Na. Mwandishi Wetu, MAELEZO, DAR ES SALAA, 8.8.2019
RAIS wa Zanzibar, Dkt. Ali
Mohamed Shein amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
kuweka mkazo wa matumizi ya bidhaa zake na wataalamu wake wa ndani katika kutengeneza
fursa za ajira na masoko ndani ya ukanda huo ili kukuza sekta za viwanda na
biashara ndani ya jumuiya hiyo.
Akizungumza katika hafla ya
kufunga Maadhimisho na Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda katika Nchi za SADC leo
Alhamisi (Agosti 8, 2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Shein alisema umefika
wakati kwa mataifa hayo kuzalisha bidhaa bora zenye kuweza kuleta ushindani
katika masoko ya ndani na nje ya Jumuiya hiyo.
Dkt. Shein alisema Mataifa ya
SADC hayana budi kutumia fursa ya maonesho hayo katika kutangaza fursa za ujuzi
na ubunifu kwa kuzalisha na kutengeneza
mtandao wa imara wa mawasiliano baina ya Nchi hizo na kuweza kuwa na soko la
pamoja litakalowawezesha kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wa Mataifa
hayo.
Kwa mujibu wa Dkt. Shein
aliongeza kuwa ili kufikia malengo ya uzalishaji wa bidhaa bora za viwandani ni
wajibu wa Serikali zote kutengeneza mtandao imara wa miundombonu ikiwemo
matumizi ya tekonolojia ya habari na mawasiliano kwa kuunda mikakati ya pamoja ya
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Jumuiya hiyo uliolenga katika kuimarisha sekta
ya viwanda ndani ya jumuiya hiyo.
“Hatujakataa mchango wa wataalamu
na bidhaa za nje, lakini chako ni chako na mwenzako si chako, hivyo hakikunyima
usikasirike, ni wakati wetu sasa kuweka mkazo katika kutegemea wataalamu wetu
na teknolojia zetu katika uzalishaji wa bidhaa zetu” alisema Dkt. Shein.
Aliongeza kuwa Nchi za Jumuiya
hiyo hazina budi kutumia fursa za Maonesho na midahalo mbalimbali ya wataalamu
inayojadiliwa katika Mikutano ya Jumuiya hiyo ili kuweza kubaini changamoto na
hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa ili kuiwezesha jumuiya hiyo kupiga
hatua kubwa za Maendeleo ikiwemo kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wake.
Akifafanua zaidi Dkt. Shein
aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar
zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali katika uboreshaji wa miundombinu ya miradi
ya Maendeleo ambayo imekuwa kichocheo kikubwa cha fursa za ajira kwa vijana
sambamba na kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika
uchumi wa viwanda.
Akitolea mfano, Dkt. Shein
alitaja baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa
(SGR), ujenzi wa viwanda vikubwa, vya
kati na vidogo ambavyo kwa pamoja vinaifanya Tanzania kuwa kielelezo cha mfano
katika Nchi za SADC katika utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo ya Viwanda ndani
ya Jumuiya hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa
Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema maonesho hayo yamekuwa chachu
na kipimo kwa Nchi za SADC kutekeleza ajenda yake ya Viwanda, kwa kuwa makundi
mbalimbali ya wazalishaji, wafanyabiashara na watoa huduma wameonesha udhubutu
wa kufikia malengo hayo katika Nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Aliongeza kuwa jumla ya washiriki
5352 walishiriki katika midahalo mbalimbali ikiwemo Nchi SADC 14, taasisi za
umma 64, viwanda 64, taasisi za kifedha 35, ambazo zote kwa pamoja zilitoa
uzoefu na kuweza kuongeza fursa ya masoko na kuweza kuimarisha mitandao ya
mawasiliano baina yao.
Naye Waziri wa Habari, Utalii na
Malikale wa Zanzibar, Mahmoud Thabit
Kombo alisema ili kufikia malengo ya Mpango Mkakati wa Jumuiya hiyo, nchi za
SADC hazina budi kutoa na kuweka mkazo wa ushiriki wa sekta binafsi katika
ujenzi wa uchumi shirikishi, kwa kuwa ushirikiano baina ya sekta hiyo na
serikali utawezesha kutengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi katika mataifa
hayo.
Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya
hiyo, Dkt. Stagomena Tax, aliisifu Serikali ya Tanzania kwa kuwa mfano ndani ya
Jumuiya hiyo katika eneo la ujenzi wa uchumi wa viwanda, na hivyo kuzitaka nchi
nyingine kuiga mfano huo ili kuweza kuleta mtangamano ndani ya Nchi wanachama.
Aliongeza kuwa ili kuweza kujenga
uchumi jumuishi kwa wananchi ndani ya jumuiya hiyo, Sekretarieti ya jumuiya
hiyo itaelekeza nguvu yake katika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa bidhaa
zilizopo ndani ya jumuiya hiyo, kwani bila miundombinu ya uhakika hakutoweza
kuwa na mazingira wezeshi ya kuwasaidia wananchi ikiwemo kuondoa vikwazo vya
kibiashara ndani ya jumuiya hiyo.
No comments:
Post a Comment