Habari za Punde

Kituo Kipya cha Daladala cha Kijangwani kuanza kutumika 01/09/2019

 Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Ayoub Mohamed Mahmoud akionyesha na kuelezea Ramani ya Kituo kipya cha Daladala cha Kijagwani kitachoanza kutumika rasmin tarehe 1-Septemba Mwaka huu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) huko Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar .
Ramani inayoonyesha Mchoro mzima wa Kituo kipya cha Daladala cha Kijagwani kitakavokuwa baada ya kukamilika.  
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.

Na Mwashungi Tahir,   Maelezo      
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud ametangaza utaratibu wa kuanza kutumika kwa kituo  cha daladala cha muda cha Kijangwani ambacho kinatarajia kutumika rasmi Septemba mosi mwaka huu.
Akitangaza utaratibu huo mbele ya waandishi wa habari Ofisini kwake Vuga,Mkuu huyo wa Mkoa alisema  taratibu zote zishakamilika  kituo hicho kitakuwa na milango miwili ya kuingilia na kutokea ambapo mlango mmoja utatumika na daladala zinazoelekea njia ya Bububu na Amani.
Vile vile mlango mwingine utatumika na daladala zinazoelekea njia ya Magomeni,Jang'ombe na Uwanja wa Ndege na kwamba utaratibu huo umekubalika katika kikao cha pamoja kati ya serikali ya Mkoa huo,Idaara ya Utoaji wa Leseni,Jeshi la Polisi na Idara  ya Mipango miji na vijiji.
"Daladala zote zinazofanya kazi  mjini hazitabadilisha roti zake na zitaendelea na ruti zake za sasa  naomba niliweke vizuri kuwa kila daladala itaendelea kama ilivyosasa na isije ikitokea watu wakatumia  mwanya huu kukatisha ruti njiani wakapandisha nauli kiholela,"alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha  Ayoub alisema  ikifika Septemba mosi mwaka huu kituo kilichokuwa kikitumika gari za kuelekea Bububu, Michenzani na cha Baraza la Wawakilishi la zamani  havitatumika tena na kwamba daladala zote za vituo hivyo vitatumia kituo hicho cha muda cha Kijangwani.
"Kwa maneno haya hakutakuwa na kituo kingine cha mjini ambacho kitatumika na daladala hizo na kwamba watatumia vituo vifupi kwa kusimama kidogo kwa ajili ya kupakia abiria na si kwenda kuegesha daladala hizo,"alisema Ayoub.
Hata hivyo  alisema hakutakuwa na utaratibu wa kuwepo kwa pikipiki ambazo zitafanya shughuli za kibiashara za kuwasafirisha abiria ndani ya kituo hicho na kwamba uamuzi huo unatokana na kuwa usafiri huo haujawa  rasmi visiwani Zanzibar.

"Wataruhusiwa kutokana na kuwa mimi sipangii jambo ambalo halipo kisheria na nimesema kuwa zitakaporasimishwa kuwa usafiri rasmi nitawapangia lakini leo ninajua jambo hili ni kinyume cha sheria hivyo hatuwezi kurasimisha kitu kuwa rasmi ,"alisema
Pia  ametoa onyo kwa madereva na matingo kwamba wakileta ukaidi agizo la Serikali  kwa kuvunja sheria zilizowekwa hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Aliongeza kuwa kituo hicho kishakamilisha taratibu zote za kisheria ambapo Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na usafirsihaji ambaye mwenye dhamana ya kutangaza kuwa kituo hicho kinatumika rasmi kwa daladala ameshakamilisha utaratibu wake na kwamba alimwandikia  Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala la Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ,Haji Omar Kheir kuanza kutumika kituo hicho.
"Waziri huyu ndiye aliyenitaka mimi nitangaze kuanza rasmi kutumika Septemba mosi mwaka huu hivyo ninaomba niwatangazie kuwa kituo hichi ndicho kitakuwa rasmi na dereva atakayeshindwa kutekeleza agizo hili jeshi la polisi litawachukuliwa hatua,"alisema Mkuu wa Mkoa huyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.