Habari za Punde

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) Yaimarisha Utendaji wake Kwa Kutumia TEHAMA

Na Frank Mvungi- MAELEZO                                                                                                          
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imetajwa kuongeza tija katika utendaji wake kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)katika huduma zake kwa wadau.

Akizungumza katika kipindi cha “TUNATEKELEZA”   Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Prof. Lazaro Busagali amesema kuwa Tume hiyo imeimarisha utoaji wa huduma zake kwa wadau kuanzia katika utoaji wa vibali na huduma zote ikiwemo za maabara.

“ Tunaipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuiwezesha Tume kuwa na  Ofisi za Kanda 21 na asilimia 90 ya vibali vinatolewa ndani ya siku moja kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu yetu ya kutolea huduma “ Alisisitiza Prof. Busagali

Akifafanua Prof. Busagali amesema kuwa Teknolojia ya nyuklia ikitumika vizuri inaleta matokeo chanya katika jamii kwa kuwa ni muhimu katika kuchangia maendeleo kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo.

Akizungumzia utendaji wa Tume hiyo Prof. Busagali amesema kuwa moja ya majukumu ya Tume ni kuhakikisha kuwa Taasisi zote zinazotumia mionzi katika kutoa huduma zake zikiwemo Hospitali zinazingatia matumizi bora ya mionzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia  sekta hiyo.

Aliongeza kuwa Tume hiyo imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika Taasisi zote zinazotumia mionzi   hapa nchini ili kuhakikisha kuwa watumiaji wa huduma za Taasisi husika wako salama dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.

Aidha alifafanua kuwa, Tume imejiwekea utaratibu wa kutoa  elimu kwa wananchi na wadau ili kuepuka matumizi ya mionzi yasiyozingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepusha madhara ya mionzi hiyo pale inapotumika vibaya.

“Serikali ya Awamu ya Tano imetuwezesha kuwa na maabara ya kisasa na pia wadau wetu ambao ni  Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kwa kutuwezesha kupata vifaa vya kisasa vya maabara yetu” Alisisitiza Prof. Busagali.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ni Taasisi ya Serikali inayosomamia na kuratibu masuala yote yanayohusu mionzi hapa nchini ikiwa na maabara ya kisasa ambayo ni mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.