Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa Shirikisho la Jamuhuri ya Brazil Nchini Tanzania Mhe Antonio Augusto Cesar alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu
mkubwa wa kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Brazil kwa maslahi
ya wananchi wa nchi mbili hizo.
Dk. Shein amesema hayo leo
Ikulu mjini hapa, wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Shirikisho la
Jamhuri ya Brazil nchini Tanzania Antonio Augusto Cesar aliefika kwa ajili ya kujitambulisha.
Dk. Shein alisema Zanzibar
na Brazil zina uhusiano wa muda mrefu na zimekuwa zikishirikiana katika masuala
mbali mbali ya maendeleo, ikiwemo ya kiuchumi na kijamii
Alisema pamoja na nchi
hizo kutofautiana kwa ukubwa wa eneo na kupatikana katika Mabara tofauti,
zimekuwa zikishirikiana kwa karibu, huku Zanzibar ikiwa na mengi ya kujifunza kutoka
nchi hiyo, ikiwemo suala la kuiendeleza sekta ya Utalii.
Alisema Zanzibar ambayo
kabla ilikuwa ikilitegemea zao la Karafuu kuendesha uchumi wake, imebarikiwa
kuwa na vivutio na rasilimali kadhaa za Utalii hususan kupitia uchumi wa bahari
(Blue Economy), eneo ambalo kuna mambo mengi ya kufanya.
Dk. Shein alimweleza
Balozi huyo dhamira ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya kuvutia Wawekezaji kutoka Brazil katika nyanja mbali
mbali, ikiwemo sekta ya Utalii, ili kuimarisha uchumi wake.
Alisema pamoja na kuwepo
sheria na miundombinu iliyo bora kuelekea maeneo ya Uwekezaji, Zanzibar
inajivunia kwa kuwepo hali ya amani na
usalama muda wote hivyo kutoa fursa adhimu ya kuwekeza.
Aidha, Dk. Shein
alimhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar na Tanzania ujumla zina matarajio ya
kupata maendeleo makubwa kutokana na kuwa na viongozi imara, hatua aliyosema
imeziwezesha nchi hizo kufikia miaka 55 ya Muungano wake ikiwa salama.
“Leo hii ni miaka 55
tangu nchi hizi kuungana, Muungano umebaki imara. nchi nyingi zimejaribu kufanya hivyo, lakini
zimeshindwa”, alisema Dk. Shein.
Katika hatua nyengine Dk.
Shein alipongeza azma ya Brazil kuendelea kushirikana na Zanzibar katika suala
zima la kuimarisha huduma za Afya, ili kuleta ustawi wa wananchi.
Nae, Balozi wa Shirikisho
la Jamuhuri ya Brazil nchini Tanzania, Antonio Augusto Cesar alimweleza Dk.
Shein hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Uongozi wa nchi yake katika kuleta
ustawi wa kiuchumi, kisiasa na kijamii
kwa wananchi wa Taifa hilo.
Alisema Brazil imeazimia
kuendeleza ushirikano na Zanzibar katika nyanja mbali mbali ikiwemo sekta ya
Afya ili kuimarisha afya za wananchi.
Aidha, alisema kuna
umuhimu mkubwa wa kuendeleza mashirikiano na Zanzibar ili kuimarisha sekta ya
Utalii, akisifia mandhari na vivutio mbali mbali vilivyopo hapa nchini, na
hivyo akaahidi kutumia fursa iliyiopo kuvutia Wawekezaji kutoka nchini Brazil.
Wakati huo huo, Balozi wa
Heshima wa Shirikisho la Jamuhuri ya Brazil hapa Zanzibar, Abdulsamad
Abdurahman, amesema zaidi ya vijana 37 kutoka Zanzibar na wachache kutoka Tanzania Bara,
wanatarajiwa kushiriki katika mkutano maalum wa Kibiashara utakalofanyika
nchini Brazil, baadae mwezi ujao.
Alisema vijana hao
walioandaliwa watashiriki katika mkutano huo wa siku kumi utakaoanza Juni, 28,
2019 kwa ajili ya kuitangaza Zanzibar kupitia sekta za Utalii, Biashara,
Kilimo, pamoja na viungo ikiwemo Karafuu.
Alisema kupitia mkutano
huo utakaowashirikisha wadau mbali mbali
kutoka Chamber na Incubator za huko, viijana hao wataangazia fursa za kuvutia
wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali pamoja na kufanya
ubia na wawekezaji wa huko.
“Hivi sasa tayari kuna
wawekezaji wapatao sita kutoka Brazil waliowekeza hapa, tunafanya juhudi ili
kuvutia wawekezaji wengi zaidi”, alisema.
Aidha, Balozi huyo
alisema wawapo nchini Brazil, ujumbe huo utatembelea miji ya Brasilia, Sao
Paolo pamoja na Rio de Geneiro, ambako utapata fursa ya kujionea shughulli mbali
mbali za viwanda vidogo vidogo, Mafuta na Gesi, mashamba ya ufugaji kuku, utengenezaji
wa na uhifadhi ya nyama ya ngombe na sekta
yenginezo.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com.
No comments:
Post a Comment