Habari za Punde

Uwanja wa michezo Bungi waekewa taa

Na Salum Vuai



MWAKILISHI na Mbunge wa jimbo la Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, wameandika historia baada ya kupeleka taa katika uwanja wa michezo wa kijiji cha Bungi jimboni humo.

Simai Mohammed Said ambaye ni Mwakilishi wa jimbo hilo, amesema wakati wa uzinduzi wa taa hizo juzi usiku, kuwa akishirikiana na Mbunge Khalifa Salum Suleiman, wametumia shilingi 21,500,000 kwa mradi huo.

Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wanakijiji cha Bungi na maeneo jirani, Said alisema lengo la mpango huo ni kuuwezesha uwanja wa Bungi kutumika wakati wa usiku kwa michezo mbalimbali hasa ligi za mpira wa miguu na michezo mingine.

Alisema hatua hiyo itachochea vijana kupenda na kushiriki zaidi katika michezo ambayo ni miongoni mwa mambo yanayosisitizwa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ikiwa pia sehemu ya ajira.

Naye Mbunge Khalifa Salum alieleza kuwa, mbali na michezo, hatua hiyo itawapa wananchi fursa ya kuutumia uwanja kwa shughuli za kijamii ikiwemo sherehe za sikukuu, na burudani ambazo kwa kawaida hufanyika hadi usiku pamoja na matukio ya kiserikali.

“Mara nyengine hali ya hewa nyakati za mchana inakuwa ya joto kali na kuwapa shida wanamichezo, hivyo kucheza usiku kutawarahisishia kuonesha uwezo wao na hivyo kunogesha burudani ya michezo,” alieleza mbunge huyo.

Suleiman alisema wataendelea kubuni njia nyengine zaidi za kuimarisha michezo katika vijijini vyote vilivyomo ndani ya jimbo hilo ili kuibua vipaji vya vijana na kuwatoa kwenye makundi hatarishi.  

Uzinduzi wa taa hizo ulitanguliwa na mchezo wa fainali ya mpira wa miguu mashindano ya ‘Chado Ndondo Cup’, ambapo timu ya Black Americans iliitungua Makonvoi magoli 3-2 na kunyakua dume la ng’ombe lenye thamani ya shilingi 1,200,000 kutoka kwa Mbunge na Mwakilishi wa jimbo hilo.

Wananchi wa Bungi wamewapongeza viongozi wao hao kwa uamuzi wa kuweka taa kwenye uwanja huo, wakisema zitaupandisha hadhi na kuweza kutumika hata kwa mechi za ligi kuu ya soka Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho, Sheha wa shehia ya Bungi Vuai Ramadhani Vuai, alisema wameipokea hatua hiyo kwa furaha na kuahidi kuzitunza taa hizo ili kuepusha uharibifu kwa kuongeza ulinzi shirikishi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.