RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza haja kwa Wizara
ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kuendelea kuviimarisha vivutio vya utalii
kutokana na utajiri mkubwa uliopo wa vivutio hivyo hapa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo katika ukumbi wa Ikulu
ndogo Kibweni mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii
na Mambo ya Kale wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa
Wizara hiyo kwa Kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar imebarikiwa
kuwa na vivutio vingi vya kitalii ikifananishwa na nchi za ukanda wa Afrika
Mashariki hivyo kuna kila sababu ya kuviimarisha vivutio hivyo ili vizidi kuwavutia
watalii wa ndani na nje ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itaendelea kutoa msukumo kupitia Wizara
yake hiyo ili kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika na kuendelea kuleta tija
sambamba na kuongeza pato la taifa.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa
Wizara hiyo kuendeleza michezo ambayo itakuwa ndio kivutio cha watalii hasa ile
ambayo ilikuwepo siku za nyuma na kuweza kuitangaza Zanzibar kwa kiasi kikubwa
ukiwemo mchezo wa Gofu.
Akieleza mafanikio yaliopatikana Zanzibar, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na kuimarisha kwa uchumi wake mafanikio
makubwa yameweza kupatikana na kuipelekea Serikali kutekeleza miradi kadhaa
ambayo haipo kwenye Bajeti wala kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ukiwemo ujenzi
wa barabara na daraja la Kibondemzungu, Mwanakwerekwe na miradi mengineyo.
Mapema Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Idd, alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kufanya utaratibu na kuweka
ratiba maalumu kwa viongozi ili kwenda kuangalia vivutio vya kitalii vikiwemo
mapango na magofu.
Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia na hasa kwa
viongozi kuzidi kuendelea kuutangaza utalii wa Zanzibar kwa kutoa taarifa na
maelezo pale wanapokuwa nje ya nchi ambapo huweza kuzungumza na viongozi pamoja
na watu mbali mbali wakiwemo wawekezaji wa sekta ya utalii.
Nae Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud
Thabit Kombo alieleza hatua za kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na
kuimarisha maeneo ya kihistoria ya Fukuchani kwa upande wa Unguja na Mkamandume
kwa Pemba ambapo Wizara imefanikiwa kuyaimarisha maeneo hayo.
Alieleza kuwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa
eneo la Mkamandume umeanza kwa kutengeneza njia maalum ya bahari ambayo ilikuwa
ikitumika kwa njia ya kusafirishia jahazi njia ambayo ikitokea katika usawa wa
bahari hadi kwenye jengo la Mkamandume pamoja na ujenzi wa kuta za ngome hiyo.
Aidha, Wizara imelifanyia matengenezo makubwa
jengo la ngome ya kihistoria ya Wareno ya Fukuchani kwa kuzijenga upya kuta za
jengo hilo, kuweka milango na madirisha mapya, kuliezeka paa la bati pamoja na
kujenga kuta zinazozizunguka ngome hiyo.
Waziri Kombo alisisitiza kuwa maeneo hayo ya
kihistoria yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kukusanya mapato ya fedha za
kigeni ambapo wageni kutoka mataifa mbali mbali hupata fursa ya kuyatembelea.
Sambamba na hayo, Waziri Kombo alieleza hatua
zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo katika kutekeleza Mradi wa kuimarisha
Utalii kwa Wote ambao unahusu ujenzi wa kituo cha utalii katika eneo la Bi
Khole huko Bungi Wilaya ya Kati Unguja.
Alieleza kuwa Mkandarasi wa ujenzi huo
ameshapatikana ambaye ni Quality Building Contractor na tayari ameshaanza hatua
za ujenzi ambapo katika awamu ya kwanza ya mradi huo unategemea kutekeleza
shughuli za uwekaji sawa muonekano wa ardhi pamoja na kuweka njia katika eneo.
Aliongeza kuwa shughuli nyengine ni kutengeneza
bustani, kujenga mikahawa 10 kwa ajili ya utoaji wa huduma za vyakula mbali
mbali, ujenzi wa baraza za kukalia zenye uwezo wa kukalia watu 2000 kwa wakati
mmoja pamoja na ujenzi wa vyoo na maegesho ya gari.
Waziri huyo anaehusika na sekta ya utalii alieleza
kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza vivutio vya utalii, kuimarisha utalii
wa ndani na kimataifa pamoja na kuongeza ajira kwa jamii hasa vijana.
Aidha, uongozi wa Wizara ulieleza juhudi
zinazochukuliwa na Shirika la Magazeti ya Serikali katika kuhakikisha linatoa
habari zake ndani na nje ya nchi kwa kutumia jumla ya mitandao sita ya kijamii
ikiwemo Twitter, Istagram, Youtube, Facebook, Tovuti pamoja na gazeti mtandao
(Online).
Pia, uongozi huo wa Wizara ya Habari, Utalii na
Mambo ya Kale ulieleza namna juhudi za makusudi zinavyochukuliwa katika
kuuimarisha utalii hasa katika kisiwa cha Pemba ambapo ulieleza kuwa kwa
kipindi hichi wageni wengi wamekuwa wakikitembelea.
Aidha, uongozi huo ulieleza ujio wa meli maalum ya
kitalii kisiwani humo ambayo itakuwa na watalii kutoka maeneo mbali mbali
duniani watakaofika kwa ajili ya kuangalia vivutio kadhaa vilivyopo kisiwani
humo.
Uongozi wa Wizara hiyo pia, ulieleza kuwa miongoni
mwa vivutio kadhaa vilivyopo kisiwani Pemba vikiwemo vile vya asili pia,
watalii wengi wamekuwa wakivutiwa na chumba cha hoteli ya Mantarif ambacho kiko
chini ya bahari.
Sambamba na hayo, uongozi huo pia ulitoa pongezi
na shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa maelekezo,busara na hekima aliyonayo katika
kuwaongoza hatua ambayo imekuwa chachu ya mafanikio katika Wizara hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment