Habari za Punde

Vilabu Ligi Kuu vyapatiwa leseni

NA MWAJUMA JUMA


VILABU 11 kati ya 16 vinavyotarajiwa kushiriki ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2019/2020  huku vitatu kati ya hivyo vikipata Leseni za Kimataifa nane wamepata leseni za ndani.

Vilabu hivyo vilikabidhiwa leseni zao hizo jana na Meneja wa Club Leseni, Suleiman Shaaba huko katika ukumbi wa VIP Amaan mjini Zanzibar.

Alisema kuwa vilabu ambavyo vimekabidhiwa leseni hizo ni vile ambavyo vimekaguliwa huku vilabu vitano vilivyokuwa havijapata vinatarajiwa kufanyiwa ukaguzi kabla ya kuanza ligi.

Alisema kuwa katika ukaguzi huo waliangalia mambo mengi lakini mambo makuu mawili ya msingi yalikuwa ni umiliki wa vilabu pamoja na uendeshaji wa program za vijana.

Hata hivyo alisema kuwa pamoja na kwamba vilabu hivyo vimekabidhiwa leseni zao lakini haimainishi kwamba ndio vimekamilika kwa asilimia 100, bali kuna mambo ambayo wamekubaliana waende kuyafanyia marekebisho.

Alivitaja vilabu hivyo vilivyokabidhiwa leseni ni JKU, KMKM, Malindi, Selem View, Jamhuri, Chipkizi, Kipanga, KVZ, Zimamoto, Mafunzo na Polisi, huku vilabu vitatu kati ya hivyo 11 vilivyopata leseni za kimataifa ni  JKU, Malindi na KMKM.

Vilabu ambavyo bado havijapatiwa Leseni ni Jang’ombe Boys, Chuoni, Mlandege, Mwenge na timu moja kutoka Pemba ambayo haijajulikana kutokana na ligi yao ya daraja la kwanza ya kutafuta timu itakayopanda kutomalizika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.