Habari za Punde

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Akutana na Ujumbe Kutoka Ubalozi wa Ujerumani,GIZ

Ujumbe wa wageni kutoka Ubalozi wa Ujerumani na Shirika la GIZ kuanzia kushoto Julia Haumy wa Ubalozini, Vera Rosendahl kutoka Wizara ya Maendeleo nchini Ujerumani, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la GIZ, Dk Mike Falken, N. Grigolelt, Andrea H. kutoka Ubalozi wa Ujerumani na Richard Shaba kutoka Ubalozi huo Ofisi ya Dodoma wakiwa katika kikao hicho.  
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Joseph Malongo (kulia) akimsikiliza Ofisa kutoka Ubalozi wa Ujerumani Julia Haumy (hayupo pichani) wakati akizungumzia kuhusu Mradi wa Kuboresha upatikanaji wa nishati endelevu. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Faraja Ngerageza na Mhandisi Juma Limbe kutoka Idara ya Mazingira.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Joseph Malongo leo Septemba 12, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Ujerumani na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ofisini kwake Jijini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine Serikali ya Ujerumani kupitia GIZ wameingia makubaliano kuhusu Mradi wa Mkataba wa kuboresha upatikanaji wa nishati endelevu katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma.

Mradi huo utakaogharimu Euro milioni 3 kwa kipindi cha miaka mitatu unatarajiwa kuboresha mazingira katika kambi za wakimbizi za Nduta, Nyarugusu na Mtendeli kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo upandaji wa miti.

Pia mradi huo utahusisha utoaji wa teknolojia ya umeme jua kwa matumizi ya kupikia, hivyo kupunguza matumizi ya kuni na mkaa unaotokana na ukataji miti kitendo ambacho kinasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Tukio hilo limehudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Faraja Ngerageza, Mhandisi Juma Limbe kutoka Idara ya Mazingira pamoja Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la GIZ, Dk Mike Falken  na Ujumbe wake kutoka ubalozini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.