliepatwa na maafa ili  serikali kuwa na Takwimu sahihi.
Kwa upande wake  Diwani wa kuteuliwa Mhe.Thuwaiba Jeni Pandu alisema  ipo  changamoto juu ya suala la udhibiti wa taka mitaani kutokana na kuchelewa kutiwa saini kwa sheria  ndogo ndogo  zitakazotumika  kuwadhibiti wananchi kutupa taka kiholela .
Alieleza kuwa wilaya ya Magharibi “B” bado lipo tatizo la uharibifu wa mazingira kutoka na baadhi ya wananchi kuendelea kuwa na mifugo kama vile Ngo’mbe akitolea mfano eneo la Fuoni Angaza lililoathiriwa na Ufugaji huo.
Nao masheha walioshiriki katika kikao hicho wameiomba  Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia usafiri katika kila shehia ili ziweze kubebwa taka kwa ajili ya kuzitupa katika jaa kuu liliyopo Kibele.
Wamesema upo muamko mkubwa kwa vijana waliojitokeza kukusanya taka katika shehia zao lakini wanakabiliwa na Changamoto ya Usafiri pamoja kipato duni ukilinganisha na kazi wanazozifanya vijana hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.