Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Ujumbe wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation ya Jijini Dar es Salaam walipofika Ikulu Zanzibar kujitambulishwa, ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Sheikh Nurdin Kishki kushoto na Sheikh Suleiman Khamis Habib.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk.
Ali Mohamed Shein ameitaka taasisi ya Al – Hikma Foundation kuzingatia kiwango chenye uwiano kwa washiriki
wa Zanzibar, pale inapoandaa mashindano ya kuhifadhisha Qur-ani.
Alhaj
Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa taasisi
ya Al-Hikma Foundation kutoka Jijini Dar es Salaam, uliofika kujitambulisha
pamoja na kumuombea dua ya kumtakia maisha mema na uongozi bora.
Alhaj
Dk. Shein alisema kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi hiyo pale inapofanya shughuli
zake, hususan zinazoambatana na mashindano ya kuhifadhi Qur-ani pamoja na upatikanaji
wa fursa mbali mbali zikiwemo za kijamii, kuzingatia umuhimu wa kuongeza
kiwango cha kuishirikisha Zanzibar kwani kiwango cha sasa ni kidogo.
Alisema
amevutiwa sana na juhudi zinazofanywa na Taasisi hiyo na kubainisha mafanikio
yaliofikiwa kuwa ni matunda yanayotokana na kuwepo kwa viongozi bora, sambamba
na kuitaka kuendelea kuitumia kikamilifu fursa ya kuwa na mlezi mahiri Alhadj
Ali Hassan Mwinyi.
Aidha,
Alhaj Dk. Shein alisema usimamizi wa mashindano ya kuhifadhisha Qur-an kunakofanywa
na taasisi hiyo ni njia bora katika kuwajenga watoto kupenda kuhifadhi qur-an,
akibainisha umuhimu wa jambo hilo kwa msingi kuwa ni lazima Qur-an ihifadhiwe
na kuendelezwa.
Alisema
Mwenyezi Mungu ameahidi kuihifadhi Qur-an, hivyo ni jukumu la waumini wanaume na wanawake pamoja na
watoto kuisoma kikamilifu.
Alisema
Zanzibar ina historia ya kuwa chemchem ya dini ya kiislamu na kueleza kuwa kwa
nyakati tofauti imefanikiwa kutowa wanazuoni
mashuhuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo akatowa wito kwa watu
mbali mbali kuja kujifunza masuala ya dini ya kiislamu.
Alhaj
Dk. Shein aliipongeza taasisi hiyo kwa kufikisha miaka 22 tangu kuanzishwa
kwake, sambamba na kutekeleza jukumu lake la kusimamia mashindano ya Qur-an kwa
kipindi chote hicho.
Aidha,
akaipongeza taasisi hiyo kwa hatua mbali mbali inazozichukuwa katika
uimarishaji wa huduma za kijamii, ikiwemo uchimbaji wa visima na ujenzi wa
misikiti, hatua aliyosema ni amali nzuri na muhimu kwa jamii ya Watanzania.
Nae,
Mwenyekiti wa Al-hikma Foundation, Sheikh Nurdin Muhammed Ahmeid Al-Ahdal
‘Kishki’ alisema Qur-an ni msingi wa dini na yule mwenye kuifahamu huwa mcha
Mungu na raia mwema.
Alisema
Kamati iliyoundwa kwa ajili ya kuhifadhisha Qur-an kutoka taasisi hiyo, pamoja
na shughuli nyengine pia inajishughulisha na suala la kuhubiri amani nchini kwa
kuzingatia umuhimu wake kama ulivyobainishwa
katika dini ya kiislamu.
Aliipongeza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa Rais Dk. Shein kwa kutoa fursa
kwa wananchi wake katika kuendeleza dini, hatua inayoliwezesha Taifa kupata
matokeo mazuri katika mashindano mbali mbali ya kitaifa na kimataifa.
Vile
vile, Mwenyekiti wa Al-Hikma Foundation Zanzibar, Omar Hussein Mussa,
alimhakikishia Alhaj Dk. Shein kuwa taasisi hiyo inafanya kazi zake kwa kuzingatia pande mbili
za Muungano, akibainisha hekma zake zimeiwezesha kufanikisha shughuli hizo kwa
uwazi na mafanikio makubwa.
Alitoa
rai kwa serikali kuipatia eneo la ujenzi taasisi hiyo, ili iweze kuanzisha rasmi
Tawi lake hapa Zanzibar, hatua itakayofungua milango ya uendelezaji wa huduma mbali
mbali za kijamii zinazofanywa na taasisi hiyo, kama vile uchimbaji wa visima,
ujenzi wa misikiti nauanzishaji wa skuli za msingi na sekondari.
Aidha,
Mwenyekiti huyo alimueleza Alhaj Dk. Shein kuwa kupitia Jumuiya ya Kuhifadhisha
Quran Zanzibar , watoto kadhaa wamepata mafanikio ya kuwa washindi katika mashindano
tofauti ya kuhifadhi Quran yaliofanyika katika nchi mbali mbali Barani Afrika.
Ujumbe
huo wa watu 13 uliosimamia mashindano ya Kimataifa ya kuhifadhisha Qur-an yaliyofanyika
hivi karibuni jijini Dar es Salaam, ulikuwa Zanzibar kwa takriban wiki moja kwa
mapumziko baada ya kufanikisha vyema mashindano hayo, ambapo mtoto Shamsuddin
Hussein Ali (21) kutoka Zanzibar alikuwa mshindi wa tatu.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment