Habari za Punde

‘Shahzada wa Stallion Attorneys atoa neno kwa wanafunzi Zanzibar University’Wahitimu watarajiwa katika fani ya sheria chuo kikuu cha Zanzibar University (ZU) wametakiwa kujituma bila kuchoka katika kufikia malengo yao waliojiwekea.
Kauli hio ilitolewa na Shehzada Walli ambae ni mwanzilishi wa kampuni inayojihusisha na maswala ya kisheria ya Stallion Attorneys    wakati alipokua akizungumza na wanafunzi hao katika sherehe maalumu ya usiku wa sheria.
Alisema wapo baadhi ya wanafunzi wengi hushindwa kufikia malengo yao kutokana na kukata tamaa kufuatia changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Hata hivyo alisema uwepo wa changamoto  hizo kwa wanafunzi zikiwemo za ajira hawapaswi kurudi nyuma badala yake wanatakiwa kuongeza bidii zaidi katika kuonesha uwezo waliojifunza wakiwa darasani.
‘’Mimi binafsi wakati namaliza chuo kikuu ni mara kadhaa niliomba kujitolea sehemu mbali mbali nilikosa fursa lakini sikuwahi kukata tamaa nilihangaika kila leo ili nitimize ndoto zangu na hatimae leo hii kwa kiasi fulani nimefanikiwa’’aliongezea.
Aidha aiwataka wahitimu hao watarajiwa kufahamu kuwa hakuna safari rahisi katika kusaka mafanikio na kwamba wanalazimika kujituma zaidi sambamba na kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya mafanikio yao.
Awali Jaji wa mahakama kuu Zanzibar Mshibe Ali Bakari alisema elimu ni jambo muhimu na kwamba wanafunzi hao hawana budi kuzingatia yale yote waliojifunza wakiwa darasani kwa muda wote.
Alisema elimu ya sheria inatokana na uwezo binafsi atatakaokua nao mtu katika utendaji wake wa kazi na kama hatakua  na ufanisi anaweza kushindwa kufanya kazi hio hata kama akiwa na elimu ya kutosha.
Kutokana na mazingira hayo aliwashauri wanafunzi hao kuzingatia zaidi elimu ya kivitendo wakitambua kwamba Taifa linawategemea katika upatikanaji wa haki pindi watakapoanza kazi kwenye maeneo mbali mbali ndani na nje ya Tanzania.
‘’Leo hii mimi nina heshimika kila mahala ninapokwenda kwa sababu ya kuekeza vijana wengi kwenye taaluma hii ya sheria binafsi najivunia hili na nataka muwe kama nilivo mimi au zaidi yangu’’aliongezea.
Aidha Jaji Mshbe alitoa wito kwa wanafunzi hao watakapomaliza masomo yao kutambua kuwa wana wajibu mkubwa wa kuthamini wateja wao iwapo wataajiriwa kwenye kampuni au watajiajiri wenyewe kwa lengo la kuwatunza na kuwaenzi wateja wao.
Nae Mkuu wa kitivo cha sheria kutoka chuo kikuu cha Zanzibar University Dkt,Makame Mohamed alisema chuo hicho kitaendelea kuwajengea uwezo wanafunzi wanaosoma sheria kwa lengo la kuhakikisha wanauzika katika soko la ajira.
Alieza kuwa kwa miaka mingi chuo chao kimekua kikitoa kozi hio ambayo anaamini ni bora zaidi na ndio maana wanafunzi kutoka maeneo mbali mbali ya nje na ndani ya Tanzania hujiunga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.