Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Baloxzi Seif Ali Iddi Ziarani Mkoani Shinyanga

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akifungua pazia kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la Tawi la CCM la Bukondamoyo katika Jimbo la Kahama Mjini.


Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Chama cha Mapinduzi hakina hiyana ya kumkataa  kujiunga na chama hicho Mwanachama wa chama chochote cha Siasa Nchini aliyeamua  kufuata Sera na Ilani ya CCM inayoendelea kutekelezeka kwa kasi kubwa.
Alisema CCM wakati wote inapinga ubaguzi, choyo na ubinafsi na ndio maana Mwanachama au Kiongozi yeyote wa Upinzani anapoamua kujiunga na Chama  hicho hatengwi katika kupewa dhamana ya uongozi kama ana uwezo, nidhamu na maarifa ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi unaoleta faida kwa Umma.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Jengo Jipya la Tawi la CCM Bukondamoyo wakati akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini kwenye Mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Jumanne Kishimba wa kuelezea Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Alisema  ipo mifano hai  ya kutokuwepo na ubaguzi ndani ya CCM inayoendelea kushuhudiwa na Wananchi walio wengi  ya baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Upinzani walioamua kurejea Chama cha Mapinduzi  kupewa Madaraka makubwa  ndani ya Chama pamoja na Serikali.
Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Kichama aliwapongeza Wananchi wa Vyama vya Upinzani katika Wilaya ya Kahama walioamua kurudi nyumbani CCM baada ya kuridhika na Kazi kubwa inayofanywa na Serikali Kuu katika Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi iliyolenga kustawisha Maisha ya Watanzania wote.
Balozi Seif aliwakumbusha Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuzingatia jukumu lao ya kuwatumikia Wananchi katika Majimbo yao wakielewa kwamba wao ndio Viunganishi kati ya Serikali na Wananchi kwenye Majimbo yao katika kuwaletea Maendeleo.
Alitahadharisha kwamba  Uongozi wa Chama hautasita kumuweka pembeni wakati wa mchakato wa kura za Maoni Mbunge au Mwakilishi yeyote asiyepita Jimboni na badala yake kusubiri ziara za Viongozi wa Kitaifa ndio waonekane katika maeneo hayo.
Akizungumzia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar  Balozi Seif   aliwakumbusha Watanzania  wa kizazi cha sasa kusoma Historia na dhamira halisi ya uwepo wa Muungano huo uliorasimishwa Aprili 26 Mwaka 1964  lakini tayari ulishawaunganisha ndugu wa Damu wa Mataifa Mawili huru kwa karne kadhaa zilizopita.
Alisema wapo baadhi ya Wananchi wakiwemo  pia Viongozi wanashindwa kutafsiri dhamira sahihi ya Muungano huo ulioridhiwa na Waasisi wa Taifa hili kwa uwepo wa Serikali mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif  alisema Waasisi hao Marehemu Mzee Abeid Aman Karume na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walizingatia uwepo wa Serikali hizo mbili kwa kuepuka fikra na mawazo ya upande Mmoja ungeumeza upande mwengine wa Muungano.
Akiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa Jimbo la  Kamaha Mjini ndani ya Kipindi cha Miaka Minne Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Jumanne Kishimba alisema huduma za Kijamii tayari zimeshaimarika ndani ya kipindi hicho na kutoa afueni kwa Wananchi wake.
Mh. Jumanne alizieleza huduma hizo kuwa ni pamoja na  Sekta ya Afya kwa ujenzi wa Hospitali Mpya ndani ya Manispaa ya Mji, Sekta ya Elimu kwa ujenzi wa Mdarasa na Daghalia pamoja na Maji safi na salama zilizofikia zaidi ya Asilimia 90%.
Hata hivyo Mbunge huyo wa Jimbo Kahama Mjini alisema ipo changamoto kubwa inayokwaza upungufu wa nguvu kazi za uzalishaji kutokana na ukosefu wa Bara bara ya Lami
Alisema Bara bara  za ndani limekuwa tatizo kubwa kwenye Jimbo hilo hasa katika Manispaa ya Mji  ambayo kwa sasa imekuwa na ongezeko kubwa la harakati za kimaisha  pamoja na idadi kubwa ya Watu.
Mapema Balozi Seif  alilizindua Rasmi jengo jipya la Skuli ya Sekondari ya Uloa katika Jimbo la Ushetu ambayo imeonyesha mfano mkubwa katika ufaulu  mzuri wa Wanafunzi wake katika Mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha Nne kuingia Kidato cha Tano na Sita.
