Habari za Punde

Wakazi wa Makete Watakiwa Kuanzisha Kampuni ya Uwekezaji-TIC


Na. Grace Semfuko, MAELEZO.24/06/2019
Wito umetolewa kwa wakazi wa Makete waishio Jijini Dar es Salaam, kuanzisha Kampuni ya Uwekezaji na Mfuko wa Maendeleo wa Wilaya hiyo utakaoangalia fursa za kiuchumi zinazopatikana Makete, Mkoani Njombe, ili kukuza pato lao na Taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Chama cha Maendeleo Makete (MDA) uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Bwana Mwambe akasema,  fursa ya kuanzisha kampuni na mfuko utawawezesha wakazi hao kununua hisa na umiliki pamoja na kuwapa fursa za kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zitakazotolewa ikiwa ni sehemu ya kuitangaza Wilaya hiyo kwa wawekezaji wengine. 

 “Makete mna fursa nyingi za uwekezaji, kuna kilimo cha ngano, pareto, viazi, matunda na mbogamboga, pia mnayo madini mbalimbali, mnao utalii wa ndege na maua kule kwenye hifadhi ya Kituro, ndugu zangu, uwekezaji katika sekta hizo inawezekana kabisa, pia mnayo ardhi ya kutosha, ni muhimu muwekeze nyumbani” alisema Mwambe.

Mwambe aliwataka wakazi hao kushirikiana na kuongeza nguvu katika kutangaza fursa na vivutio vya utalii vilivyopo katika Wilaya hiyo ambayo imebarikiwa kuwa na hali nzuri ya hewa ya kuweza kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

“Ndugu zangu uwekezaji unawezekana sana Makete, mna ardhi yenye rutuba,mna hali nzuri ya hewa, umoja wenu ni bora zaidi kuliko utengano, nawaomba sana muungane na muanzishe Mfuko na Kampuni ya Wanamakete vitakayokuwa na malengo ya kuiletea maendeleo Wilaya ya yenu”alisema Mwambe.

Aidha aliongeza Wilaya hiyo inao uwezo mkubwa wa kuzalisha ngano lakini bidhaa hiyo kwa asilimia kubwa inaagizwa kutoka nje ya nchi na kuwataka ikutafakari hilo ili kuzalisha ngano  kwa wingi.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Makete,  Bw. Burton Sinene alisema kwa sasa Wilaya hiyo inahitaji wawekezaji katika kiwanda cha kutengeneza njiti za meno (bamboo toothpick) kutokana na kuwepo kwa zao la  mianzi,  bidhaa ambayo kwa kiwango kikubwa inaagizwa nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya mezani wakati wa kula.

Katika majadiliano ya kikao hicho wakazi hao waliiomba Serikali izidi kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuweza kusafirisha mazao toka mashambani kwenda kwenye masoko mbalimbali, suala ambalo pia litawavutia wawekezaji wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.