Habari za Punde

Ushiriki wa wazawa katika uvuvi wa bahari kuu bado ni mdogo

 Mwajuma Juma

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania Dkt. Islam Seif Salum amesema kuwa ushiriki wa wazawa katika uvuvi wa bahari kuu ni mdogo ikilinganishwa na kampuni zinazofanya  uvuvi kutoka nje ya Nchi.

Alisema kuwa hatua hiyo inachangiwa na gharama kubwa katika uwekezaji wa uvuvi wa bahari kuu.


Hayo aliyaeleza alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa Waandishi wa Habari juu ya sheria na maendeleo ya Uvuvi wa Bahari Kuu kupitia Mradi wa usimamizi uvuvi wa Kanda ya Kusini  magharibi mwa bahari kuu "SWIOFish" katika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini Mjini Zanzibar.

Hata hivyo alisema kuwa wamekuwa wakijaribu kuhamasisha wazawa kujiingiza katika uwekezaji huo ingawa kuna gharama kubwa, ikiwemo kuandaa Sera nzuri hasa katika uwekezaji wa ndani.

Hivyo aliwataka waandishi  wa  Habari Zanzibar wametakiwa kuimarisha mashirikiano na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania ili wananchi wapate nafasi ya kufahamu faida za kiuchumi zinazopatikana kupitia Uvuvi wa Bahari kuu Nchini.

Dkt. Islam amesema vyombo vya Habari vina jukumu kubwa la kuwaelimisha wananchi kuhusu uchumi wa bluu kupitia rasilimali za bahari ukiwemo uvuvi wa bahari kuu pamoja na uhifadhi wa mazingira ya baharini.

Amesema pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia uvuvi wa bahari Kuu Tanzania bado sekta hiyo inakabiliwa na tatizo la upungufu wa vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri pamoja na vituo vya barafu vya kuhifadhi samaki katika maeneo ya bandari Tanzania bara na Zanzibar.

Mradi wa uvuvi wa bahari kuu umeanzishwa mwaka 2015 chini ya Ufadhili wa benki ya dunia na unamaliza muda wake mwaka 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.