Akizungumza na Wanafunzi, Walimu, Wazazi na Wana  CCM  wa Jimbo la Ushetu mara baada ya kazi hiyo kwenye Mkutano wa Mbunge wa Jimbo hilo wa kuelezea Utekelezaji wa Ilani ya CCM,  Balozi Seif  alisema wanafunzi wanaposoma vyema uhimili wa Taifa unakuwa katika mikono salama Kitaaluma.
Balozi Seif alisema uongozi wa Serikali wakati wote unahitaji kusimamiwa vyema  na Watu au kizazi kilichobobea katika kusaka Elimu. Hivyo  mfano ulioonyeshwa na Uloa pamoja na Majimbo mengine utasaidia kufanikisha  vyema azma ya Taifa kuelekeza nguvu zake kwenye Elimu kutokana na juhudi za kutandika Miundombinu.
Katika kuunga mkono jitihada za Uongozi wa Skuli ya Sekondari ya Uloa Balozi Seif aliahidi kusaidia Kompyuta Tatu na Printa zake pamoja na Seti za Jezi kwa Timu za Wanaume na Wanawake wa Skuli hiyo.
Naye kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Rajab Telak alisema kipaumbele cha Mkoa huo kwa sasa ni Elimu kutokana na muamko mkubwa ulichomoza ndani ya Mkoa huo kufuatia matokeo ya ufaulu wa Wanafunzi wake unaopanda kila Mwaka.
Mh. Zainab akiahidi kusaidia nguvu za ujenzi wa Nyumba za Walimu wa Skuli hiyo kwa kuchangia Saruji Paketi 50 alisema mila potovu lazima ziishe ndani ya Mkoa kupitia uimarishaji huo wa Sekta ya Elimu.
Akitoa Taarifa fupi ya Ujenzi wa Jengo hilo la Skuli ya Sekondari ya Uloa iliyoanza na Wanmafunzi 90 na sasa wapo Mia 774, Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Mwalim Mchunywa Shaaban alisema jengo hilo Jipya lina Madarasa Matatu, Bweni na vyoo vyake vinavyojitegemea.
Mwalimu  Shaaban alisema ujenzi huo umekuja kutokana na uhaba wa madarasa uliopelekea kuleta usumbufu kwa Wanafunzi, jambo ambalo Uongozi wa Skuli ulichukuwa jitihada za uamuzi wa ujenzi zilizoungwa Mkono na Serikali Kuu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Alisema jitihada hizo zimeleta faraja kubwa kwa Wanafunzi waliohamasika na kuipaisha Skuli hiyo kuendelea kufanya vyema katika ufaulu wao kwenye Mitihani ya Taifa ya Kidatu cha Nne.
Mwalimu Mkuu huyo wa Skuli ya Sekondari ya Uloa aliushukuru na kuupongeza Uongozi wa Serikali Kuu, Mkoa, Wilaya, Halmashauri pamoja na Jimbo la Ushetu kwa jitihada kubwa zinazochukuliwa za kuimarisha miundombinu ya Elimu kwenye maeneo yao.
Hata hivyo Mwalimu Shaaban alisema ipo changamoto  kubwa ya upatikanaji wa huduma ya Maji safi na Salama Skulini hapo tatizo linalowapa muda mwingi Wanafunzi wake kutafuta huduma hiyo na kupunguza muda wao wa kuwepo Madarasani.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe.Balozi Seif  akibadilishana mawazo na Viongozi wa Mkoa wa Shinyanga ndani ya Tawi la Bukondamoyo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Tawi hilo.
Viongozi wa Chama cha Demokrasia ya Maendeleo {CHADEMA} wa Serikali ya Mtaa wa Kahama Mjini walioamua kurejea CCM wakivishwa sare za CCM Kwenye Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini.
Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama Balozi Seif Ali Iddi akimpongeza Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kahama Mjini  Chadema Bibi Marry Izak Sumni aliyerejea CCM.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akiwa sambamba na Mkuu wa Mkoa Shinyanga Mh. Zainab Rajab Relak akilikagua moja ya Darasa kwenye Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Uloa Jimbo la Ushetu baada ya kulizindua Rasmi.
Balozi Seif  akilijaribu umadhubuti wake Dawati ndani ya darasa la Jengo la Skuli ya Sekondari ya Uloa Jimboni Ushetu baada ya kulizindua Rasmi akiwa katika ziara ya Siku Tano Mkoani Shinyanga kama Mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Balozi Seif  akiujaribu ubao wa kusomea ndani ya Darasa la Skuli ya Sekondari ya Uloa katika Jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga.
Kikundi cha Utamaduni katika halmashauri ya Ushetu kikitoa burdani ya wimbo maalum wa utunzaji wa mazingira kwenye Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Ushetu wa kuwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya kipindi cha Miaka Minne.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.