RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, aliipongeza Wizara hiyo kwa
mafanikio yaliopatikana pamoja na kupongeza hatua zilizochukuliwa hadi kufikia
Kampuni ya DSTV kurusha matangazo ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC)
moja kwa moja.
Hayo aliyasema leo, katika ukumbi wa Ikulu ndogo
Kibweni mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii na
Mambo ya Kale wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa
Wizara hiyo kwa Kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019.
Rais Dk. Shein aliwakumbusha viongozi na watendaji
wa Wizara hiyo umuhimu wa kukumbuka historia ya kuwepo kwa Chanel ya ZBC2,
hivyo akawataka kuitumia vyema fursa iliopo ili Televisheni hiyo iendelee
kuonekana katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi.
Aidha, alielezea azma ya Serikali ya kujenga jengo
kwa ajili ya kuhifadhia mitambo ya kuchapia madaftari, kwa kigezo kuwa kiwanda
cha uchapaji ni muhimu katika kuliingizia Taifa mapato sambamba na kuimarisha
sekta ya elimu hapa nchini.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza haja ya
kuufufuwa mchezo wa Golf hapa nchini kwa lengo la kushajiisha uimarishaji wa
sekta ya Utalii, sambamba na kushirikiana na taasisi binafsi ikiwemo Hoteli ya
Sea Cliff katika kufanikisha dhamira hiyo.
Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuzisaidia na
kuziunga mkono na kuzisimamia taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo bila ya
upendeleleo huku akisisitiza haja ya uongozi wa Wizara hiyo kuendelea
kuwahimiza watendaji wake kufanya kazi kwa ufanisi kwa lengo la kupata tija na
mafanikio bora zaidi.
Mapema Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Idd, alitumia fursa hiyo kuipongeza Wizara hiyo na kuieleza jinsi alivyofanya ziara za
kutembelea taasisi za Serikali za habari na kukutana na kufanya mazungumzo na
watendaji wake.
Balozi Seif alisisitiza haja kwa taasisi za habari
ambazo zinamadai kwa taasisi nyengine kuendeleza mikakati yao ya kufuatilia
madai yao ili fedha zitakazopatikana ziendelee kusaidia na kuleta tija kwa
Serikali na kufikia azma iliyokusudiwa.
Alieleza umhimu wa Shirika la Utangazaji la
Zanzibar (ZBC), kuifanya redio yake ya ZBC kuzidi kusikika ndani na nje ya
Zanzibar.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza haja kwa uongozi wa Wizara hiyo
kujua azma ya Serikali ya kuiweka Wizara hiyo kuwa na sekta ya habari, utalii
na mambo ya kale ambapo utegemezi wa sekta hizo ni muhimu katika mashirikiano
ya pamoja hasa katika kujitangaza.
Alisisitiza haja ya kukaa na kufanya kazi kwa
pamoja kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii.
Nae Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud
Thabit Kombo alieleza kuwa Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili
na Utalii imefanikiwa kuandaa tamasha la Urithi wa Utamaduni wa Mtanzania
(Urithi Vestival).
Alieleza kuwa wizara imepokea vifaa vya kisasa vya
kazi za Digitali na kuhuisha nyaraka zilizochakaa kutoka kwa Washirika wa
Maendeleo wa Serikali ya Oman vyenye thamani ya zaidi ya TZS 89,204,100 ambavyo
ni kwa ajili ya kuhuisha na kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka kwa matumizi ya
sasa na baadae.
Aidha, Waziri Kombo alieleza kuwa Wizara hiyo
imeandaa kwa mara ya kwanza kwa kushirikiana na sekta binafsi Tamasha la Utalii
la Zanzibar ambalo lilifunguliwa rasmi na Rais Dk. Shein Novemba 17 mwaka jana
2018 katika hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.
Sambamba na hayo, Waziri huyo alieleza mafanikio
ya Wizara kwa kuwasiliana na Kampuni ya DSTV ambayo inarusha matangazo yake
karibu duniani kote, ambapo hatua za kufungua ofisi hapa Zanzibar zimekamilika
ambapo hivi sasa wanafanya matengenezo ya jengo la ofisi lililopo Mlandege
Unguja hatua ambayo pia itopanua soko la ajira katika tasnia ya utangazaji.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment