Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wafanyakazi wa Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara Zanzibar (UUB) alipofanya ziara kutembelea Vifaa Vipya vya Ujenzi wa Barabara Zanzibar katika Kituo cha UUB Kibele Wilaya ya Kati Unguja, kushoto Waziri wa Ujenzi Mawasiliani na Usafirishaji Zanzibar Mhe.Dr. Sira Ubwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe Mohammed Ahmed Salum.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi
kuwa ahadi zote zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za
kutengeneza barabara kubwa na ndogo zitatekelezwa baada ya vifaa vipya na vya
kisasa kuwasili.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua vifaa vipya na vya kisasa vya
kutengenezea barabara ukiwemo mtambo wa lami wa digitali ambavyo vimenunuliwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka nje ya nchi ambavyo kwa hivi sasa
vimewekwa Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake mara
baada ya kukagua vifaa hivyo na kupata maelezo kutoka uongozi wa wa Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji Dk. Shein alieleza kuwa ni azma ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kutekeleza ahadi zake za ujenzi wa barabara ambazo
iliahidi kwa wananchi.
Alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa ahadi kwa wananchi za ujenzi wa barabara mbali
mbali za Unguja na Pemba lakini nyengine zilijengwa na nyengine bado
hazijafanyiwa ujenzi kutokana na uhaba na ukosefu wa viifaa vya kutosha vya ujenzi
wa barabara.
Alieleza kuwa kutokana
na maamuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kununua vifaa vyake wenyewe
kutakuwa ndio mkombozi mkubwa wa kutekeleza ahadi hiyo kwa azma ya utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa ndani ya kipindi chake cha uongozi atahakikisha ahadi
zilizotolewa za ujenzi wa barabara zinatekelezwa baada ya Serikali kununua
vifaa hivyo vipya na vya kisasa vya digitali.
“ Furaha yangu ni
kwamba kazi hii itakamilika na hatimae tutajenga wenyewe, kwa fedha zetu
wenyewe na wataalamu wetu wenyewe kwa vifaa vyetu wenyewe na kwa nguvu zetu
wenyewe kwani azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kufanya
hivyo”,alisisitiza Rais Dk. Shein.
Aliwaeleza wafanyakazi
wa Wizara hiyo kuwa vifaa hivyo ambavyo vimewasili kwa awamu ni vipya, na
vimeagizwa kutoka Kampuni zenye sifa duniani kutoka nchi za Itali, Brazil, Ujerumani,
Japan pamoja na India hivyo ni vyema
vikatunzwa na kuenziwa ili visijeonekana ni vya mtumba hasa ikizingatiwa kuwa
gharama yake ni kubwa kwani vifaa hivyo vimegharimu TZS Bilioni 10.3.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kuhakikisha barabara zilizoharibika
zinatengenezwa ikiwa ni pamoja na kuwekwa viraka kwa baadhi ya barabara
zilizofanya mashimo ambayo wakati mwengine husababisha foleni ya gari na hata
kusababisha ajali.
Hata hivyo, Rais Dk.
Shein amekubali rai ya uongozi wa Wizara hiyo ya kujengwa uzio katika eneo hilo
ili kuhakikisha usalama wa vifaa hivyo sambamba na kukabidhiwa hati miliki ya
eneo hilo hasa ikizingatiwa kuwa eneo lote katika sehemu hiyo ni la Serikali.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliuagiza uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha inawawekea mazingira
mazuri wafanyakazi wake sambamba na kuwaandaa watalamu kwa lengo la kuendesha
na kusimamia Idara hiyo ya Barabara ili kuepusha kukimbiwa na wataalamu ambao
hufuata maslahi kwenye Kampuni binafsi.
Alieleza kuwa Serikali
inahitaji wataalamu hivyo jitihada zifanyike za kuwaajiri vijana waliomaliza
masomo ya kada zote kwani kwa wale waliofika kiwango cha Shahada hata za Sheria
basi wanafundishika katika fani hiyo ya ujenzi kwani jambo la muhimu ni kuwapa
mafunzo japo ya muda mfupi juu ya fani hiyo kwani wanafundishika.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuzishukuru na kuzipongeza Kampuni binafsi ambazo zilishirikiana
na Serikali wakati palipokuwa na uhaba na ukosefu wa vifaa kwa kujenga na
kukarabati barabara kadhaa hapa nchini na kuzitaka ziendelee licha ya kuwa hivi
sasa Serikali tayari imeshapata vifaa vyake.
Alieleza kuwa kupata
vifaa hivyo isiwe ndio mwisho wa mashirikiano kwani tayari kumeshajengwa
mahusiano na udugu kati ya Serikali na Kampuni hizo zilizojenga barabara kwa upande
wa Unguja na Pemba.
Aliongeza kuwa kwa
vile ujenzi wa barabara unagharimu fedha nyingi hivyo, ujenzi wa barabara iwapo
utaendeshwa na Idara husika ya Barabara gharama hizo zitapungua na kuleta afuweni
kubwa kwani hilo ndio lengo la Serikali na ndio maana imeamua kununua vifaa
hivyo kwa ajili ya kujenga barabara za Unguja na Pemba.
Nae Waziri wa Wizara
ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dk. Sira Ubwa Mwamboya alieleza furaha
aliyonayo kwa ujio wa vifaa hivyo na kusema kuwa hatua hiyo itasaidia na kutoa
nafasi kubwa kwa ujenzi wa barabara ambao ulizorota kutokana na uhaba na
ukosefu wa vifaa.
Alisema kuwa kununuliwa kwa vifaa hivyo, kutafikisha
asilimia mia moja ya uwezekano wa ujenzi
wa barabara mbali mbali hapa nchini ambapo pia, zitajengwa kwa wakati sambamba
na kufikia malengo ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara kutokana na ahadi zake anazozitoa.
Mapema Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Mustafa Aboud Jumbe aliemueleza Rais Dk. Shein aina za vifaa
viliyonunuliwa na vile ambayo vimeshawasili ukiwemo mtambo wa kupikia lami
kutoka nchini Brazil, makatapila, paver,
magrader,mabuldoza, excaveta,gari ya kuwekea lami ya maji, vijiko, na vifaa vyenginevyo
huku akiahidi ujio wa gari 10 kutoka nchini India mnamo Julai mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo
alieleza kuwa ununuzi wa vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya TZS Bilioni
10.3 unatokana na agizo alilolitoa Rais Dk. Shein mnamo Septemba 2016 wakati
alipofanya ziara ya kutembelea sehemu hiyo na kuona mtambo wa kupikia lami
pamoja na vifaa ambavyo vilikuwa vimechakaa.
Alieleza kuwa vifaa
hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa barabara ya Charawe na
Ukongoroni ambao tayari umeshaanza pamoja na ujenzi wa barabara ya Ole-Kengeja
unaoendelea huku akieleza kuwa tayari lami tani 400 kati ya tani 1000
imeshawasili.
Pamoja na hayo, Katibu
Jumbe alisema kuwa wataalamu wa kuja kutoa mafunzo juu ya uendeshaji wa vifaa
hivyo wanatarajiwa kuwasili Julai 2 mwaka huu 2019 na kueleza kuwa vifaa hivyo
nusu vitapelekwa Pemba na nusu vitabaki Unguja kwa kuendelea na shughuli za
ujenzi wa barabara huku akiomba kupatiwa hati miliki sambamba na ujenzi wa uzio
katika eneo hilo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment